RAIS Jakaya Kikwete jana alitangaza baraza lake la mawaziri na kuwatupa nje mawaziri waandamizi akiwemo Mustafa Mkulo, huku akiweka wazi kuwa atawashukia makatibu wakuu na wakurugenzi wote ambao wizara na idara zao zilihusishwa na tuhuma za ufisadi.
Rais Kikwete kabla ya kutangaza baraza hilo la mawaziri, aliweka bayana kuwa hatua nzito zitachukuliwa dhidi ya watendaji wakuu wa wizara na wale wa idara mbalimbali ambazo mawaziri wake walikumbana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Alisema mawaziri waliowajibika wamefanya hivyo kutokana na dhamana zao, lakini akadai kuwa wale waliowafikisha hapo hawatapona.
“Haiwezekani waziri awajibike wakati wengine wapo. Wakati mwingine ni fitna tu ili kuwaondoa. Kila aliyesababisha naye atachukuliwa hatua tu,” alisema Rais kikwete
Hata hivyo, uteuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali, baadhi wakipinga na wengine wakiunga mkono.
Mhadhiri mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema kuwabakisha mawaziri ambao ofisi zao zilitajwa moja kwa moja na CAG, kunawavunja moyo wananchi, akidai kuwa uwajibikaji si lazima muhusika mwenyewe afanye kosa.
Aidha Dk. Lwaitama alisema haitoshi kufanya mabadiliko ya baraza hilo bali kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wote watakaobainika walitumia ofisi zao vibaya.
“Hawa watu walitakiwa kuwajibika kisiasa kabla hata Rais hajaamua kuwawajibisha nafikiri walikuwa wanasubiria aibu hii, lakini jambo la msingi ni hatua za kisheria zifuate kwa wote waliohusika na kuliingiza taifa katika matumizi mabaya,” alisema Dk. Lwaitama.
Kwa upande wake Dk. Bashiru Ally ambaye ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema baraza hilo limeenda zaidi ya lilivyojadiliwa bungeni kwa kuwagusa mawaziri wengine ambao hawakutajwa katika ripoti ya CAG.
Kuhusu mabadiliko ya kiutendaji na unafuu wa maisha kwa wananchi Dk. Ally alisema wananchi wasitegemee mabadiliko kwa kuwa tatizo la Tanzania siyo viongozi bali mfumo mzima wa uongozi ndiyo tatizo.
Alisema vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla wana jukumu kubwa la kuhakikisha mabadilko ya kweli yanapatikana katika Katiba ambayo haitampa Rais mamlaka ya kuwa mtu wa mwisho kufanya uteuzi.
“Rais anaweza kushauriwa watu wa kuwateua lakini asifuate ushauri huo hivyo kuna haja ya kuliangalia hili katika Katiba ijayo, kwa maana kutegemea yeye awe msemaji wa mwisho juu ya wateuzi wake inaweza kutufikisha pabaya,” alisema Dk. Ally.
Nae Ananileya Nkya, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, alisema haitoshi kufanya mabadiliko peke yake bali kuwe na hatua zaidi za kisheria kwa waliotuhumiwa ili kuwafanya viongozi waelewe kuwa uongozi ni dhamana.
Alisema kama hali hiyo haitafuatwa hata hao walioteuliwa wanaweza kufanya madudu zaidi ya watangulizi wao kwa kujua hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi yao.
Aliwatahadharisha mawaziri walioteuliwa kama hawana uwezo wa kutumikia nafasi hizo ni bora wakamueleza Rais badala ya kwenda kuapa huku wakijijua hawataweza kuwa waadilifu kwa nafasi zao.
“Kama wanaona hawataweza ninawashauri wasiende kuapa kwa maana Watanzania hawataweza kuvumilia uozo wa aina yoyote,” alisema Nkya.
Alisisitiza kuwa walioteuliwa katika wizara ya afya wahakikishe mabadiliko ya kweli yanafanyika katika wizara hiyo kwa ajili ya kuepusha madhara ya migomo na vifo kama ilivyotokea hivi karibuni.
Kafulila amshangaa JK
Naye Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, alisema bado baraza hilo limekuwa na mlundikano mkubwa na halisomeki kimkakati, hali itakayosababisha serikali kubeba gharama kubwa ya kuwahudumia mawaziri hao.
Alisema hakukuwa na sababu ya kuwa na waziri asiye na wizara maalum au mahusiano ya umma kwa kile alichoeleza ni matumizi mabaya ya mamlaka ya uteuzi.
Aliwataka viongozi wa kisiasa wasiishie katika hatua za kisiasa tu bali, washinikize hatua zaidi za kisheria na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote.
Alibainisha hatua hiyo itakuwa muhimu zaidi na itaondoa utamaduni wa CCM kubadilishana awamu za kula kwa kuudanganya umma kuwa wanawajibishana
Chanzo: Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment