MKUU mpya wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, ameahidi kushirikiana na makundi yote ya kijamii ili kudumisha amani ya mji huo wa kitalii na kukuza maendeleo.
Mongela alitoa ahadi hiyo juzi muda mfupi baada kuapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na kusema hawezi kufanya kazi bila kushirikiana na wadau wengine.
“Hakuna miujiza katika kufanya kazi, kwani huwezi kufanya kazi peke yako… lazima ushirikishe wadau, hasa wanasiasa, hivyo nitahakikisha nashirikiana nao ili kuendeleza mji wa Arusha,” alisema Mongela.
Baada ya kuwaapisha wakuu sita wa wilaya za Mkoa wa Arusha, Mulongo aliwaagiza kuchukua hatua katika kurekebisha mambo ndani ya halmashauri zao bila woga.
“Halmashauri zetu, hususani ya jiji la Arusha mwaka huu kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, tumepata hati chafu, hivyo busara haihitajiki hapo, ni kuamua tu kwa watakaobainika kusababisha hivyo,” alisema Mulongo.
Aidha, alimweleza mkuu wa wilaya ya Arusha kuwa anao wajibu wa kufufua kiwanda cha kutengeneza magurudumu ya magari maarufu kwa jina la General Tyre.
Alisema ufufuaji wa kiwanda hicho utachangia kuzalisha ajira kwa wakazi wa mji huo, huku kikiungana na viwanda vingine kusaidia Mkoa wa Arusha kukuza uchumi wake.
Mulongo alisema licha ya mkoa huo kuwa wa tatu kwenye kuchangia pato la taifa hapa nchini, unakabiliwa na changamoto zinazohitaji usimamizi mzuri
Chanzo: Tanzania Daima 21 Mei 2012
0 maoni:
Post a Comment