Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA yasitisha maandamano yake • Ni baada ya Mbowe kuteta na IGP Mwema

HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekubali kusitisha maandamano yake yaliyokuwa yafanyike leo katika majiji manne ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza, kuwashinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo kuachia ngazi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema akiwa pamoja na Kamishina wa Oparesheni (CP) Paul Chagonja, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova na maofisa wengine kukutana na viongozi wa CHADEMA chini ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe.

CHADEMA iliwapa viongozi hao wiki mbili tangu Februari 18 mwaka huu, kuachia ngazi kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya vinginevyo wangefanya maandamano makubwa leo kuwashinikiza wang’oke.

Hata hivyo, juzi serikali ilitangaza kuyasitisha maandamano hayo ikidai inatoa nafasi kwa wananchi waweze kumpokea Rais wa China, Xi Jinping ambaye alianza ziara ya siku mbili nchini, jambo ambalo CHADEMA walilipinga na kusisitiza kuandamana.

Jana viongozi hao wa polisi na siasa walilazimika kukutana na kuzungumza kwa kirefu na Mbowe hatimaye kufikia muafaka kwa CHADEMA kukubali kusogeza maandamano yao hadi hapo baadaye.

Sababu nyingine iliyokataliwa na CHADEMA ni ile ya kwamba Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda inayochunguza kiini cha matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012 inaendelea na kazi yake, wakidai kuwa tume hiyo haishughulikii suala la Waziri wa Elimu na naibu wake kujiuzulu.

Katika mazungumzo hayo, Mbowe aliongozana na Katibu wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), Deogratius Munishi na Ofisa habari wa chama, Tumaini Makene ambapo walikubaliana na jeshi hilo kusitisha maandamano hayo ili kutoa nafasi ya wananchi kushiriki kwa amani na utulivu katika mapokezi ya Rais wa China.

“Mbowe na IGP Mwema wamekubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya siku 14 ili kuona utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana na kushirikiana pasipo migongano kwa pande zote mbili.

Februari 18, mwaka huu, akiwa mjini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika viwanja vya Furahisha, Mbowe alisema Kawambwa na Mulugo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne.

Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

Katika matokeo hayo, Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.

Katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la pili 6,453, la tatu 15,426, la nne 103,327 na daraja sifuri 240,903.

Chanzo: Tanzania Daima, picha na Maktaba

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO