Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

KINANA, CCM WANAPANGA NJAMA ZA KUMVUA LISSU UBUNGE MAHAKAMANI!!!

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA
KINANA, CCM WANAPANGA NJAMA ZA KUMVUA LISSU UBUNGE MAHAKAMANI!!!
Dar es Salaam, 31 Mei 2013...
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani vikali njama za Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kufufua kesi ya uchaguzi dhidi ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mh. Tundu Lissu. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Wilbroad Slaa amedai kwamba CHADEMA imekamata nyaraka zinazoonyesha kwamba Katibu Mkuu wa CCM Kinana amewaelekeza waliowakuwa mawakili wa makada wa CCM waliomfungulia Mh. Lissu kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka 2010 wafungue rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyotupilia mbali kesi ya makada hao wa CCM dhidi ya Lissu. Kesi ya Mahakama Kuu ilitupiliwa mbali tarehe 27 Aprili mwaka jana.
Dr. Slaa alisema kwamba lengo la njama za Kinana na CCM ni kuhakikisha kwamba Mh. Lissu anafutiwa Ubunge ili asiweze kushiriki katika mchakato wa Katiba Mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba litakalojadili na kupitisha rasimu ya Katiba Mpya baadaye mwaka huu. Dr. Slaa alisema: “Kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge, Mheshimiwa Lissu amekuwa mwiba mkali kwa CCM na Serikali yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Amefumbua macho ya mamilioni ya Watanzania kuhusu masuala makubwa ya kikatiba na kisheria kwa hoja zake Bungeni. Uelewa wake mpana wa masuala hayo na wa Kanuni za Bunge umekuwa kikwazo kikubwa kwa CCM na Serikali yake pamoja na uongozi wa Bunge kupitisha mambo yao kinyume cha sheria, Kanuni za Bunge na maslahi ya nchi yetu. Uwepo wake ndani ya Bunge na ujasiri wake katika kutetea hoja mbali mbali umemzuia Spika wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge kuwaonea Wabunge wa Upinzani na hasa CHADEMA. Mtu huyu amekuwa adui mkubwa wa CCM ndio maana Kinana anataka aondolewe Bungeni ili asiwepo kabisa katika mjadala wa Katiba Mpya Bungeni.”
Kwa mujibu wa Dr. Slaa, mara baada ya Mh. Lissu kuwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 3 mwezi huu ambapo aliishambulia Tume ya Mabadiliko ya Katiba na CCM kwa kuvuruga mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa lengo la kuhakikisha Mabaraza hayo yanakuwa ya wanachama wa CCM tu, Kinana alimwita wakili wa kujitegemea Godfrey Wassonga wa kampuni ya mawakili ya Wassonga Associates Advocates ya mjini Dodoma na kumwelekeza afungue rufaa dhidi ya Lissu katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania haraka iwezekanavyo. Siku nne baadaye yaani tarehe 7 Mei, 2013, Wakili Wassonga alifungua rufaa hiyo katika Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania mjini Dodoma.
Ijapokuwa rufaa hiyo inaonyesha kufunguliwa na Shabani Itambu Selema na Paschal Marcel Hallu waliokuwa walalamikaji katika kesi iliyotupwa na Mahakama Kuu, Dr. Slaa alidai kwamba watu hao hawahusiki kwa namna yoyote ile na kufunguliwa kwa rufaa hiyo.
“CCM na mawakili wao wanawatumia tu wanakijiji hawa bila hata kuwapa taarifa au kuwashirikisha kwa namna nyingine yoyote. Huyu Shabani Itambu Selema amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote juu ya kufunguliwa kwa rufaa hiyo. Hawakutoa maagizo yoyote kwa Wakili Wassonga kufungua rufaa kwa niaba yao dhidi ya Lissu; hawajamruhusu Wakili huyo kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu iliyoridhika kwamba uchaguzi wa Mbunge Lissu ulikuwa halali; hawajamlipa Wakili Wassonga kwa ajili hiyo. Huyu Wakili anafunguaje kesi au rufaa bila kuambiwa au kulipwa na ‘wateja’ wake? Kama huku sio kukosa maadili ya kiuwakili ni kitu gani?”, amehoji Dr. Slaa.
Kuhusu ushiriki wa Kinana katika sakata hilo, Dr. Slaa alisema kwamba mara baada ya rufaa hiyo kufunguliwa, Wakili Wassonga alimwandikia Katibu Mkuu huyo wa CCM barua yenye kumbu kumbu Na. NO/KM/CCM/01/2013 kwa ajili ya “MADAI YA MALIPO YA AWALI YA SHAURI LA RUFAA KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI SHABANI ITAMBU SELEMA NA MWENZAKE DHIDI YA MH. TUNDU LISSU.” Barua hiyo inamkumbusha Kinana juu ya ‘makubaliano’ kati ya Wassonga Associates Advocates na CCM kuhusu kusimamia kesi ya wanachama hao wa CCM dhidi ya Mh. Lissu ambayo baadae ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu.
“Baada ya shauri husika nilipata maelekezo kutoka kwa wanasheria wa CCM kwamba tukate rufaa Mahakama ya Rufaa kazi ambayo tumekamilisha.” Wakili Wassonga anamweleza Kinana “... katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM Singida Mkoa na hawakumalizia malipo.” Barua hiyo imeambatana na hati ya madai ya malipo (invoice) kwa ajili ya ‘malipo ya awali’ ya shilingi milioni mbili.
Dr. Slaa alidai kwamba kazi ya Lissu na wabunge wa CHADEMA ndani ya Bunge inawatisha CCM na Serikali yake ndio maana sasa Kinana anataka Lissu aenguliwe kwa kutumia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. “CCM inatapatapa, Bungeni hapakaliki kwa sababu ya hoja za Lissu na Wabunge wengine wa CHADEMA. Kila siku Bunge linaahirishwa ili kukwepa mijadala mikubwa juu ya matukio muhimu yanayoisibu nchi yetu.
Njama za kuizima CHADEMA kwa kuipunguzia muda wa kuzungumza Bungeni zimeshindikana; mikakati ya kuvuruga hoja za CHADEMA kwa kuingilia hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani na kutaka sehemu za hotuba hizo zifutwe zimegonga mwamba; vitisho vya Spika Makinda na Naibu Spika Ndugai kuwasimamisha wabunge wetu hazijafua dafu. Sasa tuna taarifa kwamba Kinana anataka kuwahonga majaji ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania mamilioni ya fedha ili wamfutie Kamanda wetu Lissu ubunge. Naye atashindwa pia.”
Akizungumzia hati ya kiapo ya Shabani Itambu Selema ambaye alihama CCM na kujiunga na CHADEMA baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu mwaka jana, Dr. Slaa amesema:
“Tutaishangaa sana Mahakama ya Rufaa kama itaisikiliza rufaa hiyo hata baada ya aliyekuwa mhusika wa kesi ya msingi kusema kwa kiapo kwamba yeye na mwenzake hawajakata rufaa bali ni mambo ya Kinana na CCM yake!”
Dr. Slaa alisema itakuwa ajabu kwa Mahakama ya Rufaa kusikiliza rufaa iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Mahakama Kuu ilipotupilia mbali kesi ya msingi. “Kwa mujibu wa kifungu cha 115 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mahakama ya Rufaa inatakiwa kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu rufaa ilipofunguliwa. Huyu Kinana na CCM yake wamesubiri mwaka umepita tangu Mahakama Kuu ilipokataa kufuta matokeo ya Lissu ndio wafungue rufaa. Kama huku sio kukanyaga spirit ya Sheria hiyo ni kitu gani?”, amehoji Dr. Slaa.
Aliongeza kuwa katika kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Mh. Godbless Lema aliyekuwa anashtakiwa na wanaCCM pia, Mahakama ya Rufaa ilipiga marufuku wapiga kura ambao hawakunyimwa haki zao za kupiga kura kufungua malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
“Hata wino wa Mahakama ya Rufaa katika hukumu ya Lema haujakauka Kinana na CCM yake wanataka Mahakama ya Rufaa iyale matapishi yake kwa kusikiliza rufaa ya wapiga kura wanaodai kwa kiapo kwamba walielekezwa na wakubwa wao katika CCM kufungua kesi iliyokataliwa na Mahakama Kuu na sasa rufaa imefunguliwa kwa maelekezo ya Kinana bila hata wao kujulishwa au kushirikishwa kwa namna yoyote ile," amesema Dkt. Slaa.
Dr. Slaa alisema kwamba rufaa ya sasa inathibitisha kauli inayodaiwa kutolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya Tundu Lissu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo Kikwete alidaiwa kuwaambia wanaCCM mjini Singida kwamba ni afadhali Dr. Slaa achaguliwe kuwa Rais kuliko Tundu Lissu kuwa Mbunge.
“Kwa kazi zake ndani na nje ya Bunge Lissu amethibitisha umahiri na uzalendo wake kwa Tanzania na kwa chama chetu. Ametetea wabunge na viongozi wetu dhidi ya njama za CCM kuwachafua kwa kuwafungulia mashtaka ya uongo mahakamani; ametetea Watanzania kila mahali nchini, na ameelimisha wananchi kwa hoja zake Bungeni. Ni mmoja wa Wabunge hodari, jasiri na wachapa kazi katika Bunge hili. Huyu ndiye Mbunge ambaye Kinana na CCM wanataka aondolewe Bungeni kwa mbinu za kishetani za aina hii. Hatutakubali na tunawataka Watanzania wasikubali!”
Rufaa dhidi ya Lissu bado haijapatiwa namba ya usajili licha ya kwamba imeshalipiwa ada ya kuifungulia na tayari imeshapokelewa na Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dodoma. Aidha, rufaa hiyo haijapangiwa majaji wa kuisikiliza wala tarehe ya kusikilizwa kwake haijapangwa.
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO