Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, akisikiliza maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi. Kushoto kwa Noela ni mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices Moshi, Farida Makame. Wengine pichani ni washiriki wa kikundi hicho. Uzinduzi wa jiko hilo lililotengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa Green Voices ulifanyika hivi karibuni mjini Moshi.
Jiko la umeme-jua ambalo limetengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices Tanzania kwa ajili ya kikundi cha akinamama wa TAWOCA Moshi. Jiko hilo linafaa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira.
Wanakikundi wa TAWOCA Green Voices Moshi wakihakikisha jinsi joto la jua linavyosaidia kupika kwa kutumia jiko la umeme-jua. Kushoto ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, Robert George, pamoja na akinamama wakisikiliza maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi.
Mhandisi Noela Byabachwezi, mwenye kofia kulia, akionyesha kwa vitendo jinsi jiko la umeme-jua linavyofanya kazi.
Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, Robert George – kulia – akisikiliza maelezo mbalimbali ya akinamama wa TAWOCA Green Voices Moshi kabla ya kuzindua jiko la umeme-jua.
Picha ya pamoja.
VIUNGA vya ukumbi wa Aroma mjini Moshi vimesheheni akinamama wengi katika siku hii ya Jumamosi, kama ilivyo kawaida kwa siku kama hiyo, ambapo wote wanaonekana kuwa na nyuso za furaha kutokana na mijadala inayoendelea.
Lakini tofauti na Jumamosi nyingine ambapo akinamama wa kikundi cha Wamama wa Kahawa ambao ni wanachama wa Tanzania Women Coffee Association - TAWOCA mjini humo kujadili masuala mbalimbali ya ujasiriamali, siku hii inaonekana kuwa ya tofauti kwa sababu licha ya idadi ya akinamama kuongezeka, lakini kuna tukio kubwa na muhimu ambalo limewakutanisha.
"Leo tunazindua rasmi jiko la umeme-jua, yaani parabolic solar cooker, ambalo kupitia udhamini wa mradi wa akinamama wa Green Voices, hatimaye limeweza kupatikana baada ya jithada za miezi kadhaa," ndivyo anavyoanza kuelezea Farida Makame, mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices wa kikundi hicho, huku akionyesha kifaa kinachofanana na dish kama la satellite ambacho katikati yake kumewekwa sufuria inayong’aa kama taa kubwa ya umeme.
Anasema kwamba, jiko hilo linaweza kupika kila aina ya chakula kwa kutumia mionzi ya jua ya moja kwa moja bila kuathiri mazingira.
"Kwa kutumia jiko hili maana yake huhitaji kutafuta mkaa wala kuni, hivyo kuokoa misitu ambayo inateketea kila siku kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutafuta nishati ya kupikia," anaongeza.
Farida, ambaye pamoja na akinamama wengine 14 – wakiwemo wanahabari watano wanawake – walipatiwa mafunzo ya takriban miezi miwili jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu wa 2016, anasema kwamba lengo la kubuni na kutengeneza jiko hilo la umeme-jua ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira.
Anaeleza kwamba, haikuwa kazi rahisi kwake kukamilisha ubunifu wake, wazo ambalo aliliwasilisha akiwa mafunzoni, na kwamba ndiyo maana mradi wake umechelewa kutokana na kuhitaji teknolojia zaidi.
"Tumeanzisha huu mradi baada ya kukaa na akinamama wa TAWOCA na kuwauliza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao, moja ya changamoto ni upatikanaji wa kuni na mkaa, gesi na umeme.
"Kwahiyo tukaangalia kama kuna njia mbadala ambayo akinamama wanaweza kuitumia na ikawa nafuu na pia kiafya, kwa sababu njia ya kutumia umeme-jua ina manufaa sana kiafya, kwa hiyo tukaungana na wenzetu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini, CAMARTEC, kwa sababu ndio watafiti wa mashine na zana za kilimo, ili kutengeneza jiko hili linalotumia nishati ya jua," anasema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi anasema imekuwa ni fursa kubwa kwao kufanya kazi na mradi wa Green Voices, kwani wameweza kutengeneza kwa mara ya kwanza jiko hilo ambalo limewapa hamasa wahandisi wa kituo hicho kuliboresha zaidi kwani linaonekana kuwa na manufaa makubwa.
Anakiri kwamba, ingawa wanabuni teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengeneza majiko na makaushio yanayotumia umeme-jua, lakini hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa kituo hicho kutengeneza jiko linalotumia nguvu ya jua moja kwa moja.
"Hivi sasa tunafanya utafiti kama tunaweza kulitengeneza dogo lakini lenye nguvu au kutengeneza jiko linaloweza kukunjwa na kuhifadhiwa kirahisi kwa sababu hili ni kubwa na inakuwa shida ikiwa mtu hana nafasi kubwa ya kuhifadhia," anasema Mhandisi Noela.
Akizungumzia kuhusu ufanisi wake, Noela anasema kwamba, jiko hilo ni rafiki mkubwa wa mazingira na lina uwezo mkubwa wa kupika na hata kuoka vyakula vya aina zote ikiwa tu kutakuwepo na jua la kutosha.
Kwa maeneo kame na yenye jua kali kama mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na hata Dar es Salaam, jiko hilo linafaa sana kutumiwa bila shida, anaongeza mhandisi huyo.
Aidha, anafafanua kwamba, jiko hilo linaweza kupika chakula kwa ajili ya watu wengi na kwamba ni jukumu la jamii kugeukia matumizi ya jiko hilo lisilotumia mafuta wala nishati nyingine kwa sababu siyo tu linapunguza gharama, lakini pia linaokoa misitu kwa vile miti haitakatwa ikiwa watakuwa wanalitumia.
"Jambo jingine la muhimu ni kwamba, upikaji kwa kutumia jiko la umeme-jua mara nyingi hufanyika nje na katika mazingira ambayo yanahitaji matumizi madogo ya mafuta na kuni, au hatari ya ajali za moto na inaokoa afya za wanajamii, hususan akinamama pamoja na kuyalinda mazingira yetu," anaongeza Mhandisi Noela.
"Kama unavyoliona, jiko hili limetengenezwa kwa vifaa maalum vikiwemo vioo, ambavyo vinang’aa na kuakisi mwanga wa jua, vimepangwa kitaalam na mwanga huu unapoakisiwa unakwenda moja kwa moja kwenye sufuria ambayo kutokana na joto lake, chakula chochote kinachopikwa kinaiva bila wasiwasi wowote. Kama jua litakuwepo la kutosha, joto linalozalishwa na jiko hili linaweza kufikia hadi nyuzijoto 400 °C."
Kwa mujibu wa mhandisi huyo, vyakula vinavyopikwa kwa kutumia jiko la aina hiyo ni vyema vikawa katika maumbile madogo ili kusaidia kuiva haraka na kwamba muda wa chakula kuiva unategemea na vifaa unavyotumia, kiwango cha jua, na kiasi cha chakula kinachopikwa.
Faida kubwa za utumiaji wa jiko la umeme-jua zinatajwa kwamba, mbali ya kuokoa mazingira, ni uwezo wa kupika vyakula vigumu, kukaanga nyama, kupika supu, kuoka mikate na kuchemsha maji kwa muda mfupi.
Hata hivyo, jiko hilo linahitaji zaidi uwepo wa jua, kwani ndiyo chanzo cha joto linalofaa kupikia.
Mmoja wa wanakikundi hicho, Esther Moshi, amesema kupatikana kwa jiko hilo kutawakomboa wanawake wengi ambao mara nyingi ndio wanaokabiliwa na changamoto ya utafutaji wa nishati za kupikia kama kuni na mkaa.
"Tunashukuru mradi wa Green Voices kwa sababu unalenga kumkomboa mwanamke kutokana na adha ya upatikanaji wa nishati ya kupikia, kama majiko haya yatatengenezwa kwa wingi na kila familia kulipata, hakika yatakuwa mkombozi na yatasaidia kuokoa mazingira, " anasema.
Fatima Aziz Faraji ni mwenyekiti wa Chama cha TAWOCA, amesema ni muhimu kwa wanawake kuzidisha umoja wa vikundi ili waweze kusonga mbele na akaupongeza mradi huo kwamba utakuwa mkombozi si kwa wanawake pekee, bali jamii nzima.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, ameupongeza mradi wa Green Voices pamoja na akinamama hao na akahimiza kuwa, ni vyema kutumia teknolojia ambazo ni rafiki wa mazingira.
Amesema akinamama ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati za kupikia, na kwamba ndio wanaoongoza kupata madhara kiafya, hasa wanapotumia mkaa na kuni.
"Jitihada hizi za wenzetu wa Green Voices zinapaswa kuongezwa, kwa sababu zinalengo siyo tu kumkomboa mwanamke, bali kulinda mazingira yetu ambayo yanazidi kuteketea kila uchao kutokana na ukataji wa misitu kwa madhumuni ya kutafuta kuni na mkaa.
"Akinamama wanaathirika sana, wengine utakuta macho mekundu kutokana na moshi wa kuni, na wanapokuwa wazee ndio wanaoshambuliwa na watu wengine wasio na utu kwamba eti ni wachawi kwa sababu macho yao ni mekundu, lazima kutumia teknolojia mbadala kuwanusuru mama zetu, " alisema.
Hata hivyo, aliwataka akinamama hao kushikamana pamoja katika shughuli zao ili waweze kujiletea maendeleo, kwani umoja ni nguvu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amesema, mradi wa jiko la umeme-jua ni sehemu ya miradi 10 inayotekelezwa chini ya Green Voices ambapo Tanzania ndiyo pekee iliyopendekezwa kutekeleza mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika, , ambayo inaongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz.
Hata hivyo, taasisi hiyo inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12 barani Afrika ambayo imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices ukitajwa kuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Kwa mujibu wa Bi. Secelela, Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro.
“Miradi hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, na kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi huu wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanjaro,” anafafanua Secelela.
Anasema, lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali kupitia taasisi na idara zake zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii imekuwa ikiendesha program mbalimbali za mafunzo ya ufundi ikiwemo utengenezaji wa majiko banifu na sanifu kama inayoendelea katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Malampaka wilayani Maswa.
Hata hivyo, bajeti ndogo imekuwa changamoto kubwa kukwamisha kuwafikia wananchi wengi na kuwapatia elimu ya aina hiyo.
0 maoni:
Post a Comment