Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mbunge aiweka Tanzania kitanzini EAC

Mbunge aliyemaliza muda wake kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Dk. George Nangale, anadaiwa kuiingiza Tanzania kwenye mtego wa ardhi baada ya muswada wa sheria ya masuala ya mazingira kupitishwa na Bunge hilo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema.

Muswada huo 'Transboundary Ecosystems Bill 2010' umekwishapitishwa na Bunge hilo na sasa unasubiri kuridhiwa na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili uanze kutumika rasmi kama sheria.

Pamoja na mambo mengine, muswada huo unataka kuwepo na mfumo madhubuti wa kisheria wa usimamizi wa mazingira ya kiikolojia katika nchi wanachama kwa lengo la kuongeza ubora wa mazingira na pia kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali asili katika EAC.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya wabunge wanaoiwakilisha Tanzania kwenye bunge hilo, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema kupitishwa kwa sheria hiyo ni mtego kwa Tanzania ambayo inataka ardhi isimamiwe na nchi husika.

"Huu muswada uliwasilishwa na mbunge wa Tanzania ni kama aliingia kwenye mtego na tunasikia alishauriwa sana na wenzake lakini hakusikiliza...hatuwezi kukubali mambo ya namna hii," alisema.

Alisema nchi wanachama zimekubaliana kila moja kusimamia ardhi yake na hivyo kuruhusu suala la mazingira ya kiikolojia kuingizwa kwenye jumuiya hiyo ni kukiuka masharti ya ardhi ambayo yamekwishakubaliwa.

"Huwezi kuzungumza mazingira bila kugusa ardhi sasa tunapoanza kuchomeka vitu eti hili lisimamiwe na chombo cha Jumuiya ni kuuingiza tu nchi kwenye matatizo," alisema.

Sitta alikuwa akitoa mada kwenye semina ya wabunge wapya wanaoiwakilisha Tanzania kwenye EALA na kuwataka kusimamia maslahi ya Tanzania na kuwasilisha hoja ambazo zitasaidia kufanikisha malengo ya nchi katika jumuiya hiyo.

Alitaja vipaumbele vya Tanzania katika jumuiya hiyo kuwa ni kilimo kwa ajili ya usalama wa chakula kwa kuifanya nchi iwe ghala la chakula katika kanda ya Afrika Mashariki, viwanda vya kuongeza thamani, miundombinu ya kiuchumi, utalii na nishati kwa kuzalisha na kusambaza umeme wa kutosha jumuiya nzima.

Muswada huo pia unataka kuwepo kwa usimamizi na udhibiti wa mifumo ya ikolojia na kuanzisha Tume ya kusimamia mifumo pamoja na masuala mengine yanayohusiana na mazingira katika Jumuiya hiyo.
NIPASHE ilimtafuta Dk. Nangale jana kwa simu lakini hadi tunakwenda mitamboni hakupatikana.

Muswada huo ulikataliwa baada ya Baraza la Mawaziri wanaoshughulikia EAC kutaka majukumu ya Tume ya kusimamia mfumo wa ikolojia yawekwe wazi kulinganisha na taasisi za mazingira za kila nchi husika.

Awali, akifungua mkutano huo Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema wabunge hao wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano baina ya Bunge la Jamhuri na Serikali kwa kutopata taarifa za mwaka za shughuli za EALA hivyo Bunge kukosa fursa ya kutoa mapendekezo ya majadiliano kwenye bunge la jumuiya.

CHANZO: NIPASHE, 25 Mei 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO