CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema hakiogopi yaliyompata Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Stephen Ulimboka ambaye alitekwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Mabwepande, jijini Dar es Salaam, Juni mwaka huu.
CHADEMA kimesema, wapenda mageuzi sehemu mbalimbali duniani, walikamatwa, kuteswa na kuuawa, lakini tawala kandamizi hazikufanikiwa kuzima mabadiliko yaliyokuwa yakihitajiwa na wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi usiku na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, wakati wa harambee iliyoandaliwa na vijana wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam waliofanikisha kupatikana kwa zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) ambapo sh milioni 270 ni fedha taslimu na ahadi sh milioni 253.
Mbowe aliwataka wananchi kutoogopa yaliyomkuta Dk. Ulimboka ambaye inadaiwa alifanyiwa kitendo hicho cha kinyama na watu wanaodaiwa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa kwa lengo la kumdhibiti asiendelee kuwashawishi madaktari kugoma.
Alisema, mabadiliko yoyote yanahitaji usajiri, hivyo ni vema wananchi wakajiandaa na matukio yoyote kwa sababu serikali haioneshi nia ya kutatua kero za wananchi, wala kusikiliza manung’iniko yao.
“Tuache woga ndugu zangu, mabadiliko tunayotaka yanaweza kupatikana kwa njia ngumu, sisi hatuogopi yale yaliyomkuta Dk. Ulimboka, tunaamini mageuzi yatapatikana muda si mrefu,” alisema.
Mbowe alisema, CHADEMA haitachukua nchi kwa kutumia mtutu wa bunduki wala maandamano, bali vuguvugu la mabadiliko (M4C), ndilo litakalofanikisha azma hiyo.
Aliongeza kuwa, CHADEMA kimejipanga kwa hilo kutokana na kuwa na dhamira yake ya kweli na akili walizojaaliwa na Mungu katika kuwatafutia ukombozi Watanzania.
“Nchi hii tutaingoza vizuri… tutawakomboa Watanzania, hatuwezi kumuachia mtu kuongoza nchi wakati hawezi kusimamia rasilimali za taifa, hawezi kusimamia madini wala gesi, ufisadi wa kutisha, ni lazima kufanya mabadiliko ya kweli ili nchi iweze kusonga mbele, tuwaachie urithi mzuri watoto wetu, CCM ni lazima waondoke,” alisema.
Mbowe alisema, wananchi wanatakiwa kuungana pamoja na kuondoa woga ili kujenga taifa bora na kupata ushindi mnono katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Alisema, hivi sasa hawezi kuzungumzia kama anagombea ubunge wala urais kwa sababu haongozi kundi au genge la watafuta vyeo na madaraka, bali kundi la watu wanaopenda mabadiliko.
Kipaumbele cha CHADEMA
Alisema endapo CHADEMA itaingia madarakani, kipaumbele cha kwanza hadi cha tatu, kitakuwa ni elimu kwa sababu CCM haijaipa uzito mkubwa kwa makusudi.
Mbowe alisema, CCM imefanya hivyo kwa kuwa inataka watu wawe wajinga ili wapate mwanya wa kuendelea kuwatawala kwa urahisi.
“Serikali ya CCM imewadumaza Watanzania na kuwafanya kuwa masikini wa akili kuliko rasilimali kwa kuwa, waliona wakiwasomesha watailinda dhahabu na rasilimali nyingine muhimu ambazo zitawasaidia kupambana na umasikini,” alisema.
Aliongeza kuwa, endapo CHADEMA itaingia madarakani, itakuwa na fursa ya kusilikiza matatizo ya walimu, kuwasikiliza madaktari na hata wafanyakazi katika sekta nyingine ili kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora.
Michango ya kuing’oa CCM
Katika harambee hiyo ya juzi iliyoandaliwa na vijana wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kukiwezesha chama hicho kufikia azma yao ya kuingia madarakani mwaka 2015, zaidi ya sh milioni 500 zilipatikana.
Wanachama na wapenda mabadiliko kutoka katika mikoa mbalimbali pia walishiriki kwenye harambee hiyo kwa njia ya simu na kutuma fedha, na wengine waliahidi kuziingiza katika akaunti ya M4C ili kuimarisha harakati za vuguvugu hilo la mabadiliko.
Mara baada ya kukamilisha harambee hiyo, aliyekuwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema alitangaza kiasi cha fedha zilizopatikana kuwa ni sh milioni 385 ambazo hazijajumlishwa na fedha zilizochangwa katika mitandao ya simu.
Aidha, alisema Oktoba mwaka huu wanachama wa CHADEMA wanaoishi nchini Uingereza, watakipatia chama hicho magari manne aina ya Canter na ifikapo Desemba watatoa helikopta kwa ajili ya kusaidia harakati hizo.
Pia, alitaja namba za akaunti za M4C kuwa ni pamoja na 01J1080100600 kuchangia kwa maana ya ukombozi wa nchi.
Mwenyekiti wa M4C, Alex Mayunga alisema, fedha hizo zitatumika kununulia magari pamoja na vifaa mbalimbali vitakavyofanikisha kampeni na kutangaza chama nchi nzima kuhakikisha wanashinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
Published by Tanzania Daima on 12 Aug, 2012
0 maoni:
Post a Comment