Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

ABSALOM KIBANDA APELEKWA NJE YA NCHI KWA MATIBABU YAKE

Wauguzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI) Hospitali ya Taifa Muhimbili wakimpeleka kwenye gari la wagonjwa. Wanaoshudia ni marafiki na wanahabari wenzake .Akiwepo mkurugenzi wa makampuni ya IPP media Bw. Reginald Mengi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda amesafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Kibanda, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Limited, alisafirishwabaada ya kuvamiwa na majambazi na kushambuliwa nyumbani kwake saa 6.15 usiku wa kuamkia jana, maeneo ya Goba Kunguru, Mbezi Juu, Kata ya Kawe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TEF ikiwa imesainiwa na Katibu wake, Neville Meena, Mwenyekiti huyo alivamiwa na watu wasiofahamika wakati akiingia nyumbani kwake.

Ilisema akiwa kwenye lango, ghafla walitokea watu watatu ambao walivunja kioo cha gari upande alikoketi, na kumvutia nje na kutekeleza walichokusudia.


Kibanda alijeruhiwa kichwani ambako alipigwa na kitu ambacho  yeye alisema ni nondo huku jicho la kushoto likiathirika (inadhaniwa kwamba lilichomwa na kitu chenye ncha kali), kucha ya kidole cha mkono wa kulia iling’olewa sambamba na meno mawili.

“Baada ya watesaji hao kuondoka, alipata msaada kutoka kwa familia na majirani zake ambao walimkimbiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa hadi leo (jana) asubuhi alipohamishiwa Taasisi ya Mifupa ya Hosipitali hiyo (MoI) kuendelea na matibabu,” ilisema taarifa.

TEF inakiona kitendo hicho kama uthibitisho kwamba mazingira ya kazi ya waandishi wa habari nchini si salama sana, na kama tasnia “tunapaswa kuchukua hatua za kutathmini upya mazingira ya kazi zetu, ili kuhakikisha tunakuwa salama.”

Ilisema mwendelezo wa vitendo vya kushambulia waandishi wa habari ambavyo katika siku za karibuni vimeibuka, vinalifanya Jukwaa liamini kwamba wanahabari sasa wanatishwa ili wasitekeleze majukumu yao ipasavyo.

Hivyo TEF inaamini kwamba  vyombo vya Dola, vitachunguza, kuwatia mbaroni kisha kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa tukio hili na mengine kadhaa ambayo sasa yamegeuka kuwa sehemu ya utamaduni nchini.

Hata hivyo, TEF ilitoa mwito kwa wanahabari nchini, kuendelea kufanya kazi zao bila woga, lakini wakichukua hadhari kutokana na mazingira yanayojitokeza sasa.

Polisi kwa upande wake imeunda jopo la maofisa wanne waandamizi waliobobea katika upelelezi ili kushirikiana na wapelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na askari wa mkoa wa Kinondoni kuchunguza tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Suleiman Kova, alisema:  “Kutokana na unyeti wa suala hili, uchunguzi wa makini unafanyika na hivyo makao makuu ya Polisi yameongeza maofisa wanne waandamizi waliobobea katika upelelezi na sisi kanda maalumu tumetoa watano na Kinondoni nao watatoa maofisa wake, ili kuchunguza suala hili.”

Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda alisema  Kibanda alivamiwa na watu wasiofahamika na kumjeruhi kichwani, usoni kwenye jicho la kushoto, kidole cha pete (chanda) mkono wa kulia
na michubuko miguuni. 

“Taarifa za awali zinaonesha kuwa tukio hili lilitokea wakati anarudi nyumbani kwake eneo la Goba Kunguru maarufu kama Kwa Pepsi… alipofika katika nyumba hiyo alipiga honi ili afunguliwe akiwa katika gari namba T653 AZR aina ya NISSAN X-TRAIL,” alisema.

Alisema kabla mlinzi, Baka Ibrahim, hajafungua lango kuu alisikia sauti ya Kibanda akiomba msaada na hivyo akabaini kuna hatari na kuomba msaada kwa majirani ndani ya uzio huo wenye nyumba sita, ambapo majirani wawili walijitokeza pamoja na familia ya Kibanda na wakatoka nje ya lango kuu ili kutoa msaada.

“Walipofungua mlango walikuta gari la mlalamikaji likiwa peke yake na mlango wa mbele kushoto ukiwa wazi, vioo vya madirisha ya mlango wa dereva na abiria vikiwa vimevunjwa,” alisema.

Kova alisema katika ufuatiliaji walisikia sauti ya mtu meta 30 kutoka kwenye gari akiomba msaada na walipofika eneo hilo walimtambua kuwa ni Kibanda na walipomkagua walibaini majeraha yakitoka damu.

“Majeruhi alipelekwa haraka hospitali kwa msaada wa majirani zake sambamba na taarifa kupelekwa kituo cha Polisi Kawe, na polisi wa kituo hicho walishirikiana nao kumpeleka Muhimbili,” alisema Kova.

Kamanda Kova alisema baada ya taarifa hizo, viongozi waandamizi wa  Polisi pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani walifika hospitalini hapo kwa ufuatiliaji na upelelezi wa shauri hilo ulianza usiku huo huo na ikagundulika kwamba ndani ya gari hakuna kilichoibwa.

Akizungumza na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alipofika kumjulia hali, Kibanda alisema tukio hilo lilitokea nje ya lango lake wakati akirejea nyumbani ambapo aliona kundi la watu mbele ya gari na kumvamia huku wakivunja kioo wakimtaka ashuke.

Kibanda alisema alihamia upande wa pili wa gari ili kujiokoa lakini walimshusha na kumshambulia kwa kipigo.

“Nilihamia mlango wa upande wa pili wa gari langu kwa lengo la kujiokoa lakini walinikamata wakanitoa nje na kunishambulia… wamenipiga na nondo kichwani, wamenishambulia usoni, mkononi, wameninyofoa kidole na kunitoboa jicho na baadaye nilisikia wakiambiana ‘mshambulie kwa risasi’ na kusikia ikikokiwa lakini risasi haikutoka,” alisema Kibanda.

Akizungumzia tukio hilo, Dk Mwinyi alisema ni la kusikitisha sana “lakini amefika katika mikono salama na kuhudumiwa vizuri.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Limited, Hussein Bashe alisema  akimkariri Kibanda, kwamba alivamiwa na watu watatu, mmoja akiwa na bunduki, wawili nondo na wakati wakimpiga walikuwa wakiwasiliana wao kwa wao wakisema ‘piga piga, tumpige risasi huku mwingine akikataza.”

Bashe alishukuru madaktari  wa Muhimbili,  kwa ushirikiano waliouonesha kwani tangu alipofikishwa hapo usiku huo walimhudumia kwa hali ya juu.

Hati ya kusafiria ya Kibanda ilikuwa imezuiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na kesi inayomkabili ya uchochezi ambapo jana ilikuwa ikisikilizwa. Alipewa ili kumwezesha kusafirishwa nje ya nchi.

Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Nchimbi katika taarifa yake, alisema Serikali imelaani kitendo hicho cha uhalifu na kuahidi uchunguzi wa kina kufanyika na hatua kuchukuliwa.

Pia aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuacha uchunguzi ufanyike, ila watoe ushirikiano wa kuwezesha wahalifu hao kukamatwa.

Picha na maelezo: Father Kidevu Blog

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO