Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Wakili Nyange Mawalla aliacha wosia wa kisheria ulioelekeza azikwe Kenya

MGOGORO wa maziko ya Wakili Nyaga Mawalla, umeingia katika sura mpya, baada ya wakili wake, Fatuma Karume, kutoa wosia wake ambao ameelekeza azikwe Kenya.

Akizungumza jana jijini Arusha, wakili mwenzake , Albert Msando, alisema Fatuma, ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Karume, ndiye aliyeachiwa wosia huo.

Akifafanua kuhusu wosia huo, Msando alisema Nyaga alielekeza katika wosia huo maeneo mawili ya kuzikwa, kulingana na mazingira ya kifo chake.

Kwanza alielekeza kwamba siku akifia Tanzania, azikwe katika shamba lake kubwa la kisasa, lenye mandhari ya hali ya juu, lililopo Momela wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Pili kwa mujibu wa wakili Msando, aliyeongozana na Wakili Joseph Naiamanya, Nyaga alielekeza katika wosia huo wa kisheria, kwamba akifa nje ya nchi, maziko yake yafanyike katika nchi hiyo hiyo.

Msando ambaye ni Wakili, aliendelea kusema kuwa kwa sasa ndugu jamaa na marafiki, wako katika vikao vyakawaida na sio vya mvutano, ili kuangalia na kujadili mahali pa maziko na  hakuna mvutano kama unavyotafsiriwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Msando, kwa sasa mwili wa marehemu Nyaga, bado uko katika Hospitali ya Nairobi na uchunguzi wa polisi wa nchini Kenya, bado haujakamilika ndio maana mwili huo umechelewa kutolewa majibu ya kiini cha kifo chake.

Utata wa kisheria Kwa mujibu wa wanasheria, ikiwa Nyaga atarejeshwa nchini na ikatokea mtu yeyote kwenda mahakamani kuhoji, Mahakama italazimisha mwili huo urejeshwe Kenya kwa maziko.

Mwanasheria mwingine alisema kwamba wosia wa marehemu ulisajiliwa kwa wakili ni matamshi ya mwisho yaliyojikamilisha ambayo hayawezi kukiukwa kisheria. Wanasheria waliozungumza na gazeti hili, wamebainisha kuwa akirejeshwa nchini na Mahakama ikiamuru arudishwe Kenya kuzikwa, kutailazimu familia kufuata utaratibu wa itifaki ya Kenya na hivyo kuamsha mgogoro mwingine wa kidiplomasia.

Wazee waeleweshwa Kutokana na mgogoro huo, taarifa zilizolifikia gazeti hili zimesema kuwa viongozi wa dini na mila, wametumwa kwa wazazi wake, ili walegeze kamba na kukubali maziko ya mtoto wao yazingatie wosia wake.

Vyanzo vya habari kutoka karibu na familia hiyo, vinasema kuwa mdogo wa marehemu, Wilfred Mawalla ametuma viongozi wa dini wakiwemo wachungaji, mapadri na wazee wa mila ya kichaga, kwenda kwa wazazi wake.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao wametakiwa kwenda Marangu kuwaomba wazazi wakubaliane na wosia wa mtoto wao aliouacha akiwa hai.

Tayari mama yake mzazi ambaye jina lake halijapatikana, alishasisitiza kwamba, angependa mwanawe kipenzi azikwe nyumbani kwao Marangu Moshi, na sio mahali pengine popote. hatohudhuria mazishi ya mwanawe, iwapo atazikwa eneo tofauti na Marangu.

Mtoa habari wetu alieleza kwamba kutokana mvutano huo, Wilfred ndipo alipoamua kuwatumia viongozi na dini na mila kwenda kijijini Marangu, kwa lengo la kumlainisha mzazi huyo abadili msimamo wa kutaka maziko yafanyike Marangu.

“Hapa ni kizungumkuti, wazazi wanasema wao ndio wenye kauli ya mwisho ya kuamua na sio wosia ulioachwa, na Wilfred anasema lazima tuheshimu wosia uliachwa na marehemu na ndio maana wametumwa viongozi wa dini na mila kwenda kuwalainisha wazazi wote,” alisema mtoa habari.

Chanzo: Habari Leo

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO