Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

HABARI KAMILI KUHUSIANA NA MLIPUKO WA “BOMU” KANISANI ARUSHA JANA

Na Mwandishi wa Tanzania Daima

picha za tukio la bomuBaahdi ya waumini wa dhehebu la Katoliki wakiwa wameanguka chini na kushindwa kuinuka baada ya kujeruhiwa na mlipuko unaodhaniwa kuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono uliotokea jana katika Kanisa la Mt Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Shambulio hilo lilitokea wakati ibada ya kuzindua Parokia ya Mt Joseph Mfanyakazi ambapo Balozi wa Papa Askofu Mkuu Fransisco Padila akiwa mgeni rasmi na mwendesha ibada hiyo.

Balozi wa Vatican nchini,Askofu Mkuu Fransis akiondolewa kwenye eneo la Kanisa hilo kwa usalama wake. Picha na Filbert Rweyemamu


****************************************

WATU wawili wamekufa na wengine 66 kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu wakiwa katika ibada ya kutabaruku parokia mpya ya Olasiti, jijini Arusha jana.

Mlipuko huo umetokea huku kukiwa na vuguvugu la machafuko ya kidini nchini pamoja na onyo la Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, kuwataka Watanzania wawe macho na magaidi wa vikundi vya Al Shabab na Al-Qaeda wanaoweza kufanya mashambulizi wakati wowote.

Miongoni mwa walionusurika ni balozi wa Baba Mtakatifu nchini Mhashamu Askofu Mkuu Francisco Padila, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Arusha Josephat Lebulu, mapadri na waumini waliohudhuria ibada hiyo.

Kati ya watu waliojeruhiwa, wengine walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao walifika kusali katika kanisa hilo walisema lilikuwa la kushtukiza baada ya kitu ambacho wanadai kilikuwa katika mfuko wa Rambo kilipodondoka nje ya jengo la kanisa hilo na kulipuka.

“Kwa kweli tukio hili lilikuwa la ghafla sana ambalo hatukulitegemea kwa kuwa waumini wote tulikuwa tukimuangalia Askofu Mkuu akikaribia kukata utepe na ghafla ukatokea mlipuko huo na kuzua taharuki kubwa kwetu,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Mpaka wakati tunaelekea mitamboni jeshi la polisi lilikuwa likimshikilia mtu mmoja kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo akidaiwa ndiye aliyerusha kitu kilichosababisha mlipuko huo katika kanisa hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, baada ya kufika katika eneo la tukio aliwataka waumini kutulia na kutohusisha tukio hilo na dini yoyote.

“Ndugu zangu tukio limeishatokea….., ni tukio kama mengine; tutulie linafanyiwa uchunguzi na tusilihusishe tukio hilo na dini yoyote,” alisema.

Mulongo alipata wakati mgumu wakati akitoka katika Hospitali ya Mount Meru baada ya kikundi cha wananchi waliokuwepo hapo kuanza kumzomea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kwa uchunguzi kuhusiana na mlipuko huo.

Kamanda Sabasi alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuchunguza sampuli za mchanga waliochukua katika eneo hilo la tukio ili kujua mlipuko huo umetokana na kitu gani.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, akiwa ameongozana na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, walifika katika kanisa hilo na kuamsha kelele za kushangiliwa na wananchi kujisahau kama kuna janga limetokea katika eneo hilo.

Akizungumza katika eneo hilo, Lema aliwapa pole waliofikwa na maafa hayo huku akilitaka Jeshi la Polisi kutumia nguvu ileile waliyoitumia kumkamata yeye kufanikisha kukamatwa wahusika wa tukio hilo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Frida Mokitu, alithibitisha kupokea majeruhi 42 na kuelezea kifo cha watu wawili ambao hawakulitambuliwa majina yao kwa wakati huo.

Majeruhi wengine 16 walipelekwa katika Hospitali ya Seliani iliyoko katikati ya jiji la Arusha wakiendelea kupata matibabu na wagonjwa wengine wawili wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Baadhi ya majina ya majeruhi iliyopatikana jana walioko katika Hospitali ya Mount Meru ni Concesta Julius Mbaga, Edith Ndowo, Christopher Raymond, Frank Donatus, Deborah Joakim, Elizabeth Isidory, Beather Cornel, Neema Daudi na Anold Alex.

Wengine ni Sophia Kimolo, Lightness Nelson, Theophilda Inocent, Jackline John, Faustin Andrea, Regina Daud, Donald Swai, Restuta Alex, Alfonce Nyakondi, Mathias Kiya, Anna Didas, Albert Njou, Flomena Nyereza, Dereck Kessi, Mary Okeere na Joyce Okeele.

Aidha wengine ni Doreen Pankaras, Fatuma Tarimo, Faustin Andrea, Anna Didas, Anastazia Regine, Anna Kessy, Elizabeth Masawe na Faustin Shirima.

Utoaji damu

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Arumeru Mashariki na kada wa CHADEMA James Ole Millya waliwahamasisha wananchi wa Arusha kujitokeza kujitolea damu kwa ajili ya kusaidia matibabu kwa majeruhi.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Lema alisema, “Nimewahamasiha wapigakura wangu wafike kujitolea damu, zoezi hili limeongozwa na Nassari na Ole Millya nitafuatia mimi, na vijana wengi zaidi ya 200 wamefuatana nasi tuko hapa hospitali ya mkoa, maana tunajua katika hali hii ndugu zetu wanaweza kuhitaji damu.”

Akizungumzia tukio hilo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino, Padri Charles Kitima, alisema kitendo hicho ni uhalifu uliotendwa ili kuvuruga ibada.

“Kama ni bomu tujiulize nini kinaingia nchini, nyumba za ibada ni tulivu, ni mahali ambapo tunapaswa kukimbilia hivyo hatutegemei vitu kama hivi kutokea huko, ila tusubiri taarifa ya jeshi la polisi, serikali inapaswa ijiulize ni kwa nini kwenye nyumba za ibada, ingawa tunatoa tahadhari kuwa uhalifu huu usihusishwe na mapenzi ya Mungu, ni maslahi ya waovu kwa maslahi ya kutesa watu.”

Wananchi wavunja geti

Wakati majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru, mgonjwa mmoja ambaye jina halikupatikana alizidiwa hali iliyolazimu ahamishiwe KCMC lakini gari la wagonjwa lililombeba mgonjwa huyo lilipofika getini halikufunguliwa kutokana na kutokuwapo kwa walinzi.

Kutokuwapo kwa walinzi hao kuliamsha hasira za wananchi ambao waliamua kusubiri kwa dakika 10 na baada ya hapo waliamua kuvunja geti la hospitali hiyo ili kuruhusu gari liwahi KCMC.

Bilal, IGP Mwema wazuru

Wakati huohuo Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, walifika eneo la tukio jana jioni kuwajulia hali majeruhi na kutoa pole kwa waliofikwa na maafa hayo.

Dk. Bilal alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake huku akiwataka watu wa dini mbalimbali kukaa kwa amani na kuepusha chokochoko ya aina yoyote ile.

Dk. Bilal aliamua kumchukua mtoto wa kiume Anorld Alex (10) aliyeumia katika tukio hilo na kuahidi kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili akapatiwe matibabu kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Tukio la Arusha

Tukio la jana limetokea siku chache tu baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Saidi Mwema, kusema zipo dalili za kuibuka makundi ya kigaidi ndani ya nchi yakiratibiwa na makundi ya Al-Qaeda na Al-Shabab.

Mwema alitoa kauli hiyo April 21 visiwani Zanzibar kwenye semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo aliwakilishwa na Kamishna Mwandamizi wa Polisi Hussein Nassor Laisseri, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu hali ya uhalifu Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

Matukio ya kigaidi yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchi jirani ya Kenya ambapo inadaiwa kikundi cha Al Shabab kimekuwa kikiendesha matukio hayo kupinga serikali ya Kenya kupeleka majeshi yake nchini Somalia.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO