Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Dunia itegemee nini Uchaguzi wa Marekani leo?

MAMILIONI ya Wamarekani leo wanapiga kura kumchagua rais ambaye ataiongoza nchi hiyo kwa miaka minne ijayo baada ya Rais Baraka Obama wa Chama cha Democrat kumaliza kipindi chake. Rais ajaye ataapishwa Januari mwakani, hivyo rais aliyepo madarakani ataendelea kuongoza wakati wa kipindi hicho cha mpito.
   Kulingana na Katiba ya nchi hiyo, rais anaruhusiwa kugombea kiti cha urais kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja, hivyo Rais Obama ameteuliwa na chama chake hicho kugombea kiti hicho cha muhula wake wa pili akipambana vikali na Mitt Romney wa Chama cha Republican, ambaye ameteuliwa kugombea kwa mara ya kwanza kwa tiketi ya chama chake.
   Wagombea hao wawili wanapambana vikali kiasi kwamba kura za maoni zinaonyesha kwamba wamekabana koo, kwa maana kwamba hakuna anayeweza kuapa kwamba lazima ataibuka mshindi. Ni ushindani unaoonekana kuwa moja ya michuano mikali zaidi katika historia ya nchi hiyo tajiri sana na yenye nguvu za kijeshi kuliko nchi nyingine yoyote duniani.   Picha hii ni imechukuliwa mtandao wa BlackExcellenceX
Ni uchaguzi ambao kampeni zake huchukua muda mrefu na fedha nyingi kuliko chaguzi nyingine za urais duniani kote na ni uchaguzi ambao mchakato wake huonyesha kiwango kikubwa cha demokrasia iliyopevuka kutokana na uwazi, ushirikishi pamoja na mamlaka za uchaguzi kutoa haki pasipo kupendelea upande wowote.  Kama tulivyosema hapo juu, ni chaguzi zinazotumia fedha nyingi, ingawa michango na matumizi ya fedha hizo huratibiwa na mamlaka zilizowekwa kisheria na kikatiba.
     Kutokana na nguvu za Marekani kijeshi na kiuchumi, nchi hiyo hupewa nafasi kubwa na muhimu katika kuamua na kushawishi mwelekeo au maamuzi kuhusu masuala mengi duniani na katika vyombo na taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la Umoja huo, Umoja wa Kujihami (Nato) na jumuiya na taasisi nyingine, zikiwamo za Ulaya, Asia, Pacific, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
  Kwa maneno mengine, hakuna maamuzi yoyote makubwa yanayofanyika kimataifa na wakati mwingine katika nchi mojamoja pasipo nchi hiyo kuhusishwa na kutoa kauli ya mwisho. Huo ndiyo mfumo wa kibabe na kibeberu uliowekwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia na baadhi ya nchi washirika, zikiwamo Uingereza na Ufaransa. Ni mfumo ulioipa sauti na haki ya pekee katika IMF na Benki ya Dunia baada ya taasisi hizo kuasisiwa mjini Bretton Woods, Marekani mwaka 1945.
   Ndiyo maana kila uchaguzi unapofanyika nchini Marekani, dunia nzima hufuatilia uchaguzi huo kwa umakini mkubwa kwa sababu sera za Rais wa Marekani huathiri nchi nyingine kwa namna moja ama nyingine. Hivyo ndivyo ilivyo kwa uchaguzi wa leo kwa sababu wagombea wawili hao wana sera tofauti kuhusu masuala ya  ndani na nje ya nchi, hivyo mataifa mengi yako roho juu yakisubiri matokeo. Kura za maoni zilizofanyika katika nchi nyingi za mabara ya Afrika, Ulaya, Asia, Pacific, Amerika ya Kusini na nchini Canada zinaonyesha kwamba zingependa Rais Obama aibuke mshindi katika uchaguzi wa leo.
   Hata hivyo, mshindi atatakiwa awe na kura za majimbo (Electoral College votes) zisizopungua 270 kati ya 538. Kura hizo hazitokani na kura zitakazopigwa leo, isipokuwa kila jimbo limetengewa kura kutokana na wingi wa wawakilishi wake bungeni. Kwa mfano, Jimbo la California lina kura 55 wakati New Hampshire lina kura 4 na mshindi anakumba kura zote za jimbo.
   Hivyo, kupata kura nyingi zitakazopigwa leo hakumuhakikishii mgombea kuwa Rais.  Hata hivyo, sisi tunawatakia wagombea wote kila la kheri, ingawa tunadhani kwamba ushindi wa Rais Baraka Obama utakuwa wa manufaa zaidi kwa Tanzania, Afrika na dunia kwa jumla.
Kutokana na nguvu za Marekani kijeshi na kiuchumi, nchi hiyo hupewa nafasi kubwa na muhimu katika kuamua na kushawishi mwelekeo au maamuzi kuhusu masuala mengi duniani na katika vyombo na taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la Umoja huo, Umoja wa Kujihami (Nato) na jumuiya na taasisi nyingine, zikiwamo za Ulaya, Asia, Pacific, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Source: Mwananchi
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO