na Marietha Mkoka
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda, amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege, kwa tuhuma za ubadhirifu.
Kusimamishwa kazi kwa Ekerege kumekuja baada ya kuwepo sintofahamu ya muda mrefu kuhusiana na kukabiliwa na tuhuma nzito za upotevu wa takriban sh bilioni 38 zinazotokana na ukaguzi wa magari nje ya nchi.
Kigoda alitangaza uamuzi huo jana, na kudai kuwa ni kwa ajili ya kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo, ambapo ameunda kamati maalum ya uchunguzi. Hata hivyo, waziri huyo hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na suala la mtendaji huyo mkuu wa TBS.
Waziri huyo aliyeanza kazi wiki iliyopita, alisema ameamua kumsimamisha kazi Ekerege ili kulifanya shirika hilo lirudi katika hali yake ya kawaida ikiwemo kupisha bodi iliyoundwa kutimiza wajibu wake.
Tuhuma dhidi ya Ekerege ziliibuliwa na kamati mbili za kudumu za bunge, ya Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali (PAC), ambapo wajumbe wa kamati hizo waliokwenda kufanya ukaguzi nje ya nchi walibaini madudu mengi, ikiwemo kutokuwepo kwa ofisi za ukaguzi kama ilivyodaiwa na shirika hilo, kiasi cha kusababisha upotevu wa sh bilioni 38.
Wajumbe wa kamati hizo walibaini malipo ya kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi.
Hatua ya kumsimamisha Ekerege, imekuja baada ya mtangulizi wake, Waziri Cyril Chami, kushindwa kumchukulia hatua ikiwemo kumsimamisha, jambo ambalo pamoja na tuhuma nyingine dhidi ya mawaziri kadhaa, lilizua mzozo mkubwa bungeni kiasi cha kuwalazimisha wabunge kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Chami pia inadaiwa alikataa ushauri wa aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyarandu, ambaye alitaka asimamishwe kazi kupisha uchunguzi, na akadiriki kuendelea na msimamo huo hadi alipoachishwa uwaziri wa viwanda na biashara.
Katika utetezi wake, Chami alidai kushindwa kumwondoa mkurugenzi huyo madarakani kwa kile alichodai kuwa mtendaji huyo ni mteule wa Rais kama alivyo yeye. Kauli hiyo, na kubaki madarakani kwa Ekerege, kuliwashangaza wengi ambao waliamini kuwa hakukuwa na sababu ya kutomwondoa kwa vile lengo lilikuwa kutaka tume ya uchunguzi ifanye kazi yake ikiwa huru. Aidha inajulikana wazi kuwa kusimamishwa sio kufukuzwa, na hivyo angeweza kurudi kazini ikiwa ataonekana hana hatia.
Hata hivyo Dk. Kigoda ambaye ni Mbunge wa Handeni hakuwa tayari kuwataja wajumbe wa kamati hiyo ya muda waliopewa kumchunguza Ekerege.
Katika hatua nyingine waziri huyo alisema atainua sera ya kukuza viwanda na biashara ikiwemo kuinua wafanyabiashara wadogo na ushirikiano baina ya serikali na viwanda vidogo.
“Tumepanga kuwasaidia wajasiriamali na kuangalia maeneo ambayo watu wakiwezeshwa watainua uchumi wao na kuboresha utendaji kazi,” alisema.
Alisema kiwanda cha General Tyre kitahitaji kufufuliwa na viwanda vya Pamba na Korosho.
Pia alivisifu viwanda vinavyoiingizia serikali mapato kuwa ni kiwanda cha Saruji Twiga, Sigara (TCC) na viwanda vya bia kutaka viwanda vingine kuiga mfano ikiwemo kuongeza juhudi.
Akizungumzia uwekezaji katika nchi, waziri huyo alisema kuwa suala la kupunguza gharama za umeme halijapata ufumbuzi hivyo juhudi zinahitajika kukabiliana na changamoto hiyo
Source: Tanzania Daima, 19 Mei 2012
0 maoni:
Post a Comment