Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

NEC: MAAMUZI YA RUFAA ZA MAPINGAMIZI YA WAGOMBEA WA UBUNGE NA UDIWANI KATIKA UCHAGUZI MDOGO


Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ilipokea Rufaa moja ya kupinga Uteuzi wa Mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mdogo wa Bunge Jimbo la Dimani – Zanzibar.
Rufaa hiyo ilikatwa na Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bwana Juma Ali Juma akipinga Maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani aliyemthibitisha Mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF) Bwana Abdul Razak Khatib Ramadhani kuwa ni mgombea halali.
Rufaa hiyo ilikuwa na sababu mbili ambazo ni:- (i) Hakurudisha Fomu za Uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea Ubunge. Katika kikao chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016, Tume imepitia Rufaa hiyo na kuona sababu zilizotolewa na mkata Rufaa hazina nguvu ya kisheria, kwa kuwa, Mgombea wa CUF amerudisha Fomu za Uteuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Pia, Fomu zake za Uteuzi zimesainiwa na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Kwa mantiki hiyo, Tume imekubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani – Zanzibar. Hivyo, Mgombea wa CUF amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali na aendelee na kampeni za kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.
Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imepokea Rufaa tatu; kutoka Kata ya Kijichi – Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani na Kata ya Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Mkoa wa Dodoma.
Kata ya Misugusugu Halmashauri ya Mji Kibaha, Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM Bwana Bogasi Hussen Ramadhani.
Katika Kata ya Kijichi, Rufaa ilikuwa ni ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas dhidi ya mgombea wa CHADEMA Bwana Fredrick Felician Rugaimukamu.
Kata ya Ihumwa Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Magawa Edward Juma dhidi ya maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi.Tume katika kikao chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016 imepitia Rufaa zote na imeamua ifuatavyo:


Rufaa ya mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi katika Kata ya Misugusugu Halmashauri ya Mji Kibaha na ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas katika Kata ya Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na zimekataliwa. Hivyo, Tume inakubaliana na Maamuzi ya Wasimamzi wa Uchaguzi wa Halmashauri hizo na wagombea waendelee na Kampeni kwa mujibu wa Ratiba.


Kuhusu Rufaa ya Mgombea wa CHADEMA kutoka Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tume, imepokea barua ya Msimamizi wa Uchaguzi, Manispaa ya Dodoma, ikiwa imeambatishwa na barua ya Mgombea wa CHADEMA kuiondoa Rufaa yake na kwamba anakubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ambayo yalimuengua. Pia, leo Tume imepokea barua za kujitoa Ugombea za wagombea wa CHADEMA na ACT - WAZALENDO katika Kata ya Ihumwa. Kwa maana hiyo Rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa CHADEMA Kata ya Ihumwa imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa na amejitoa ugombea kabla haijasikilizwa.


Mwisho, Tume inavisisitiza Vyama vya Siasa, Wagombea na Wananchi wote wa maeneo yenye Uchaguzi Mdogo kufanya Kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi.
Imetolewa na:-
Jaji Mkuu (Mst. Znz) Hamid M. Hamid
MAKAMU MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
30/12/2016
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO