Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Julius Mtatiro azungumzia vurugu za Zanzibar, apinga uchomaji makanisa na matumizi ya nguvu kuzuia uhuru wa kutoa maoni

mtatiroNaibu Katibu Mkuu Bara (CUF), Ndg Julius Mtatiro

HILI LA ZANZIBAR HALIUNGWI MKONO “LABDA NA MWENDA WAZIMU TU”
Habari za uchomaji wa makanisa Zanzibar katika vurugu za hivi karibuni haziungwi mkono kwa namna yoyote ile. Yeyote anayefanya vitendo hivi ni gaidi kwa sababu anafanya vitendo vya kigaidi. Serikali ya zanzibar ichukue hatua kali sana za kisheria kwa yeyote aliyehusika na vitendo hivi bila kujali yeye ni nani.

Kuchoma makanisa ni jambo la hatari sana, sielewi anayefanya hivi yeye ni dini gani, sijui ni dini ipi inayoruhusu uchomaji wa nyumba za ibada za dini nyingine, ni dini ya shetani peke yake inaweza kufanya hivyo.

Kuna watu wanasema ati ni “waislamu” ndiyo wanafanya vitendo hivyo, mie nakataa, nasema wanaofanya hivyo siyo waislamu. Waislamu walioko Zanzibar naowajua mimi ni wakarimu, ni watulivu na wasikivu na wanapenda amani. Hata mapambano ya wafuasi wa CUF na CCM yaliisha kwa wao wenyewe kuridhiana.

Wazanzibari siyo wakatili kiasi hiki. Kuchoma makanisa hakuwezi kufananishwa na kuchoma Mahakama, ikulu,polisi n.k. Uchomaji wa makanisa au misikiti ni uchonganishi mkubwa unaoibua vita mahali pengi duniani. Anayefanya hivyo ana malengo mabaya sana siyo kwa wananchi wa Zanzibar tu bali kwa wananchi wa wa Tanzania kwa ujumla.

Hii ni kwa sababu makanisa yakishachomwa tetesi zinasema wamechoma waislamu(jambo ambalo siliamini), tetesi hizi zikizidi na pakatokea athari kubwa kwa makanisa na labda watu(wakristo) wakachomwa na kufariki ndani ya makanisa hayo, ina maana wakristo watapoteza ndugu zao.

Kama Zanzibar pana wakristo wachache ambao hawawezi kulipiza kisasi cha adui wasiyemjua, lazima ndugu zao wakristo walioko bara watataka kulipiza kisasi kwa wazanzibari(waislamu) walioko Tanganyika ambao wamejenga na kuoa na kufanya biashara Bara na ambao hata ZAN ID(Vitambulisho vya ukaazi vya Zanzibar hawana) – kwamba kwa sheria za uraia za Zanzibar hata wakirudi kesho hawatambuliki kama wazanzibari.

Nakadiria kuwa kuna wazanzibari takribani laki tatu au laki nne walioko Tanganyika. Wengi wao wana maduka na biashara nyingi, wamenunua mashamba yao huku Tanganyika na kwa kweli maisha yao na vifo vyao na maziko yao viko huku Tanganyika kila inapotokea.

Sasa fikiria hawa “magaidi” wanaojivalisha na kusingizia waislamu watakapoendelea kutuchonganisha na tukajikuta hasira zimepanda kila upande. Utastukia mali za wakristo na makanisa yanachomwa na hata wahusika kuuawa huko Zanzibar na utastukia pia wazanzibari walioko Tanganyika nao wanaanza kuhujumiwa mali zao na kuuawa na “magaidi” wa bara watakaojivisha joho la “ukristo” au “joho la kuwapigania ndugu zao waliouawa Zanzibar” kwa maslahi yao.

Mchezo huu utaendelea mbele, kwa sababu wazanzibari wengi watakaouawa na kuhujumiwa huku Tanganyika ni waislamu(hii ni kwa sababu asilimia 99 ya wazanzibari ni waislamu) itapelekea waislamu wenzao ambao ni mamilioni walioko Tanganyika kutaka kuwatetea waislamu wenzao wenye asili ya Zanzibar. Hapo ndipo itaibuka vita kamili ya dini ya kikristo na kiislamu(Naomba haya yatokee wakati sipo duniani, naomba nisishuhudie ukatili wa Rwanda ndani ya nchi ninayoipenda kama Tanzania).

Vita ya kidini, lol! Mamilioni watateketea, malaki watachinjwa, akina mama watabakwa, watoto watanajisiwa…..what a hell? Wendazimu wachache waliochekewa watavaa majoho ya dini…..CNN watatangaza vita ya kidini Tanzania, Mashirika ya kimataifa yataingiza misaada na geresha huku nchi inahujumiwa. Vikundi vya waasi kina Kony na mwenzie nao wataingia kutuunga mkono, hatimaye Tanzania itageuka kuwa jehanamu ya duniani. Nyerere na wenzie watakuwa wanalia na kupiga vifua vyao kwa huzuni kuu. Kisiwa cha amani kimegeuka kuwa Dimbwi la maafa na laana ya damu za mauaji.

Mambo haya huanza kama mchezo tu. Na yameanza, hakuna mtu mwenye haki ya kudai haki yake na kuhujumu mali za watu wengine na kuchoma makanisa ya watu wengine. Wanaofanya vitendo hivi ni wahuni wakuu na serikali ya Zanzibar ichukue hatua kali sana.

Uhuni wa namna hii ulitokea pale Tandahimba mwezi uliopita ambapo “polisi” walihusika “live” katika oparesheni ya kikatili ya kuchoma “waziwazi” maduka zaidi ya 55 ya wafanyabiashara na gari moja na pikipiki moja. Kabla hawajaanza oparesheni “ushenzi” hiyo “polisi” walitengeneza tukio kwa “kuichoma” ofisi ya OCD ili wapate nafasi ya kulipiza kisasi kwa wananchi wasio na hatia(kisasi cha kutengeneza) – Ujinga ulioje, aibu iliyoje?

Pana makundi yanadai Zanzibari huru, yaachiwe uhuru wao, yasikilizwe. Wajanja wasijitokeze wakatumia upenyo huo ili kuyavunja makundi hayo kwa kuyabambikizia uchomaji makanisa ili kuyahusisha na hila za dini moja kuhujumu dini nyingine, tuache michezo hii ya kipuuzi. Siamini kama uamsho na wanaharakati wale ndio wanachoma makanisa, naamini kuna janja nyuma ya suala hili. Labda pana wajanja wanataka kuua “move” ya mjadala wa kudai Zanzibari huru.

Majuzi wazanzibari waliamua kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, wakapiga kura wakaamua sawia na serikali yao ikawa, hawakutushirikisha kwa sababu peke yao wanaweza kusimamia na kuendesha mambo yao na tumeona wanaweza. Mie nasema wazanzibari wakidai Zanzibar huru yao tusiwapige na kuwakamata na kuwanyanyasa, tukae nao mezani tusikilize hoja zao. Na kama wengi wao wakitaka Zanzibar huru yao tuwape.

Baba yangu mzee aliyeko kijijini hatapungukiwa na lolote iwapo Zanzibar itaendeleza muungano na Tanzania au itajitoa. Zanzibar ikijitoa katika muungano haitaongeza wala kupunguza kilo ya sukari au kilo ya mchele. Watanzania wana matatizo makubwa yanayotishia uhai wao kila kukicha kuliko muungano huku Tanganyika . Muungano ni jambo la kisiasa tu na kama “mkuu wa kaya anasema usijadiliwe” lazima utavunjika tu, hana namna ya kuuokoa maana kushindana na umma wa upande mmoja ni kazi bure.

Mie nawashauri sana pia wana vikundi vya uamsho na na watu wote wanaodai Zanzibari yao kuwa watumie busara na njia za kawaida sana kudai haki yao wanayoiamini. Kwa sababu tume ya jaji warioba inakwenda kukusanya maoni ya katiba waisubiri, ikifika waioneshe na waieleze kuwa hawautaki muungano.

”Majority of zanzibaris” wakiwa na msimamo huo maana yake ni kuwa katiba ya Tanzania “itafeli” kwa sababu lazima ipitishwe na pande zote za muungano kwa uwiano sawa. Hii ni njia nyepesi sana kuliko njia zingine, wanaweza kuendelea kutoa elimu juu ya kuupinga muungano kwa njia ya makongamano na mikutano tu. Hii itawasaidia kutengeneza mtizamo mzuri na kuondoa uwezekano wa watu wowote wenye nia mbaya kutumia shughuli zao na kujenga taswira mbaya sana zinazoweza kuweka amani, usalama na mshikamano wa wananchi hatarini.

Mwisho ni kwa serikali zote mbili, hii ya Jakaya na ile ya Shein na Maalim Seif. “Movement” hii ya uamusho na makundi mengine ya kijamii, kiharakati na kidini upande wa Zanzibar ya kudai kuvunja muungano siyo jambo la kubeza na kuchezea. Ukiwatizama wale uamsho utaona umati wa watu wanaokusanya ni mkubwa kuliko mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Hii ina maana kuwa panahitajika busara na nia thabiti katika kumalizana na wananchi hawa.

Serikali zote mbili zikae nao chini na kutatua suala hili. Ni bora kuuvunja muungano kwa heri(kwa utaratibu), kuliko kuuvunja kwa nguvu. Muungano ukivunjika kwa nguvu na ghafla patatokea mpasuko mkubwa sana. Pana ma-laki ya wazanzibari wako Tanganyika, pana mahusiano makubwa yameshajengwa. Tunahitaji “mechanism”na akili nyingi kulishughulikia.

“Nguvu na mabavu havitasaidia kuzima mawazo thabiti ambayo wananchi wanayaamini, nguvu na majeshi vinaweza kuua mwili tu lakini haviui dhamira” Hata kama wananchi hawa watapigwa na kukamatwa na kuwekwa gerezani moto huu hautazimika. Muungano utizamwe upya, tusikilize matakwa ya wananchi wengi, ikiwa wengi watasema uvunjwe basi na tuuvunje kwa amani.

(Haya ni maoni yangu binafsi, kwa namna yoyote ile yasihusishwe na chama changu wala uongozi wangu ndani ya chama).
Julius Mtatiro +255 717/787/ 536759,
Dar es salaam,
29 Mei 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO