POLISI mkoani hapa imempa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) saa 12 kujisalimisha vinginevyo adhalilishwe.
Polisi pia inashikilia viongozi watatu wa juu wa Chadema, akiwamo Mwenyeki wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavita), John Heche, kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi na ukabila kwa Rais na wananchi wake.
Habari za kipolisi zinadai kuwa wengine waliokamatwa ni Alphonce Mawazo ambaye alikuwa Diwani wa Sombetini (CCM) ambaye hivi karibuni alihama chama hicho pamoja na Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM wa Wilaya ya Arusha, Ally Bananga na kujiunga Chadema hivi karibuni.
Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi nchini, Isaya Mngulu alipoulizwa juu ya hao kukamatwa hakukanusha wala kuthibitisha, bali alisema wanahojiwa kwa maneno waliyotoa kwenye mkutano wa hadhara Jumamosi.
‘’Kweli kuna viongozi wa Chadema tumewakamata baada ya maneno waliyotoa katika mkutano wa hadhara Jumamosi, lakini kwa sasa ni mapema kuyataja,’’ alisema Mngulu.
Hata hivyo, Naibu Kamishina huyo alisema Polisi inamtaka Mbunge huyo ajisalimishe kabla ya saa 12 jioni (juzi) baada ya jitihada za makusudi za kuheshimiana kushindikana ili aende Polisi mwenyewe.
Mngulu alisema si kwamba Polisi inashindwa kumpata, bali inampa muda na iwapo
utapita bila kujisalimisha, hatua kali za kumsaka zitafanyika na hiyo haitatambua ubunge wake, kwani hayuko juu ya sheria za nchi.
‘’Nassari njoo mwenyewe Polisi vinginevyo itakudhalilisha na haitautambua ubunge wako, kwani wewe hauko juu ya sheria,’’ alisema.
Naibu Kamishina huyo alisema katika mkutano wa hadhara Jumamosi uliohudhuriwa na viongozi kadhaa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, matamshi
ya uchochezi yalitamkwa.
Alisema miongoni mwa matamshi hayo ni ‘’kumpiga marufuku Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete, kukanyaga jimbo la Arumeru Mashariki na Kanda ya Ziwa, kwani maeneo hayo ni ya Chadema’’.
Mngulu alitaja matamshi mengine ambayo yanamdhalilisha Rais na mwanawe, Ridhiwani, yakihusisha uteuzi anaoufanya Rais kwa viongozi mbalimbali nchini.
Alisema hayo matamshi hayana maana yoyote kwa jamii, kwani yana lengo la uchochezi kwa Rais na wananchi wake. Baada ya matashi hayo jukwaani, Mbowe alisimama na kuyakana akisema si ya Chadema, bali ya vijana hao wenye damu moto wa gesi na ni kauli binafsi na yeye haziungi mkono.
Akizungumzia suala la uvamizi wa mashamba na mauaji katika wilaya ya Arumeru, Mngulu alisema Polisi imekamata watu 12, kati yao saba wamefikishwa mahakamani na watano wako katika uchunguzi mkali wa Jeshi hilo.
Mngulu alitaja waliokamatwa katika tukio la mauaji ya Msafiri Mbwambo Aprili 27 kuwa ni pamoja na Daudi Mkumba, Mathias Kurwa na Said Mkwela.
Alisema wote ni wakazi wa Usa River, Arumeru mkoani hapa na jana walifikishwa mahakamani kwa mashitaka ya mauaji.
Naibu Kamishina huyo aliendelea kusema kuwa watu wengine watatu wamekamatwa kwa madai ya kuhusika na tukio la mauaji ya Noel Mang ambaye alikutwa amekufa baada ya watu zaidi ya 20 kuvamia shamba, kuchoma moto stoo ya matrekta, jenereta la umeme na kusababisha hasara ya Sh 222,775,000.
Alisema waliokamatwa ni pamoja na Godlove Manang (26) mkulima mkazi wa kijiji cha Sing’isi, Arumeru; Anthony Kiungai (23) mkulima na Judica Kitomari (26) dereva na wote walifikishwa mahamani kwa tuhuma za kuharibu mali.
Mngulu alizungumzia pia suala la baadhi ya viongozi kutishiwa kuuawa na kusema Polisi imebaini kuwa watu hao walijitumia ujumbe, kwani hata mmiliki wa namba inayotuma ujumbe huo kwa wengine inaonesha kwamba hata mwenyewe alijitumia kwenye namba yake nyingine.
Mbowe na ushahidi
Naye Halima Mlacha anaripoti kwamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wasira amemtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, atoe ushahidi wa madai yake kuwa CCM na Serikali yake imekuwa ikiua watu.
Pia waziri huyo ameonya viongozi wa siasa kuwa makini na kauli zao wanazotoa katika jamii kwa kuhakikisha hazijengi uhasama wala kugawa nchi kwa maslahi yao kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Ikulu Dar es Salaam jana, alisema amesikitishwa na kauli za Mbowe dhidi ya CCM na Serikali na kumtaka akiwa kiongozi athibitishe madai yake kuwa chama hicho na Serikali yake wamekuwa wakiua watu.
“Napenda kuliweka wazi hili kuwa CCM kamwe sera zake si kuua watu kisiasa, sasa mwenzetu Mbowe amekuwa akitoa kauli kali dhidi yetu, wakati yeye ni kiongozi mkubwa tu anayeweza kujitokeza na kutoa ushahidi wa nani kauawa na nani na wapi,” alisema.
Alisema ni vema viongozi wanapotoa kauli zao wahakikishe kuwa wanawajibika na nazo na kutambua kuwa chochote wanachokitoa iwapo kitakuwa na walakini, kutazalisha mtafaruku na mgawanyiko katika Taifa, jambo ambalo ni hatari.
“Hata kama ni propaganda basi hakikisheni propaganda zenu zinakuwa na ukweli, si kusema uwongo unaohatarisha amani na utulivu wa Taifa,” alisisitiza Wasira
Chanzo: Habari Leo (Picha na SERIA JR)
0 maoni:
Post a Comment