Mamia ya watu walijitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo (38), aliyeuawa kwa kukatwa shingo na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 28, 2012 umbali mfupi kutoka nyumbni kwake, Usa-River.
Baadhi ya barabara za jijini Arusha zilifungwa kwa muda, na baadhi ya shughuli zikisimama kwa muda ili kuruhusu watu kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu katika Hospitali ya Mt Mero kuanzia saa 3 asubuhi.
Askari wa kikosi cha usalama barabarani, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Thobias Andengeye, waliongoza msafara wa magari kutoka katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru hadi nyumbani kwake marehemu eneo la Magadini, Usa River kisha kanisa la Wasabato Liganga ambako ilifanyika ibada na baadaye kusindikiza katika Uwanja wa Ngaresero ambako hotuba na heshima za mwisho zilifanyika.
Viongozi mbalimbali wa CHADEMA na serikali waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, wabunge Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Vicent Nyerere (Musoma Mjini) na Cecilia Paresso (Viti Maalumu).
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Naibu Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu, kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Silla.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Msafiri Jonathan Mbwambo (38) likishushwa kwenye gari kwa maandalizi ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho katika viwanja vya Ngusero, Usa-River jana. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, viongozi wa chama, RPC wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, OCD wa Arumeru na wananchi wengine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye (katikati) akifuatilia hotuba za wasemaji wa makundi ya jamii yaliyowakilishwa. Kutoka kushoto anaonekana kwa mbali Mh Vicent Nyerere (Musoma), Mh Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Mh Godbless Lema, Mh Cecilia (Viti Maalumu), Kamanda Andengenye, na OCD John wa Arumeru
Kamanda Andengenye akisalimia wananchi. Baadae aliahidi kuwa Jeshi lake litatoa zawadi ya shilingi milioni 10 kwa mtu atakaesaidia kupatikana kwa waliohusika na mauaji hayo na kwamba Polisi watahakikisha wanawasaka wahalifu hao kwa udi na uvumba hadi wapatikane.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mh Joshua Nassari (CHADEMA) akizungumza kwa hisia kuhusiana na mauaji yanayowaandama viongozi wa chama chake
Mbunge wa Musoma, Mh Vicent Nyerere akitoa heshima za mwisho. Mh Vicent ndie alieteuliwa kuwakilisha chama chake katika maziko yanayofanyika leo kijijini kwa Marehemu, Same-Kilimanjaro
Kuna walioshindwa kujizuia na kuishia kuangua kilio. Simanzi kubwa
Msiba ulikuwa mchungu kwa kada nyingine za siasa pia, na si CHADEMA pekee
Kuna waliopandisha mori kama huyu mama. Hapa anaondolewa eneo la viwanja hivyo
Aliekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema akielekea kutoa heshima za mwisho akiwa ameambatana na mtoto wake. Nyuma yake ni Mbunge mpya Viti Maalumu, Mh Cecilia aliechukua nafasi ya marehemu Regia Mtema aliekufa kwa ajali ya gari mapema mwaka huu.
Watoto walioachwa na marehemu, Nazaeli (14), Helen (10) na Magreth (6).
Mke wa marehemu, Eunice akifarijiwa na majirani zake.
Baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana CHADEMA Mkoa wa Arusha wakijadiliana jambo ukiwa unasubiriwa msafara wa kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Same uanze kuondoka
0 maoni:
Post a Comment