MAOMBI yaliyowasilishwa na jopo la mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kufuta na kumfungulia kesi nyingine mteja wao yatasikilizwa na Jaji Laurence Kaduri.
Jaji Kaduri wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alipangwa kusikiliza maombi hayo jana. Majalada mawili ya kesi ya kujihusisha na ugaidi inayomkabili Lwakatare na Ludovick Joseph yalifikishwa mahakamani hapo Jumanne.
Majalada hayo yalipelekwa Mahakama Kuu kutokana na maombi yaliyowasilishwa na jopo la mawakili wa Lwakatare ambao wanaiomba mahakama hiyo kuyafanyia marejeo au kuchunguza ili kujiridhisha usahihi na uhalali wa mwenendo wa kesi katika jalada namba 37 na namba 6 ya mwaka huu.
Wanaomba mahakama hiyo kutengua hati ya DPP iliyofuta mashtaka dhidi ya washtakiwa hao kabla ya kuwafungulia mashtaka mengine kama hayo.
Jopo hilo linaomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa uamuzi wa maombi ya dhamana uliokuwa umepangwa kutolewa na Hakimu Mkazi Emilius Mchauru Machi 20 mwaka huu katika kesi namba 37 iliyofutwa.
“Tunaomba mahakama ifanye marejeo na kutengua mwenendo wa kesi mpya namba 6/2013 iliyofunguliwa baada ya kesi namba 37 kufutwa badala yake tunaomba jalada lililofutwa liendelee.
“Tunaomba mahakama iamue kwamba utaratibu wa DPP kufuta mashtaka ulikuwa kinyume cha sheria na haukuwa sahihi au itoe nafuu nyinginezo kadri inavyoona inafaa,”ilisema hati hiyo ya maombi.
Washtakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Kisutu Machi 18 mwaka huu na Machi 20 mwaka huu waliachiwa kabla ya kukamatwa tena na kusomewa upya mashtaka ya kujihusisha na ugaidi.
Lwakatare na mwenzake waliachiwa mbele ya Hakimu Mchauru baada ya kukubaliana na maombi yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri ambao uliwasilisha hati kutoka kwa DPP ikionyesha a haikuwa na haja ya kuendelea na kesi hiyo.
“Mheshimiwa DPP amewasilisha nole prosequi chini ya kifungu cha sheria namba 98(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai akionyesha kwamba Jamhuri haina haja ya kuendelea na mashtaka hayo, tunaomba yafutwe,”alidai Wakili Mkuu wa Serikali, Prudence Rweyongeza.
Washitakiwa walisomewa mashtaka upya na Wakili Rweyongeza mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana.
Alidai washitakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwamo ya kula njama ya kumdhuru kwa sumu na kumteka Denis Msaki, Desemba 28 mwaka jana maeneo ya Stop Over Kimara.
“Shtaka la kwanza kwa ajili ya washitakiwa wote wawili ni kwamba wanadaiwa Desemba 28 maeneo ya King’ong’o Kimara Stop Over walikula njama ya kutenda kosa la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Denis Msaki.
“Shtaka la pili kwa washitakiwa wote limefunguliwa chini ya kifungu cha sheria namba 24 (2) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002. Washitakiwa wanadaiwa walikula njama ya kumteka Denis Msaki kinyume cha sheria namba 4(2) aya (C) (iii) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
“Mheshimiwa shtaka la tatu linawakabili washitakiwa wote ambao pia wanadaiwa kinyume cha kifungu namba 5(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, kwa pamoja walifanya mkutano wa kufanya vitendo vya kigaidi, walipanga, walishiriki mkutano huo wenye lengo la kupanga kitendo cha ugaidi kwa kumteka nyara Denis Msaki.
“Shtaka la nne la kuhamasisha vitendo vya ugaidi, linamkabili mshitakiwa wa kwanza. Lwakatare, anadaiwa Desemba 28 mwaka jana, akiwa mmiliki wa nyumba aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi,” alidai Rweyongeza.
Hakimu Katemana hakuruhusu washtakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa vile kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu. Aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Jopo la mawakili wanaomtetea Lwakatare ni Tundu Lissu, Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Mabere Marando wakati mshitakiwa Ludovick hana wakili wa kumtetea.
Mtanzania
0 maoni:
Post a Comment