Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA kimeacha historia ambayo ni vigumu kufutika katika uzinduzi wa operesheni Sangara kanda ya kati uliofanyika Ifakara-Kilombero jana.
Katika mkutano huo ulikusanyika umati mkubwa kuwahi kushuhudiwa katika wilaya hiyo kwa miaka ya karibuni.
Akihutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi katika mkutano huo jana, ikiwa ni sehemu ya Operesheni Sangara awamu ya pili, Kiongozi mkuu wa upinzani nchini ambaye pia ni Katibu mkuu wa CHADEMA Dk.Wilbroad Slaa aliyeambatana na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa Serikali ya CCM imekuwa na kiburi cha kuwatisha wanaotaka kutetea maslahi ya wananchi huku ikifungia hata vyombo vya habari kama Mwanahalisi.
“Serikali ina nguvu ya kuvifungia vyombo vya habari kwa sheria dhalimu ya magazeti ya mwaka 1977, lakini kamwe haitaweza kuzuia kina Dr Slaa kupiga kelele'' alisema kiongozi huyo. Dk. Slaa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu na halaiki hiyo huku anga likihanikizwa kwa kelele za RAIS....RAIS...RAIS...., aliongeza kuwa, kuanzia sasa CHADEMA itaanzisha mapambano kwa ajili ya haki ya Watanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe alisema umati uliokusanyika unaonesha namna wakazi wa Kilombero walivyomthamini aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, marehemu Regia Mtema.
Mbowe aliomba jina la uwanja wa Ifakara libadilishwe na kuitwa Uwanja wa Ukombozi, na kwamba hali hiyo iwe chimbuko la ukombozi kwa Mkoa wa Morogoro.
Aliwataka wakazi wa Kilombero kuacha kulalamika na badala yake wachukue hatua kwa kuachana na CCM na kujinga na CHADEMA.
Katika mkutano huo maelfu ya wananchi walijiunga na CHADEMA wengi wao wakiwa ni kutoka CCM.Mara baada ya mkutano huo baadhi ya watu walionekana wakifuta machozi huku wakisema wanaamini bado siku chache tu CHADEMA kuingia madarakani na kukomboa watanzania kiuchumi.
Mbali na Dk. Slaa na Mbowe, viongozi wengine waliokuwa katika msafara huo ni Joshua Nassar (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Hamad Yusuph (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Suzan Kiwanga (Viti Maalumu), Joyce Mukya (Viti Maalumu) na wengine wa makao makuu.
Picha & Maelezo: Chadema Blog
0 maoni:
Post a Comment