Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Chadema, Shibuda jino kwa jino

MGONGANO wa kisiasa baina ya Chadema na mbunge wake, John Shibuda umeingia hatua nyingine baada ya mbunge huyo jana kulitaka Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limwombe radhi kwa kauli yake.

Shibuda, ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki, amechachamaa na kutoa siku tatu kwa Bavicha kufanya hivyo kwa alichokieleza ni kumdhalilisha.

Amesema iwapo Baraza hilo litashindwa kufanya hivyo, atalishitaki kwa wapiga kura wake ambao watatoa msimamo wao, huku akisisitiza kwamba kinachomponza ndani ya Chadema ni yeye kuwa Msukuma.

Katika hatua nyingine, Chadema imebainisha ajenda kuu tatu itakazozipa mkazo katika mijadala ya Bunge lijalo la Bajeti ikiwamo kuishinikiza Serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro sugu nchini.

Ajuta kuwa Chadema

Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Shibuda alisisitiza, kwamba hatakubali kuwa ‘kitoweo’ cha wajinga ndio waliwao, akisema alipokuwa CCM walitambua mchango wake na alipohamia Chadema, alikutana na mfumo mwingine wa uongozi.

Hata hivyo, alisema azma yake ya kugombea urais iko pale pale iwapo chama hicho kitampitisha kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

"Niko tayari kupoteza maisha yangu kwa kupigania utu wangu, uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 nilizunguka na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa katika Kanda ya Ziwa nikamnadi kuwa anafaa kuwa Rais, sasa najiuliza kazi yangu ni kutangaza wengine wagombee urais?

“Kama chama kitanipitisha kugombea urais nitagombea na itakuwa zamu ya Dk. Slaa kunipigia debe," alisema Shibuda.

Akizungumzia kauli zilizotolewa na Bavicha, alisema amesikitishwa na kauli za Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche, baada ya kutangaza kuwa atagombea urais 2015 kwa tiketi ya Chadema na kauli za kumbeza na kuonekana hafai zimekuwa zikitolewa dhidi yake bila kuulizwa.

"Heche lazima aniombe radhi kwa kunikashifu mbele ya Watanzania, lakini hapo ndipo desturi ya mtu mzima ovyo inapothibitika, kwani mtu unatakiwa kuchunguza kwanza kabla ya kusema," alisema Shibuda.

Aliongeza: “Nawaomba wananchi wawe watulivu hasa wapiga kura wangu, kwani kama kuna mabaya yanatakiwa yatoke ulimini mwangu, na si mtu kunisemea; matakwa ya kauli ya Bavicha ni kifuniko cha siri sana na kama wanaona kutangaza kwangu kugombea urais ni vibaya ni bora watangaze nani wanamtaka agombee nafasi hiyo kupitia Chadema.

"Inasikitisha, Mwenyekiti wa Baraza anatangaza dhambi ya kubaguana, kuna dhambi gani Shibuda kusema kusudio lake la kugombea urais? Tabia aliyoonesha Mwenyekiti inatambulisha huzuni ya fikra mtambuka, kuwa hakuna mtu anayeweza kuchaguliwa bila kura mchanganyiko," alisema.

Alisema wameamua kumchokoza kupitia vyombo vya habari, kwani akiwa kwenye semina ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, iliyokuwa imeandaliwa na Mpango wa Kutathimini Utawala Bora Afrika (APRM) mwanzoni mwa wiki mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete alimwuliza kama atagombea urais akamjibu, lakini anashangaa dhambi yake inatokea wapi.

"Ni kweli Rais Kikwete aliniuliza, jibu nililompa ni kumwambia kuwa ni kweli nitagombea, kwani ukisikia mtu kapeleka posa na wewe unamtaka msichana huyo huyo si nawe utapeleka posa ili mshindane?" Alihoji Shibuda.

Alisema yeye ni miongoni mwa watu walioingiza wanachama wengi Chadema na hata Dk. Slaa alipogombea urais 2010 hakupigiwa kura na wanachama wa Chadema peke yao, kwani wapo hata wana CCM waliompigia lakini anashangaa dhambi ya ubaguzi ilikotoka.

Alisema katika uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki hivi karibuni, Chadema ilikuwa na mgombea Anthony Komu na alikwenda kuomba hata watu wa CCM wampigie kura, lakini hakusikia akionywa kwa nini alifanya vile.

