BAADA ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza lake la Mawaziri, Rais Jakaya Kikwete sasa anatarajia kuifumua sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumatano imebaini.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM, vilisema kuwa Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho taifa, ameamua kuitisha vikao vya chama ghafla pamoja na mambo mengine, kufanya mabadiliko kwenye sekretarieti yake.
Duru za kisiasa kutoka ndani ya chama hicho tawala, zilisema kuwa mabadiliko hayo yanatokana na mmoja kati ya wajumbe wa sekretarieti, Januari Makamba, kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu.
“Kama utakumbuka mara ya mwisho Rais Kikwete aliamua kuwaondoa mawaziri wote kwenye sekretarieti ya chama ili wajumbe hao waweze kufanya kazi muda wote. Alimwondoa Waziri Bernard Membe, Nape akalazimika kuachia u-DC. Kwa vile Makamba amekuwa waziri ni wazi kwamba ataachia nafasi hiyo na Rais ataijaza kwa kumteua mjumbe mwingine,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Wajumbe wengine wa sekretarieti hiyo ni pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mhasibu Mkuu, Mwigulu Nchemba, Martin Shigela, Amina Makilage, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi, Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Asha Juma na Katibu Mkuu, Willson Mkama.
Katika kujaza nafasi hiyo, Rais Kikwete anaweza kuwagusa wajumbe wengine kama ataona kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Ukiachia mabadiliko hayo, vikao hivyo vya CCM ambavyo vinaanza Mei 11 hadi 14, vinajadili mambo mbalimbali, ikiwemo hali ya kisiasa ndani ya chama hicho hasa kipindi hiki ambapo kinakabiliwa na kukimbiwa na wimbi la wanachama wake.
“Kuna mambo mazito ya kujadili. Kasi ya CHADEMA na ushindi wake Arumeru imeibua hofu, wimbi la wanahama wa CCM kuhamia CHADEMA, mpasuko ndani ya chama, suala la uchaguzi wa chama na mjadala wa Katiba ni baadhi ya mambo yatakayoibua mjadala mzito,” alisema mtoa habari wetu.
Mtoa habari wetu alisema kuwa kikao hicho pia kinaweza kuwaweka kiti moto wabunge wa CCM walioungana na wenzao wa upinzani kutia saini za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao hivyo kuanzia jana hadi Mei 11 kutakuwa na vikao vya maandalizi, Kamati ya Maadili kukutana Mei 12 asubuhi na Kamati Kuu (CC) chini ya Rais Kikwete itakutana siku hiyohiyo jioni.
Mei 12 kutakuwa na semina maalumu kwa wajumbe wote wa CC na NEC na Mei 14 itakuwa siku ya NEC.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Nape alisema kuwa vikao hivyo ni maalumu kwa ajili ya wajumbe kujadili mjadala wa Katiba mpya.
Alipoulizwa kama kuna hatua zozote ambazo zitachukuliwa na kwa baadhi ya wabunge waliosaini fomu ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Nape alisema hoja hiyo haipo na haiwezi kuwepo kwani wabunge hao walitoa haki yao Kikatiba kuwawakilisha wananchi wao.
“Kwanza ikumbukwe kuwa Rais akiwa Tanga aliwapongeza wabunge kwa kuonyesha msimamo wao leo itakuwaje Rais tena awageuke na kuanza kuwawajibisha? Hilo halipo kabisa!” alisema.
Katika hatua nyingine, Nape alisema mawaziri wote waliotuhumiwa wawajibishwe kwa uzito wa makosa yao kama watabainika kuhusika.
“Hakuna mtu aliye juu ya sheria, kama mawaziri wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wako ndani ya Baraza la Mawaziri au wale walioachwa ni lazima kila mmoja achukuliwe hatua kadiri ya kosa lake, kama leo hii Rais mstaafu Benjamin Mkapa kafikishwa mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi itakuwa Baraza la Mawaziri?” alihoji Nape.
Chanzo: Tanzania Daima, 9th May 2012
0 maoni:
Post a Comment