Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Zitto aitupia kombora CCM - Mshahara wa Rais uwe wazi

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amekirushia kombora Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema hakina nguvu tena ya kuendelea kutawala. Kabwe alikwenda mbali zaidi na kusema ili Tanzania iwe salama, ni lazima CCM ishindwe katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Zitto aliyasema hayo jana, katika mahojiano ya moja kwa moja baina yake na mtandao wa kijamii wa Jamii Forum (JF), ambapo alijibu maswali mbalimbali aliyoulizwa.

Kauli ya Zitto, ilikuja baada ya mmoja wa wachangiaji kutaka kujua mtazamo wake kuhusu hali ya vyama vya upinzani nchini na hatima ya CCM kuelekea 2015.

Akijibu swali hilo, Zitto alisema chama chake kina nafasi kubwa ya kushika dola na kueleza kuwa jambo muhimu ni kwa chama hicho kinachokua kwa kasi kujipanga vizuri.

“Ili Tanzania iwe salama, ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine wanaweza kukata tamaa.

“Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa. Njia pekee ya kuisaidia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kuondoka madarakani.

“CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola. Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.

Zitto aihofia CCM

“Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula fedha za walipa kodi, halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi.

Je, kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na limitation (ukomo) mfano, vyama vitatu tu?”, aliuliza mmoja wa wachangiaji katika mtandao huo.

Akijibu swali hilo, Zitto alisema haoni sababu ya kuundwa kwa sheria inayoweka ukomo wa idadi ya vyama vya siasa na kueleza kuwa utitiri wa vyama vya siasa ndiyo afya ya demokrasia.

“Tusiminye kabisa watu kuwa huru kuanzisha vyama vya siasa. Baada ya muda ni vyama vyenye uwezo wa kukonga nyoyo za wananchi ndivyo vitabakia. Wala hatuna haja ya kuweka sheria,” alisema.

Hata hivyo, Zitto alisema licha ya hivi sasa Tanzania kuwa na vyama vya siasa visivyopungua 20, lakini mbele ya safari haoni uhai wa vyama zaidi ya vinne.

Alivitaja vyama vikubwa vitakavyosalia kuwa ni CCM na CHADEMA, ingawa alionyesha hofu kuwapo na uwezekano wa kundi moja la CCM kujitenga na kuunda chama kingine chenye nguvu zaidi ya chama chake.

“Huko mbele ninaona Tanzania yenye vyama sio zaidi ya vinne. Vyama vikubwa viwili, CCM na CHADEMA. CUF watakuwa ‘balancing party’ kama ilivyo LibDems UK au Greens na Liberals Ujerumani.

Zitto ang’aka kuhusishwa na CCM

Katika mahojiano hayo, Zitto alikanusha kuwa na uhusiano na CCM, na kusema kuwa hiyo ni propaganda inayofanywa na watu wachache wenye nia ovu dhidi yake.

“Ukitaka kummaliza mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa Tanzania, mhusishe na ama usalama wa Taifa au CCM.

“Ndivyo ilivyokuwa kwa Mabere Marando miaka ya tisini. Marando ameishia kuweka sawa historia ingawa propaganda dhidi yake zilikuwa kali sana kiasi cha kuogopwa kweli kweli. Napita njia hiyo hiyo ya Marando na wanaonipaka matope haya wataona aibu sana ukweli utakapodhihiri.

“Siku za mwisho za uhai wake ndugu Chacha Wangwe naye aliambiwa ni CCM na kwa kweli alikufa akiwa na chuki sana kuhusu tuhuma hii.

“Faida kubwa niliyonayo mimi ni kwamba, mtaji wangu wa kisiasa ulikuwa ni mkubwa mno na ndiyo maana tuhuma hizi hazijaniathiri.

“Ninaamini tuhuma kama hizi zingekuwa kwa watu wengine, wangekuwa wameshafutika kwenye historia ya siasa.

“Sijawahi kuwa mwana CCM, familia yangu yote kabisa ni waanzilishi wa CHADEMA. Sina historia na CCM. Inawezekana wanaosema mimi ni CCM wengi wao wamewahi kuwa CCM, wana familia zao ndani ya CCM na wamewahi kula matunda ya CCM. Mimi sijawahi na wala sitawahi.

“Baadhi ya watu wanapandikiza chuki hizi kwa sababu zao wenyewe. Hawanisumbui maana najua ni kikundi kidogo cha watu wachache wenye malengo yao ovu. Wajue tu kwamba hawawezi kuwadanganya Watanzania ambao wanafanya maamuzi yao yasiyotokana na propaganda ila kutokana na matendo ya kila mmoja.

“Onyo: Watu hao hawawezi kummaliza Zitto kisiasa bila kuiathiri CHADEMA, maana the image of Zitto is so intimately intertwined with CHADEMA that you couldn’t attack Zitto without jeopardizing the image of Chadema, and vice versa,” alisema.

Alalamikia vyama kukosa itikadi

“Unalizungumziaje ombwe la itikadi miongoni mwa vyama vya siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa?” aliuliza mchangiaji.

“Hii ni changamoto kubwa sana kwa nchi yetu, itikadi za kisiasa husaidia kunyoosha sera za vyama. Hivi sasa chama chochote chaweza kuwa na sera yoyote ile kwa kuwa hakuna uti wa mgongo ambao ni itikadi.

“Lazima vyama vijipambanue kwa itikadi zao. Kwa kukosekana kwa itikadi zinazoeleweka vyama vimekuwa kama 'electoral machines' tu.

“Kukosekana kwa itikadi kunafanya vyama kudandia masuala. Mfano juzi hapa mmesikia Mkutano Mkuu wa CCM umeazimia elimu iwe bure. CHADEMA tulisema hivi mwaka 2010, CCM wakasema huo ni uwendawazimu, kwani haiwezekani.

Rais ajaye ni wa kizazi kipya

Zitto alirejea kauli yake kuutaka urais na kusema anaamini rais wa awamu ya tano atakuwa kijana.

“Mimi ninaamini kabisa kuwa rais ajaye wa Tanzania ni lazima atokane na kizazi cha baada ya uhuru. Nchi inahitaji a fresh start.

“Hebu tazama nchi hii, asilimia 70 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 29! Asilimia 65 ya wapiga kura wapo kati ya umri wa miaka 18 – 40. Hili ni Taifa la vijana.

“Nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17! Unaweza kusema hili ni Taifa la watoto. Hawa wazee wetu walipokuwa wanachukua nchi walikuwa vijana.

“Mwalimu Julius Nyerere alikuwa Waziri Mkuu akiwa na miaka 39, Mzee Rashid Kawawa alikuwa Waziri Mkuu akiwa na miaka 37. Waziri Mkuu wakati huo ndio alikuwa Mkuu wa Serikali, maana Mkuu wa nchi alikuwa Malkia wa Uingereza.

“Kuna watu lazima watafsiri chochote atakachosema Zitto. Hata hili ninaloandika hapa mtasikia, watasema tu. Kuna watu wanaumwa ugonjwa wa zittophobiasis ni lazima waseme.

Mshahara wa Rais uwe wazi

Baadhi ya wachangiaji walitaka kujua iwapo ipo haja ya kuendelea kufanya siri mishahara ya viongozi wa juu wa nchi, kama vile Rais wa Jamhuri, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais.

“Sijui mshahara wa Rais na naamini ni katika vitu ambavyo walipa kodi wanatakiwa kujua. Mshahara wa Rais hautakiwi kuwa siri kwa Mtanzania yeyote.

“Inapaswa kuwa wazi kabisa na kila raia ajue. TRA watakuwa wanajua kama sio tax exempt. Nadhani tukifuatilia kupitia Utumishi tunaweza kupata hizo data.”

Imenadikwa na gazeti  Mtanzania, 24 Novemba, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO