Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Taifa Stars raha tupu, yaidungua Morocco 3.-1 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam

 

WASHAMBULIAJI wa kimataifa wanaokipiga klabu ya TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu jana wamekiongoza kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kuifanyia maangamizi Morocco ‘Simba wa Atlas’ baada ya kuichapa mabao 3-1.

Katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, ilipigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.

Licha ya kosa kosa za hapa na pale, hadi mwamuzi Helder Martins kutoka Angola akipuliza filimbi kuashiria mapumziko, hakuna kamba iliyokuwa imetikiswa.

Kipindi cha pili, Stars yenye udhamini mnono wa Kilimanjaro Premium Lager, iliingia kwa kasi na mtokea benchi, Ulimwengu aliyechukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto alitikisa nyavu dakika ya 46 akimalizia mpira wa kurusha wa Erasto Nyoni.

Dakika ya 48 Samata alishindwa kuitendea haki pasi ya Ulimwengu, ambako shuti lake lilitoka nje ya goli kabla Morocco kujibu shambulizi ambako krosi ya Abourazouk ilitoka nje kidogo ya lango la Stars.

Samata dakika ya 67 alirekebisha makosa baada ya Athumani Idd ‘Chuji’ aliyeingia kuchukua nafasi ya Mrisho Ngasa kupiga pande refu na kumkuta mshambuliaji huyo aliyewaacha mabeki wa Morocco kabla ya kuutumbukiza kambani na kuamsha hoi hoi na shangwe kwa mashabiki.

Nusura Amri Kiemba ambaye alitandaza soka maridadi aipe Stars bao la tatu, dakika ya 76 baada ya kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa kabla ya mabeki kuokoa.

Kama haitoshi, Samata alirudi kambani tena dakika ya 79 baada ya kuunganisha vema krosi ya Ulimwengu aliyemuacha beki Eladoua Chin na kuandika bao la tatu. Baada ya bao hilo, Belakhdar alilimwa kadi nyekundu kwa kuzozana na mwamuzi.

Dakika ya 90, Stars ilimtoa Samata na nafasi yake kuchukuliwa na John Boko, na sekunde chache baadaye Morocco wakapata bao la kufutia machozi likifungwa na Abourazouk.

Kwa ushindi huo, Stars ambayo iko kundi moja na Ivory Coast, Gambia na Morocco imefikisha pointi sita, ikiwa nyuma ya vinara Ivory Coast yenye pointi saba.

Baada ya mpira kumalizika, mashabiki waliotanda uwanjani walikuwa wakiimba kwa furaha, huku wengine nje ya uwanja wakilizunguka basi la Stars.

Nje mashabiki walijipanga msururu huku na huku na kuacha njia katikati ya kupita wachezaji huku wakipeana mikono.

Wachezaji Sure Boy, Samata, Kaseja na Ulimwengu walishangiliwa sana na mashabiki hao kutokana na soka walilotandaza dimbani.

Taifa Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Sureboy, Mbwana Samatta, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto.

Morocco: Lamyaghri Nadr, Bellakhadar Youngbs, Hafid Abdelilah, Bergdich Zakarya, Achchakir Abderrahm, Hamma Younes, Barada Abdelaziz, Eladova Issam, Chafn Kamal, Belghazouani Chahr, Abourazouk Hamza.

Stori na Tanzania Daima, Kwa Picha Zaidi Kong’oli Hapa

Kikosi cha Taifa Stars.

Kikosi cha Morocco.

Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars),Thomas Ulimwengu akiwatoka Golikipa na Beki wa Timu ya Taifa ya Morocco wakati wa Mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza Kombe ya Dunia Mwaka 2014 kule nchini Brazil,uliochezwa jioni hii kwenye uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam.Taifa Stars imeshinda Bao 3 - 1,mabao mawili yaliyotiwa kimiani na Mshambuliaji Machachari,Mbwana Samatha huku moja likifungwa na Thomas Ulimwengu.

Beki wa Timu ya Morocco akiruka juu kuondosha hatari iliyokuwa ikielekeza langoni mwake.

Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars),Thomas Ulimwengu akiwatoka mabeki wa Timu ya Taifa ya Morocco wakati wa Mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza Kombe ya Dunia Mwaka 2014 kule nchini Brazil,uliochezwa jioni hii kwenye uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam.

Hatari langoni mwa timu ya Morocco.............

Kiungo Mshambuliaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars),Shomari Kapombe akichuana vikali na Beki wa timu ya Morocco wakati wa Mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza Kombe ya Dunia Mwaka 2014 kule nchini Brazil,uliochezwa jioni hii kwenye uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam.

Lango la timu ya Morocco ilikuwa ni hatari muda wote wa mchezo.

Kipa wa Timu ya Morocco akiusindikiza kwa Macho mpira ulioingia wavuni,baada ta kuigwa na Mchezaji Mbwana Samatta wa Taifa Stars.

Mbwana Samatta akishangilia goli lake.

Mbwana Samatta akiondoka na mpira huku mabeki wa Morocco wakimfukuzia.

Mrisho Ngassa wa Taifa Stars (kushoto) akijiandaa kumtoka beki wa Morocco,Achchakir Abderrahim.

Kapombe akimpiga chenga safi Beki wa Morocco.

Mashabiki wa Taifa Stars wakiendelea kufurahia ushindi wa timu yao.

Wachezaji wa Taifa Stars wakimpongeza mwenzao Thomas Ulimwengu baada ya kufunga bao la kwanza.

Shangwe tupu uwanja wa Taifa.

Ulinzi wa nguvu uwanja wa Taifa.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO