KAMATI ya nishati na madini, Jumanne November 20, 2012 itakuwa jijini Arusha kukusanya maoni kutoka kwa wadau (wananchi) wa sekata hiyo katika mkutano utakao fanyanyika katika viwanja vya Youth League CCM Mkoa.
Lengo la kamati hiyo ni Kukusanya maoni ili tusifanye makosa, Ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye kutunga sera.
Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa utaratibu bora wa kusimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi nchini. Kuakikisha kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora ili Taifa letu lipate mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na mapato hayo yatumike vizuri kama msingi wa kujenga uchumi endelevu wa kisasa, utakaonufaisha wananchi wengi zaidi, hivyo watanzania wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi kesho kuanzia saa nane mchana mpaka saa kumi hili kujadili na kutoa maoni ya rasimu ya awali ya sera mpya ya gesi nchini.
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini Tanzania katika maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari ambapo mpaka sasa jumla ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi ya utafutaji inaendelea na upo uwezekano wa ugunduzi zaidi.
Kiasi hicho kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi ya wazalishaji gesi wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo gesi asilia iliyothibitika nyingi zaidi kuliko sisi.
Lakini kiasi cha gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu kinatosha kutuwezesha kuwa wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na tukijipanga vizuri na kuisimamia kwa umakini sekta hii ndogo, inaweza kutusaidia kuharakisha maendeleo.
Kinyume chake, tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama nchi, tusipate faida kubwa. Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo uvumbuzi wa gesi na mafuta umevuruga uchumi wao.
Hivyo, kabla hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye kutunga sera, kuandaa mkakati na kutunga sheria itakayosimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi.
Sisi tunaoanza leo tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na tuna fursa ya kuchukua uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima tuchukue hatua sasa. Tukichelewa itakuwa vigumu kurekebisha makosa baadaye.
Pamoja na hayo ni muhimu wananchi waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja. Hatutarajii mapato katika miaka michache ijayo. Isitoshe lazima tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai leo ni wadhamini wa kile ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo itabidi tufikiri vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata kitumike leo na kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi vijavyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo itakwisha.
Kwa pamoja tuhakikishe Tanzania inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi ya rasilimali hii kwa faida na maendeleo yetu na vizazi vijavyo.
Source: HAKI MADINI.ORG
0 maoni:
Post a Comment