CHAMA cha mapinduzi(CCM) mkoani Arusha kinataraji kumpokea na kumkaribisha nyumbani katibu mkuu mteule wa CCM taifa, Abdulraham Kinana leo katika uwanja mdogo wa ndege uliopo Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo pia atapata fursa ya kuwahutubia wafuasi wa chama hicho mkoani Arusha katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, sanjari na kufungua mashina mbalimbali ya wakereketwa.
Katika ziara hiyo Kinana ataambatana na katibu wa itikadi na uenezi,Nape Nnauye, Naibu Katibu Mkuu wa CCM bara, Mwigulu Nchemba pamoja na wajumbe mbalimbali wa sekretarieti mpya ya CCM ambapo wanataraji kuongoza mashambulizi ya kushambulia ngome ya Chadema.
Katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani Arusha, Isaac Kadogoo alisema mkutano huo utafanyika leo sambamba na kufungua matawi na maandamano makubwa ya kumpokea Kinana kuanzia uwanja mdogo wa ndege Kisongo hadi wilayani Arumeru na kisha kurejea katikati ya jiji la Arusha.
Kadogoo alisema kwamba lengo la shughuli hiyo ni kumkaribisha Kinana ambaye ni mkazi wa mkoani Arusha sanjari na kuelezea sera mbalimbali yakiwemo maendeleo yaliyoletwa na CCM mkoani Arusha na nchini kwa ujumla.
0 maoni:
Post a Comment