Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki (kulia) akizungumza jambo na Naibu wake, Lazaro Nyalandu kabla ya kuzindua bodi ya ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameanza kuonyesha makali baada ya kusitisha utoaji vibali vya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi, huku akiapa kuifumua Idara ya Wanyamapori na kuisuka upya kama sehemu ya mkakati wake wa kumaliza tatizo la rushwa na ufisadi.
Tamko hilo la Balozi Kagasheki limekuja kipindi ambacho wizara hiyo imekuwa ikitajwa kuwa na mianya mingi ya ufisadi ambayo imekuwa ikiwaingiza majaribuni mawaziri na baadhi ya watendaji wake, hivyo kujikuta katika tuhuma nzito za rushwa.
Hatua hiyo ya Balozi Kagasheki inatafsiriwa kama kukwepa kivuli cha watangulizi wake pamoja na baadhi ya watendaji ambao kama alivyowahi kunukuliwa mara baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Mara baada ya kuapishwa Balozi Kagasheki alikaririwa akisema uteuzi wake ni changamoto kubwa akijua kwamba wizara anayokwenda kuiongoza ina matatizo lakini akasema lazima wananchi wapate faida ya rasilimali zao na kwa kufanya hivyo ataanzia kwenye ripoti ya CAG kusafisha njia.
“Watanzania watuangalie utendaji wetu wa kazi. Lazima tuondokane na tabia ya ripoti kuvumbua uovu na kuziacha tu zikapita. Nitahakikisha ripoti ya CAG haipuuzwi. Wizara hii watu wanakula vibaya hivyo nitawashughulikia na haya matatizo ya vitalu na wizi wa nyara za Serikali yote nitayashughulikia.”
Akizungumza Dar es Salaam katika uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana, Balozi Kagasheki alisema kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya wizara hiyo ili kurejesha uwajibikaji katika sekta hiyo.
“Watu hawa hawana huruma linapokuja suala la fedha. Fedha kwao ni kila kitu na wanaiabudu kama Mungu kwao,” alisema Kagasheki na kuongeza:
“Idara ya wanyamapori inakusanya fedha nyingi lakini, haziinufaishi Serikali wala Watanzania isipokuwa wao wenyewe. Wanaonufaika na fedha hizo ni wafanyakazi wenyewe wa idara na marafiki zao nje ya nchi.”
Balozi Kagasheki alisema Idara ya Wanyamapori kama ikisimamiwa vizuri kwa kukusanya mapato kikamilifu kiwango hicho cha fedha kinaweza kupunguza matatizo ya wananchi.
“Kuna pesa nyingi zinapatikana kupitia wanyama wanaosafirishwa nje ya nchi lakini, wananchi bado wanasota na ugumu wa maisha kwani fedha hizo zingeweza kuisaidia Serikali katika kuwahudumia wananchi wake,” alisema na kuongeza:
“Bei ya wanyama ni kubwa na ni mambo ya aibu kuona wanaofaidika ni wachache hivyo, kila mmoja wetu katika wizara ambaye anajua analigharimu taifa kwa kujineemesha akae akijua mabadiliko yatakayofanyika yatamukumba.”
Kuhusu Bodi
Balozi Kagasheki aliitaka Bodi hiyo yenye wajumbe saba kuhakikisha inafuatilia kwa kina na inarejea mipaka ya awali kwa misitu iliyovamiwa kuitunza na kuiendeleza.
“Shughuli za kilimo, malisho, uchimbaji wa madini na makazi na hata kufikia shule za mijini kujengwa na kusajiliwa vikiwa ndani ya eneo la hifadhi, viwanja kupimwa na kuwekewa mawe ndani ya hifadhi ni tatizo ambalo linatakiwa kutatuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema.
Alitaja baadhi ya misitu iliyoathiriwa na wavamizi kuwa ni Geita, Biharamulo, Mlele Hills, Pugu Kazi Mzumbwi, Maeneo ya Misitu ya Mikoko, Misitu ya Nishati Ruvu na Mbeya.
“Pamoja na changamoto zilizopo, ni mategemeo ya wizara kwa wajumbe wa Bodi ni kutoa ushauri uliotukuka na wa kina hususan usimamizi wa misitu kwa ujumla, ukodishaji wa misitu, ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali na katika muktadha wa uendeshaji wa misitu kibiashara,” alisema.
Awali, Mtendaji Mkuu wa TFS, Juma Mgoo alisema TFS itahakikisha inafanya kazi zake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuharakisha utoaji wa vibali, leseni na vyeti kwa wakati.
“Madhumuni makubwa ni kuhakikisha tunarejesha heshima ya wizara hii ambayo kama itatumika vizuri itachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa na kuwanufaisha wananchi wenyewe na siyo watu binafsi,” alisema Mgoo.
Wajumbe wa Bodi hiyo ni Ester Mkwizu kutoka Mfuko wa Taasisi Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambaye ni Mwenyekiti, Gladness Mkamba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Boniventura Baya kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Profesa Yonika Ngaga kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Morogoro (Sua), Profesa Himid Majamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rawson Yonazi na Sosthenes Sambu kutoka Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkwizu alisema: “Hapa hakuna ufanisi kama hatutawashirikisha wananchi wenyewe ambao ndiyo wanaojua kila kitu kutokana na kuwa wahusika wakuu wa misitu hivyo tunaomba ushirikiano wao.”
Published by Mwananchi on 22 May 2012
0 maoni:
Post a Comment