Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo, Bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
Reginald Miruko na Daniel Mjema, Dodoma
SERIKALI imesema eneo linalogombewa na Malawi katika Ziwa Nyasa ni mali ya Tanzania na sasa imeziamuru kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa mafuta kuondoka eneo hilo kuanzia jana.
Onyo hilo dhidi ya Malawi lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia amesisitiza kuwa Tanzania itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Hii ni mara ya pili Serikali kuionya Malawi katika mgogoro huo. Wiki iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni Samuel Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi.”
Sitta alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana, akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13, bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo (jana),” alisema Membe.Alisema Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na haitaruhusu utafiti huo wa uchimbaji wa gesi na mafuta uendelee.
Alisema chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Kiini cha Mgogoro
Kuhusu kiini cha mgogoro, Waziri Membe huku akirejea historia ya mipaka tangu ukoloni, alisema ni hatua ya Serikali ya Malawi kushikilia msimamo kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi wakati Tanzania inashikilia kuwa mpaka upo katikati ya Ziwa.
“Wenzetu wanadai ziwa lote lipo Malawi lakini, nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati,” alisema.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo baina ya Cameroon na Nigeria.
Alisema katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Dunia, iliamuliwa kuwa mpaka baina ya nchi hizo mbili upite katikati ya Ziwa Chad ukifuata msitari ulionyooka.
“Ni dhahiri, tunalo tatizo kati ya Tanzania na Malawi linalohitaji kutatuliwa kuhusu mahali hasa ulipo mpaka baina ya nchi hizi mbili na lilianza tangu enzi ya awamu ya kwanza,” alisema.
Waziri Membe alisema tatizo hilo lilishindwa kupatiwa ufumbuzi kutokana na Rais Kamuzu Banda wakati huo akiwa madarakani kuamini kuwa ‘Tanzania ilikuwa ni kichaka cha kuhifadhi maadui wa Serikali yake.’
“Baada ya mabadiliko ya uongozi, tulianza kujadili tatizo hilo kwa njia za kidiplomasia na mwaka 2005 iliundwa tume ya pamoja ya kushughulikia mgogoro huo,” alisema.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alikutana mara mbili na Rais wa zamani wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika na kukubaliana iundwe Tume ya Pamoja ya wataalamu kushughulikia mgogoro huo.
Hata hivyo, alisema wakati tume hiyo ikianza kukusanya nyaraka mbalimbali, suala hilo lilichukua sura mpya na kuanza kuhatarisha usalama wa Tanzania na wananchi wake.
Alisema Serikali ilipata habari za kuaminika kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa, kaskazini ya Msumbiji limegawanywa katika vitalu mbalimbali.
“Kwamba Serikali ya Malawi ilitoa vitalu hivyo kwa kampuni za kutafuta mafuta na gesi na yakaomba kibali cha kuruhusu ndege za utafiti ziruke katika anga la Tanzania,” alisema.
Waziri Membe alisema ombi hilo lilikataliwa na JWTZ lakini, Serikali imepata ushahidi kuwa ndege ndogo tano za utafiti zenye uwezo wa kutua ufukweni na majini zilionekana zikivinjari na kutua Ziwa Nyasa upande wa Tanzania Januari 29 na Julai 2 mwaka huu.
Alisema Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Malawi kwa maandishi na kuomba ufanyike mkutano wa mawaziri na wataalamu wa nchi mbili kuhusu mustakabali wa mpaka wa nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulifanyika Tanzania Julai mwaka huu na baada ya majadiliano, pande zote mbili zilikubaliana kwa kauli moja kwamba lipo tatizo baada ya kila upande kushikilia msimamo wake.
Alisema pande zote mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo hayo Agosti 20 hadi 27 mwaka huu, nchini Malawi ukihusisha wataalamu wa mipaka na sheria za kimataifa wa nchi hizo mbili.
“Katika mkutano huo, Serikali ya Tanzania iliitaka Malawi kutoruhusu mtu au kampuni yoyote kuendelea na shughuli za utafiti na tunaonya hatutaruhusu utafiti huo uendelee,” alisema.
Alisema Serikali inathamini uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuitaka Malawi kuheshimu makubaliano na kuongeza kwamba njia nzuri na bora ya kutatua tatizo hilo ni ya mazungumzo ya amani.
“Katika kipindi chote cha mazungumzo Serikali ya Malawi isiruhusu shughuli zozote za uchimbaji wa madini na mafuta katika eneo hilo kwa sababu ni eneo la Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa Serikali inayo dhamana ya kuwalinda wananchi 600,000 wanaoishi na kutegemea Ziwa Nyasa.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa alisema tamko hilo la Waziri linaonyesha kwamba kilichopo sasa baina ya nchi hizo ni kutunishiana misuli.
Alisema vita si suluhisho la mgogoro huo na kushauri kuwa iwapo Malawi imeweka watafiti wa mafuta ziwani, Tanzania nayo itafute wa kwake nao waanze kutafiti.
Alisema inavyoonekana mgogoro huo hauwezi kumalizika kwa mazungumzo yanayofanyika Dar es Salaam, bali kufikishwa kwa wasuluhishi wa kimataifa, The Hague.Malawi yajibu mapigo
Wakati huo huo
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Malawi, Patrick Kabambe alikaririwa na Redio Sauti ya Ujerumani jana jioni akisema kuwa wataendelea na utafutaji wa mafuta na gesi katika Ziwa Malawi huku akidai kwamba amesikia Tanzania inapeleka askari eneo hilo.
Waziri huyo alisema hilo ni Ziwa Malawi na siyo Nyasa na kueleza kuwa utafutaji wa mafuta na gesi utaendelea na hakuna wa kuwasimamisha huku akihoji Tanzania kuja juu sasa na si wakati mwingine.
“Tutaendelea kutafuta mafuta na gesi katika Ziwa Malawi na tunashangaa kwa nini sasa ndiyo wanalalamika na siyo wakati mwingine?” alikaririwa akisema.
Published by Mwananchi on 7th August, 2012
0 maoni:
Post a Comment