"Leo Msukuma Shibuda, anatoa kauli ile ile inakuwa haramu, je Mtanzania ajifunze nini? Labda ningekuwa Mchaga nisingeulizwa, inasikitisha sana," alisema.

Alisema: “Hata nikifukuzwa ndani ya chama hicho, watakaofanya hivyo watakuwa wamepata faida gani? Lakini hilo litathibitisha uongozi wa Chadema kuwa wa kidikteta na nawaomba viongozi wa Chadema watafakari kwa kina bila jazba, kwani tabia waliyoonesha vijana wa Chadema haipendezi hata kidogo.

"Juzi nilimpigia simu Mbowe (Freeman) na kumwuliza kama aliwatuma vijana wanitukane, akasema atanipigia lakini mpaka sasa hajafanya hivyo," alisema.

Shibuda alisema kama alikosea kujiunga Chadema atawataka radhi Watanzania, lakini hatakubali kudhalilishwa kwa namna yoyote.
"Mwaka 2005 nilipotangaza kugombea urais kupitia CCM hakuna aliyenishangaa Umoja wa Vijana au Wanawake hawakunichafua, si NEC ya CCM, au Kamati Kuu na wala sikutishwa kufukuzwa kwenye chama, sikupewa sifa za ajabu, iweje iwe hivyo Chadema ambacho ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo?"

Alihoji Shibuda. Alisema keshokutwa atakuwa Shinyanga na atatoa kauli baada ya kuzungumza na wapiga kura wake.
Kuhusu kumchukulia hatua Shibuda anayeshutumiwa na Bavicha kutangaza mbele ya NEC ya CCM nia yake ya kuwania urais mwaka 2015 huku akiahidi kumwomba Rais Kikwete awe Meneja wake wa kampeni, Mnyika alisema hakuna hatua zozote za kinidhamu watakazomchukulia.

“Tulishamwandikia barua ya onyo kali kipindi cha nyuma kuhusu kauli zake na wakati ule mimi (Mnyika) nilikuwa Katibu wa Wabunge wa Chadema, nilipeleka malalamiko kwenye chama, sasa mimi si Katibu tena na mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyoletwa rasmi chamani kumhusu,” alisema Mnyika.

“Aprili 26, Kamati Kuu cha chama ilikaa na kujadili hatma ya taratibu za kinidhamu kuhusu kauli za Shibuda na kutoa onyo kali kwake, hizi kauli za hivi karibuni kwetu si kipaumbele, kwetu kipaumbele ni kuing’oa CCM madarakani na kutetea wananchi,” alisema Mnyika.

Shibuda ambaye alibwagwa kwenye kura za maoni za CCM za kuwania ubunge mwaka 2010 na kuhamia Chadema alikoukwaa, mara kadhaa amekuwa akipinga kauli na misimamo ya wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni likiwamo suala la posho ambalo yeye aliunga mkono ongezeko lake huku upinzani ukipinga.

Mnyika alisema endapo malalamiko yatawasilishwa rasmi na Bavicha au mwanachama yeyote, vikao rasmi vitakaa na kujadili suala hilo kwa hatua za kinidhamu.

Hata hivyo alisema Chadema ni chama cha demokrasia, hivyo kila mtu ana haki kuzungumza chochote bila kugeuza demokrasia karaha. Kauli iliyoonekana kusigana na ya Bavicha iliyotolewa na Heche dhidi ya Shibuda.

Ajenda tatu za Chadema Chadema jana ilibainisha ajenda kuu tatu itakazozipa uzito katika mijadala ya Bunge ikiwamo kuishinikiza Serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro sugu nchini, ikiitaja kuwa ni inayohusu Serikali na wafanyakazi kwenye mishahara. Pia mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na migogoro ya ardhi ambayo kwa mtazamo wake, inaona kuwa pamoja na Serikali imekuwa ikishughulika na matokeo badala ya vyanzo.

“Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Chadema Bunge lijalo itaweka nguvu kubwa katika mambo makuu matatu, mfumuko wa bei za bidhaa zinazoongeza ugumu wa maisha kwa Mtanzania, Katiba mpya na migogoro sugu,” alisema Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika.

Mnyika alikuwa akijibu swali kuhusu malengo ya Chadema katika Bunge lijalo linalotarajiwa kuanza Juni 12. Mnyika alizungumzia maazimio ya Baraza Kuu la Chadema ya hivi karibuni kuhusu operesheni maalumu katika mikoa ya Kusini baada ya Nyanda za Juu Kusini na kauli ya chama kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo mchakato wa Katiba mpya.

Akifafanua kuhusu ajenda hizo, Mnyika alisema wataichachamalia Serikali kuhusu hatma ya migogoro kuhusu mishahara ya wafanyakazi na makato makubwa ya kodi, adha ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na migogoro ya ardhi inayozuia maendeleo nchini.

Mnyika alisema pia kuwa suala la mfumuko wa bei, kupanda kwa maisha, ongezeko kubwa la matumizi ya fedha katika Serikali kuliko mapato kunakosababishwa na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, japo yalizungumzwa katika Bunge lililopita, watayawekea mkazo wa pekee ili kuishinikiza Serikali kuchukua hatua.

“Suala la Katiba, sisi Chadema tunaona kwamba Serikali haijalipa kipaumbele kwenye eneo la Bajeti na kuhusu matakwa tuliyokubaliana ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa awamu ya pili na ya tatu, Bunge lijalo tunataka dhamira ya dhati ya Serikali kuhusu muundo wa Bunge la Katiba na Mchakato wa Kura za Maoni,” alisema Mnyika.

Akizungumzia uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema operesheni maalumu ya ‘Vua gamba, vaa gwanda’, itahamia mikoa ya Mtwara na Lindi Mei 28.

Alisema operesheni hiyo inayolenga pia kutoa elimu ya uraia ili wananchi washiriki vizuri kutoa maoni ya Katiba mpya, sambamba na kutafuta nguvu ya umma kuhusu mambo mbalimbali na kujenga oganaizesheni ya chama mijini na vijini, itakuwa ya jimbo kwa jimbo na wataweka kambi ya siku zisizopungua 15 katika mikoa hiyo.

Ili kuiongeza nguvu operesheni hiyo, Mnyika alisema itatanguliwa na mkutano mkubwa wa hadhara Dar es Salaam Mei 26 ili kufungua pazia la mchakato wa Katiba mpya.

Hata hivyo hakuwa tayari kutaja eneo kwa madai kuwa bado uamuzi haujatolewa kuhusu wapi mkutano huo ufanyike.

Aponda msimamo wa CCM “Sisi tofauti na CCM wanaong’ang’ania na kulazimisha kufikiri kwa niaba ya wananchi kuhusu maoni ya Katiba mpya, kwamba kipi wanadhani kijadiliwe na kipi kiachwe, tunataka wananchi waamue wenyewe, haiwezekani wewe chama tawala uamulie watu cha kujadili, tutakuwa tunarekebisha Katiba na si kuandika mpya,” alisema Mnyika.

Alidai amesoma na kupitia vyombo vya habari kuhusu ilichosema CCM kwenye suala la Katiba mpya na kuona inachakachua mchakato huo na haina dhamira ya dhati ya kutaka Watanzania waandike Katiba mpya, bali kurekebisha iliyopo.

Huku akinukuu vipengele kadhaa vya Ibara ya Nane na ya 21 ya Katiba ya sasa, vinavyotoa mamlaka kwa umma kuhusu kujadili mambo ya msingi ya mustakabali wa nchi, alisema Chadema inaipinga CCM kuainisha maeneo wanayodhani hayana haja kujadiliwa, kuondolewa au kuongezwa.

Maeneo aliyodai Mnyika kuwa CCM wameyang’ang’ania isivyo sawa kwa kuwa ni chama tawala, ni pamoja na muundo wa serikali mbili, akitaka wananchi waachwe hata wakitaka tatu, ardhi kuendelea kuwa chini ya mamlaka ya Serikali (Rais) na baadhi ya mamlaka ya Rais.

Hata hivyo katika hayo, CCM haikulazimisha yafuatwe bali ilibainisha na kueleza maoni yao kuhusu maeneo hayo na kueleza bayana kuwa wanaweza kujadili vinginevyo kwa mujibu wa Sheria.

Mnyika alitumia fursa hiyo kuionya CCM kwa alichodai ni kutaka kumiliki mchakato wa Katiba mpya na kueleza kuwa sheria haijazuia wananchi kuhoji na kutoa maoni kuhusu mambo yote yanayohusu nchi na kama ikiendelea hivyo hatma yake ni kupata Katiba mbovu.

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Gloria Tesha, Dar (HabariLeo, 19Mei 2012)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO