Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

FIFA yapewa ‘tano’ uchaguzi TFF

Mh Amos Makalla (kushoto ) akiwa na Angetileh Oseah. Picha na Shafih Dauda

***********************

na Clezencia Tryphone

WAKATI Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikitarajiwa kukutana Mei 9 kujadili maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa (FIFA), kuanza upya mchakato wa uchaguzi, serikali na wadau mbalimbali wamejitokeza kupongeza agizo hilo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kikao hicho cha dharura chini ya uenyekiti wa Rais Leodegar Tenga, kitakuwa na ajenda hiyo moja tu, katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.

FIFA katika maelekezo yake, imetaka kwanza iundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF, ambao unatakiwa ufanyike kabla ya Oktoba 30, mwaka huu.

MALINZI ANENA

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea nafasi ya urais wa TFF na kukatwa kwa madai ya kukosa uzoefu, Jamal Malinzi, aliishukuru FIFA kwa uamuzi huo na kubainisha kuwa ataendelea kugombea kiti hicho muda utakapofika.

Malinzi alisema azma yake ya kuwania nafasi hiyo iko palepale na kudai kuwa hajatetereshwa na chochote.

“Sijatetereka na lolote, wadau, umma wa Watanzania na wajumbe wa mkutano mkuu wajue hilo na muda ukifika nitaomba ridhaa ya wajumbe ya kuwa Rais wa TFF,” alisema Malinzi.

Aidha Malinzi alisema huu ni wakati wa TFF, kupitia Kamati ya Utendaji na Rais Tenga, kuwa makini na maamuzi yake na isijefanya mambo yakarudi nyuma ambako yametoka mpaka kufikia hapa sasa.

“Inahitajika umakini mkubwa, ili tusije tukarudi kule tulikotoka ambapo mteuliwa wa Rais wa TFF, alidiriki kumbeza rais wa TFF, kwa kumwambia hadharani kuwa Tenga hajasoma sheria na wengine tukaambiwa hatujawahi kuongoza mpira bali tuliongoza bonanza.

“Kwa mujibu wa katiba ya TFF viongozi wanapatikana kwa kura, hivyo basi turuhusu sanduku la kura litupatie viongozi,” alisema Malinzi.

Malinzi aliongeza kwa kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu, kuhakikisha TFF inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na pale watakapoona inapindishwa wasisite kuwa wakali.

SERIKALI NAYO

Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, alisema kuwa uamuzi uliotolewa na FIFA, umeweza kuondoa hali ya sintofahamu ambayo ilikuwa imetawala katika uchaguzi huo na ni wakati muafaka hata kwa wale walioshindwa kujitosa kipindi hicho, kufanya hivyo sasa.

Alisema hata katika baadhi ya vitu ambavyo vimeonekana kutolewa uamuzi ni vile ambavyo hata serikali ilivitaka vifanyiwe kazi na kudai kuwa kwa sasa wanasubiri Kamati ya Utendaji ya TFF ikutane na kupanga ratiba ya mchakato, ikiwemo mkutano mkuu wa dharura wa kubadili katiba.

“Nilipoingilia mchakato TFF, wasiopenda haki walinidhihaki sana, nashukuru FIFA wamethibitisha hili....namshukuru Tenga kwa ushirikiano alioipatia serikali, nawashukuru wadau wa mpira wa miguu kwa ushirikiano na utulivu waliouonyesha wakati wa kipindi kigumu cha sintofahamu,” alisema Makalla.

WADAU NAO

Baadhi ya wadau, nao wameunga mkono uamuzi huo wa FIFA, huku wakiitaka TFF kuwa makini na maamuzi ya sasa ili zoezi hilo liweze kufanyika bila ya kuwa na kigugumizi kama awali.

Wadau hao, Athuman Makaranga, aliyekuwa Katibu Mkuu Yanga (Mwesigwa Selestine) pamoja na Wallace Karia aliyekuwa mgombea wa Makamu wa Rais wa TFF, kila mmoja alionyesha kuridhishwa na FIFA.

Makaranga alisema uamuzi wa FIFA ni mzuri, ila amebaki na sintofahamu kuona Kamati ya Uchaguzi na ya Rufaa zilizoboronga uchaguzi huo kuendelea kupeta na kudai kuwa wasipokuwa makini hali itakuwa tete zaidi ya awali.

Karia, kwa upande wake alidai kuwa hilo ni funzo kubwa kwa soka hapa nchini na kuwa wadau wengi walijua FIFA itaegamia upande wa TFF pekee, huku akiwataka wale ambao walikosa nafasi za kuwania awali, wajitokeze huku yeye akidai kuwa bado hajajua kama atawania nafasi hiyo kwa sasa.

Kwa upande wake, Mwesigwa alisema, “Uamuzi wa FIFA kutaka mchakato wa uchaguzi wa TFF uanze upya ni wa kupigia saluti. Katika hili hakuna mshindi ila mpira wa Tanzania ndio una nafasi kubwa ya kuwa mshindi, kwani uanzishwaji wa kamati mbili za nidhamu (lower & upper disciplinary bodies), utakuwa wa tija iwapo kamati hizo zitaongozwa kwa uadilifu chini ya watu waadilifu,” alisema Mwesigwa.

Aidha Mwesigwa alisema kamati hizo zitachuja na kupunguza vichocheo vya migogoro, ambavyo mara nyingi ni matokeo ya ubinafsi, uchu wa madaraka, rushwa na hata uelewa mdogo/potofu wa sheria na taratibu za soka.

“Ni matumaini yangu kwamba huko mbeleni wadau wa michezo watafikiria kuwa na chombo cha kitaifa cha usuluhishi na upatanishi wa michezo (National Sports Mediation and Arbitration), hii inaweza kuiepusha dola (serikali, mahakama na Bunge), kuwa sehemu ya migogoro ya michezo kama tulivyoona katika sakata la FIFA,” aliongeza Mwesigwa

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO