Matayarisho ya kuweka tabaka la C1, kabla ya kuwekwa lami katika barabara za Arusha (Picha na Gazeti la HabariLeo)
********
JIJI la Arusha ni kitovu kikuu cha utalii nchini. Ni moja ya majiji matano yaliyoko nchini.
Mengine ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Tanga. Jiji la Arusha lina ukubwa wa kilomita za mraba 208, baada ya kuongezwa eneo kutoka Wilaya ya Arusha. Eneo lililoongezwa linajumuisha Kata ya Moshono, Olasiti na Kijiji cha Terrati kilichopo kwenye Kata ya Terrati.
Kuongezeka kwa maeneo hayo, kunafanya Jiji la Arusha kuwa na mitaa 137, Kata 19 huku tarafa zikiendelea kuwa tatu kama ilivyokuwa awali. Huwezi kuzungumzia utalii wa aina yoyote nchini bila kutaja Jiji la Arusha.
Idadi ya wageni imezidi kuongezeka siku hadi siku, kutokana na Jiji hili kuwa na vivutio vingi vya utalii na mazingira bora na safi yanayovutia watalii na wageni wanaofika kwa shughuli mbalimbali.
Kwa kujua umuhimu wa Jiji hilo, Halmashauri ya Jiji la Arusha imekuwa inahakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi na wageni wanaotembelea jiji hilo kila mara.
Pamoja na kuboresha utoaji wa huduma zake Jiji la Arusha kwa muda mrefu limekabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji ikiwepo miundombinu duni ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa jiji hilo.
Akizungumzia tatizo la ubovu wa miundombinu, mkazi wa eneo maarufu la Kaloleni, Antony Lekule, anasema pamoja na uzuri lakini zipo kasoro zinazolitia doa Jiji la Arusha.
“Arusha ni mji mzuri sana lakini hakuna barabara, mitaro na njia nzuri za waenda kwa miguu. Mvua ikinyesha siku mbili tu hapafai. Mjini maji yanafurika barabarani, Soko Kuu hapapitiki na kila mahala…kwa ujumla Arusha miundombinu hairidhishi.”
Changamoto na kilio hicho cha wakazi wa Arusha kipo mbioni kupata suluhisho. Hii inatokana na kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Kukuza Majiji (TSCP) wenye lengo la kuboresha miji nchini.
Mpango huo ulioanza kutekelezwa katika Jiji la Arusha ni suluhisho la kero za wananchi wa
eneo hilo katika eneo la miundombinu na usafi wa mji kwa ujumla wake.
Pamoja na hayo, mradi huo haukusahau nyanja ya utawala bora kwa watendaji wa jiji lengo likiwa ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kusimamia shughuli zote zilizoko chini ya mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomih Chang’ah, akizungumzia kuhusu mradi huo anasema; “tumeanza kutekeleza mradi mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba 2011 chini ya Mpango wa TSCP.”
Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Denmark, lengo likiwa ni kuboresha miundombinu, uimarishaji na usimamizi wa utawala bora katika baadhi ya Majiji na Manispaa.
Jiji la Arusha ni miongoni mwa Majiji na Manispaa zilizobahatika kuwepo katika mradi huo ambapo kazi zinatekelezwa kwa awamu.
Mkurugenzi huyo anasema, “katika awamu ya kwanza kazi zinazofanyika ni ujenzi wa barabara za katikati ya mji (CBD Roads) zenye urefu wa kilometa 7.23, ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wenye urefu wa mita 800 na uwekaji wa taa za kuongozea magari katika makutano ya barabara tatu.”
Kazi imeanza na barabara zilizoko kwenye awamu ya kwanza, ambazo ziko katikati ya mji zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Babu, Wachaga, TCA(Technical) na Romboshine.
Baada ya muda mfupi barabara hizo zitakamilika na kazi itaendelea kwenye maeneo mengine ya katikati ya mji. Maeneo yatakayowekwa taa za barabarani ni kwenye makutano ya Esso – Sokoine, Makongoro - Col. Middletone na Unga Ltd – Sokoine (Friends Corner).
Akielezea kwa kina kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Chang’ah anasema “kundi la pili litahusisha ujenzi wa barabara za Majengo-Bumiko, Canal Ndomba, NMC-PPF na Njiro, zote zikiwa na urefu wa kilometa saba wakati kundi la tatu litahusika na uimarishaji wa Dampo la takataka katika eneo la Murriet lenye ukubwa wa ekari saba na kundi la nne ni ununuzi wa vifaa vya kukusanyia na kusafirishia takataka.”
Anasema barabara zote zitakazojengwa katika mradi huo ni za lami na zitakuwa na njia za wapita kwa miguu pamoja na mifereji ya kupitisha maji machafu. Mhandisi Lamsy Afwilile ni
Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika Jiji la Arusha na mradi huo, unatekelezwa chini ya idara yake.
Akizungumza kuhusu mradi huo, anasema utakuwa na tija kwa wananchi wa Jiji la Arusha kwa sababu barabara zitakapokamilika zitapunguza kero kubwa ya msongamano wa magari.
Katika kuimarisha, usimamizi na utawala bora kupitia mradi huo, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kujengea uwezo watumishi kwenye maeneo ya usanifu wa kitaalamu, manunuzi na usimamizi wa fedha.
Maeneo mengine ni katika miradi na mikataba, kutunza na kulinda mazingira ya afya ya jamii, kuandaa mpango mkakati wa mji kwa kutumia teknolojia ya kompyuta, kuimarisha uwezo wa halmashauri katika makusanyo ya ndani kutoka katika vyanzo vyake na pia usimamizi wa mali za kudumu.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa Mradi katika masuala ya Ufundi, Mhandisi Joachim Mbwale, anasema mradi huo wa TSCP kwa upande wa Jiji la Arusha, umeanza vema na kwamba kazi zinaendelea vizuri.
Aidha, Mhandisi huyo kutoka Kampuni ya Kimataifa ya SNCLSVSLIN ambayo inashirikiana na Kampuni ya MMK, anasema katika ujenzi wa barabara unaoendelea sasa, barabara huchimbwa kwa sentimita 69 hadi kufikia tabaka la chini kabisa ambalo kitaalamu linaitwa G3.
Anasema lami hubebwa na matabaka matano ambayo ni G3 ambao ni udongo wa chini kabisa kwa kuanza kubeba tabaka la G7 lenye unene wa sentimita 15, kisha tabaka la G 15 lenye unene wa sentimita 15, likifuatiwa na tabaka la C1 lenye unene wa sentimita 20 na baadaye tabaka la CRR lenye unene wa sentimita 15.
Anasema baada ya kuridhishwa na matabaka hayo yote, lami huwekwa kwa unene wa sentimita 4 na kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Sh bilioni 25.75, ambapo utekelezaji wake utakamilika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Hii ni Makala ya Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,Nteghenjwa Hosea iliyochapishwa kwenye gazeti la HabariLeo, 24 Mei 2012.
0 maoni:
Post a Comment