Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA na Polisi wavutana Mkutano wa Jangwani kesho Mei 26

chademalogo1

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KURUGENZI ya Ulinzi na Usalama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inapenda kutoa taarifa kuwa matembezi ya wanachama wake kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kuhudhuria mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika Viwanja vya Jangwani, yako pale pale kama ilivyopangwa na kutolewa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Itakumbukwa kuwa mkutano huo wa hadhara utakaofanyika Mei 26, 2012 umeshakamilisha taratibu zote, ikiwemo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambalo tayari limesharidhia kushiriki kwa kutoa ulinzi kwa mkutano huo, siku hiyo ya Jumamosi.

Katika barua yetu ya Mei 23, 2012, kwenda kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tulisema kuwa kutokana na hamasa kubwa ambayo imejitokeza kwa wanachama wetu juu ya mkutano huo mkubwa wa hadhara, katika majimbo yote ya jiji na kutokana na hali halisi ya ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wengi unaopelekea kutomudu gharama mbalimbali za maisha zikiwemo za usafiri (nauli za mabasi) wamejipanga kufanya matembezi ya amani, ya mshikamano, kuhudhuria mkutano wa Jangwani.

Katika mazungumzo na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo, tumeona dhahiri kuwa jeshi letu linajenga hoja dhanifu zaidi na kufanya kazi kwa mtindo wa kupiga ramri badala ya kufanya kazi kisasa kwa kutumia hoja yakinifu zenye mantiki, katika kutimiza jukumu lao kubwa la ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Ni vigumu kwa mtu yeyote makini kuweza kukubaliana na hoja za Jeshi la Polisi kuwa hawataki wananchi watembee kwa amani kutoka maeneo mbalimbali kwenda eneo la mkutano eti tu kwa sababu kunaweza kuibuka vitendo vya ukabaji, uporaji katika matembezi hayo! Huku ni kufanya kazi kwa mtindo wa kupiga ramri!

Kumbukumbu zinaonesha kuwa hakuna maandamano yoyote ya CHADEMA yamewahi kuwa na vurugu au vitendo vyovyote vile vya uvunjifu wa amani isipokuwa tu pale ambapo Jeshi la Polisi liliingilia kati na kusababisha vurugu, likapiga watu, likatesa watu hata kusababisha vifo kwa visingizio na hoja zisizokuwa na msingi kama hizi wanazotoa sasa, huku wakitumia lile maneno yao maarufu 'taarifa za kiintelijensia'.

Pamoja na madai ya jeshi hilo kuwa hakuna askari wa kutosha kulinda matembezi hayo ya amani na mshikamano, kutokana na mantiki hiyo hapo juu, hatutashangaa wakipatikana askari wengi wa kuanzisha vurugu, kupiga watu, kutesa na hata kusababisha vifo, kama ambavyo imetokea katika maeneo mengine kwa kisingizio cha kuzuia maandamano.

Imetokea hivyo Arusha, imetokea hivyo Songea (Ruvuma), imetokea hivyo Ikwiriri, Rufiji, ambako Jeshi la Polisi lenyewe limekiri wazi kabisa kuwa lilikuwa chanzo cha vurugu hata wananchi kupoteza maisha. Imetokea hivyo sehemu mbalimbali ambako polisi hudai hawana askari wa kutosha kuwalinda wananchi na mali zao, lakini wanapatikana askari wengi wakati wa kuvuruga na kupiga watu hata kusababisha vifo.

Tunawaomba ndugu zetu wa Jeshi la Polisi watoe ushirikiano kwa wananchi. Wasifanye kazi kwa ubaguzi wa aina yoyote ile katika makundi mbalimbali ndani ya jamii wala maelekezo ya kisiasa, hasa kutoka kwa chama tawala, CCM kama ambavyo imedhihirika mara kwa mara.

Tunapenda kusisitiza kuwa polisi wasifanye kazi kwa mtindo wa kupiga ramri na kujenga hoja dhanifu. Wanachama na wapenzi wa CHADEMA wamedhihirisha mara kadhaa, pasi na shaka yoyote kuwa wanaweza kufanya matembezi ya mshikamano bila kuathiri haki za watu wengine. Kwa amani na utulivu.

Tutaendelea kuthibitisha hivyo Mei 26, 2012, kuelekea Jangwani na mahali pengine popote ambapo tutatumia haki ya kikatiba kufanya matembezi ya mshikamano au kuandamana katika misingi ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, kudai haki, mabadiliko ya kweli katika utawala na mfumo, kudai uwajibikaji wa serikali kwa watu au katika kupiga vita ufisadi na uonevu wa watawala dhidi ya wananchi.

Imetolewa  Mei 24, 2012 Dar es Salaam na;
Wilfred Muganyizi Lwakatare
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama-CHADEMA

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO