Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Utata wa kifo kigogo UVCCM Arusha

Benson Mollel (kwanza kulia, enzi za uhai wake) akiwa katika moja ya shughuli za UVCCM mkoani Arusha. Picha ya makataba kwa hisani ya Issa Michuzi 

Na Moses Mashalla, Arusha 

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business,  iliyopo Mtaa wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel alikutwa akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.

Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi wakati wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.

Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa mmoja wa vinara wake.

Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza  tukio hili ambalo ni la ghafla.”

Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel japokuwa sifahamu nini hasa kimejiri huko."

"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote watutaarifu," alisema Shigela.

Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.

Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga.  Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.

Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.

Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na kuchukua chumba namba 208.

Mmoja wa walinzi hotelini hapo aliyetembulika kwa jina la Obeid Mollel kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Victoria Support Services, alisimulia kuwa marehemu aliingia na mwanamke huyo na kisha kuondoka ghafla kabla ya kurejea tena wakiwa wote usiku.

Alisema kuwa wakati wakiwa hotelini hapo marehemu aliomba kuegesha gari lake jipya aina ya Mark II Grande ambalo halijasajiliwa na kwamba alipokubaliwa alifanya hivyo kisha akaenda chumbani. Ilibainika kuwa mwanamke huyo aliondoka jana asubuhi.

Taarifa zaidi

Mmoja wa wahudumu hotelini hapo (jina lake limehifadhiwa), alisema kuwa mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mariam aliwasili hotelini hapo saa 5.00 asubuhi na kuomba kupelekwa moja kwa moja chumba alichokuwapo marehemu.

Mhudumu huyo alisema wakati mwanamke huyo akiomba kupelekwa chumbani, marehemu naye alipiga simu mapokezi akiomba mwanamke huyo apelekwe chumbani kwake, agizo ambalo walilitekeleza.

Kwa mujibu wa mhudumu, baadaye kama saa 6.00 mchana walimwona mwanamke huyo akitoka nje ya hoteli hiyo na kuondoka.

Alisema kwamba baadaye waliamua kupiga simu ya chumba alichofia marehemu ili kujua endapo ataendelea kupanga kwani muda wa kawaida ulikuwa umemalizika lakini simu hiyo ilikuwa ikiita bila majibu.

Mmoja wa wahudumu ambaye alikuwa akifahamiana na marehemu, aliamua kumpigia kupitia simu yake ya mkononi lakini nayo haikupokewa.

Mhudumu huyo aliamua kupanda ngazi kwenda chumbani kwa marehemu na katika hali isiyo ya kawaida alikuta mlango ukiwa wazi na marehemu akiwa amelala.

"Nilijaribu kumwamsha, lakini hakuamka na ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi wa hoteli na baadaye waliviarifu vyombo vya usalama.

Chanzo cha kifo hiki kinakanganya maana kama kweli ni mauaji basi yamefanyika kwa ustadi mkubwa,” alisema mhudumu huyo na kuongeza:

“Unajua vyumba vyote vya huko juu ghorofani ukifunga mlango tu huku chini sisi mapokezi tunasikia, sasa cha ajabu mlango tumeukuta wazi. Hapa kuna maswali mengi," alieleza mhudumu huyo.

Source: Mwananchi, Jumapili,Marchi3  2013 

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO