Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Nswanzugwako wa CCM abwagwa tena, hatma ya ubunge wa Opulukwa wa CHADEMA kujulikana leo

MAHAKAMA ya Kuu Kanda ya Tabora imeitupa kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera wa NCCR-Mageuzi.

Jaji Haruna Songoro amesema kesi hiyo imetupwa kwa kuwa upande wa walalamikaji umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa madai yao.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Nsanzugwanko, akidai kuwa Buyogera alimtangaza kwamba ni mchawi na kuwa alifuja sh milioni 31 za mfuko wa jimbo.

Jaji Songoro pamoja na kutoa uamuzi huo, alimwamuru Nsanzugwanko kumlipa Buyogera gharama zote alizotumia katika kesi hiyo. Baada ya kutolewa hukumu hiyo, wafuasi wa Buyogera walimbeba juu na kuondoka naye mahakamani hapo.

Kwa upande wake Nsanzugwako ameahidi kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, akidai kuwa jaji alionyesha upendeleo wa wazi.

Hatma ya ubunge wa Opulukwa leo

Wakati huohuo Mahamaka Kuu Kanda ya Tabora, leo itatoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Meatu mkoani Simiyu, yaliyompa ushindi, Meshack Opulukwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kesi hiyo namba 1/2010 ilifunguliwa na mpiga kura, Masanja Renatus Salu, ambaye analalamikia ushindi wa Opulukwa kutokana na kuwepo kwa dosari katika uchaguzi huo.

Katika hati ya malalamiko, Salu anamlalamikia Opulukwa kutumia lugha ya ubaguzi dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Salum Khamis.

Madai mengine ni kuwa baadhi ya wasimamizi wasaidizi katika vituo nane walimpigia kampeni mbunge huyo na msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo mara mbili kinyume cha taratibu za Tume ya Uchaguzi.

Katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Frederick Wambali, upande wa mlalamikaji ulileta mahakamani hapo mashahidi 15 ili kuthibitisha madai yao huku upande wa utetezi ukileta mashahidi tisa.

Katika mwenendo wa kesi hiyo, wananchi wengi waliokuwa wakiisikiliza kutoka katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Meatu, Bariadi, Maswa na Shinyanga, wanataka kujua hatma yake leo.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni watatu ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Opulukwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Meatu.

Mlalamikaji alikuwa akiwakilishwa wa wakili wa kujitegemea, Kamaliza Kayaga, wakati Opulukwa alikuwa akiwakilishwa na wakili pia wa kujitegemea, Godwin Mganyizi.

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO