Kwa matokeo hayo ya viti sita kwenda CHADEMA, ni wazi kuwa nafasi ya kuongoza Halmashauri ya Mji mdogo wa Usa River itachukuliwa na chama hicho kwa maana kwamba tayari wanakura nyingi endapo kila chama kitapigia upande wake! Viti maalumu pia vinaweza kuongeza idadi ya kura za Chadema katika kumchagua meya wa Halmashauri ya Mji huo mdogo wa Usa River.
Chadema waliibuka washindi kwa kuchukua uenyekiti wa mitaa ya Mji Mwema, Kisambale, Manayata Kati na Banana.
Mitaa mingine ni Magadini na Ngarasero ambao ulielezwa kuwa ngome kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM katika mji huo.
CCM kwa upande wao waliweza kujinyakulia mitaa yaMlima Sioni, Magadirisho na Usa Madukani.
TAARIFA ZAIDI KUHUSU UCHAGUZI HUO KAMA ILIVYOANDIKWA NA GRACE MACHA WA TANZANIA DAIMA INAELEZA…..
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kudhihirisha umwamba wake katika Mkoa wa Arusha, ambapo kwa mara nyingine tena kimeipiga kikumbo CCM na kutwaa halmashauri mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Usa River.
Ushindi huo unakuja zikiwa ni siku chache tangu chama hicho kiitwae Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha ambayo ilikuwa ikiongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi, aliyefariki dunia.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Halmasuri ya Arumeru Mashariki kugawanywa, na hivyo kuunda halmashauri mpya ya mamlaka ya mji mdogo wa Usa River.
Kabla ya kugawanywa, mitaa yote ilikuwa ikiongozwa na CCM na hivyo, ikalazimika viongozi hao wajiuzulu ili uchaguzi ufanyike upya wa kuwapata wenyeviti wapya wa mitaa tisa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, tayari CHADEMA kilikuwa kimejizolea ushindi mkubwa katika mitaa sita, huku CCM kiking’ara kwenye mitaa mitatu.
Mitaa hiyo na kura zake kwenye mabano ilikuwa Manyata Kati (CHADEMA 118, CCM 78), Nganana (CHADEMA 127, CCM 117), Kisambare (CHADEMA 613, CCM 190), Ngarasero (CHADEMA 785, CCM 355) na Magadini ambako CHADEMA walipata kura 303 dhidi ya 106 za CCM.
Hata hivyo, CCM ilifanikiwa kurejesha mitaa mitatu ya Magadirisho, Mlima Sioni na Usa Madukani.
Kwa ushindi huo, CHADEMA sasa wamefanikiwa kuongoza halmashauri ya pili katika Mkoa wa Arusha, kwani kwa zaidi ya miaka kumi wamekuwa wakiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kuwa wanataka kuifanya halmashauri mpya ya Usa River iwe ya mfano katika Jiji la Arusha.
“Tumejipanga kuiboresha Usa River kuanzia usafi, mapato na miundombinu yake, kwani CCM wamekuwa wakisuasua, lakini sasa wameachia,” alisema.
CHADEMA kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa CCM katika Mkoa wa Arusha kwani hata kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, chama hicho kilitwaa kiti hicho kilichokuwa kikikaliwa na wapinzani wao baada ya aliyekuwa mbunge kufariki.
0 maoni:
Post a Comment