Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Orodha ya Watanzania Wanaowindwa Kudhuriwa

 

*Orodha yao yafikia wanne, nyendo zao zafuatiliwa
*Dk. Bana, Lwaitama, Bashiru wazungumza

 

 

WAKATI hali ikiwa bado tete nchini kutokana na tishio la uwepo wa kundi la watu ambalo halijafahamika, linalotekeleza vitendo vya utekaji na utesaji raia kinyama, orodha ya baadhi ya majina ya Watanzania wanaowindwa imefahamika.

Uchunguzi wa kina wa MTANZANIA Jumapili umeonyesha kuwapo kwa kundi la watu wasiofahamika ambalo limekuwa likifuatilia nyendo za Watanzania wanne kwa ukaribu na hata kuiba baadhi ya vifaa vyao vya kazi katika mazingira ya kutatanisha, vinavyoaminika kuwa na nyaraka au kumbukumbu muhimu.

 

 

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, watu ambao wamekuwa wakifuatiliwa nyendo zao ni Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari Ltd (2006) na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana, Hussein Bashe, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msaki na viongozi kadhaa wa dini.

Uchunguzi umeonyesha kuwa Zitto, mwanasiasa kijana ambaye misimamo yake ya kisiasa inadaiwa kuwakwaza baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya Chadema na hata nje ya chama hicho, amekuwa akiishi maisha ya wasiwasi na wakati mwingine ameshindwa kushiriki kikamilifu shughuli mbalimbali za chama chake na zisizo za chama kutokana na hofu ya kuuawa.

Ingawa hakuna rekodi yoyote ya shambulio la kumdhuru lililokwishaelekezwa dhidi yake, taarifa zilizokusanywa na Mtanzania Jumapili zimeonyesha kuwa Zitto, mara kadhaa amekuwa akizuiwa na watu wake wa karibu kuhudhuria baadhi ya shughuli za kisiasa na hasa zinazohusu siasa za majukwaani, kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazoonyesha mipango ya kumdhuru.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vilivyo karibu na Zitto vilivyofikiwa na gazeti hili wakati wa uchunguzi, vimeeleza kuwa Zitto amekuwa katika hatari ya kudhuriwa na watu wasiojulikana tangu alipoonyesha mwelekeo wa kuwania urais 2015.

Jambo hilo limeibua joto la kisiasa ndani na nje ya chama chake, hususani kwa wale ambao wana nia ya kuwania wadhifa huo, baada ya Rais Jakaya Kikwete kung’atuka.

Zitto mwenyewe amepata kukaririwa zaidi ya mara moja akieleza kuwa anao maadui ndani na nje ya Chadema na kauli ambayo amekuwa akiisisitiza ni ile ya kuwepo kwa kundi maalumu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambalo halifurahishwi na mwenendo wake wa kisiasa, lililoamua kumshughulikia.

Na hata ndani ya Chadema, Zitto amekuwa na uhusiano wenye shaka na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Willbrod Slaa, wanaodaiwa kutofurahishwa na staili ya maisha yake ya kisiasa na hasa ushabiki wake wa siasa za kileo zinazosimamia misingi ya kweli ya kidemokrasia.

Wa pili katika orodha hii ni Kibanda, ambaye hivi karibuni alivamiwa na kundi la watu wasiofahamika, wakamshambulia na kumjeruhi vibaya na hivyo kulazimu kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Kibanda, mwandishi wa habari kitaaluma, ambaye amejijengea jina kubwa kutokana na uwezo wake wa kiuandishi, anatajwa kuwa mmoja wa waandishi ambao kalamu zao zimekuwa na athari mbaya kwa baadhi ya wanasiasa anaotofautiana nao kimsimamo na kimtizamo.

Watu walio karibu na Kibanda wanaeleza kuwa ingawa ni mmoja wa waandishi wa habari wachache mwenye uhusiano wa kirafiki na watu wengi, hilo halikumuondoa kwenye hatari ya kuwindwa, baada ya kuweka wazi msimamo wake wa kumuunga mkono mmoja wa wanasiasa wa CCM anayetajwa kuwa ana nia ya kuwania urais mwaka 2015.

Wadadisi wa wafuatiliaji wa mambo ya siasa wa hapa nyumbani wanaeleza kuwa Kibanda amekuwa akiangaliwa kwa jicho baya na baadhi ya wapinzani wa kisiasa wa mwanasiasa huyo ambao wanaamini kuwa ushawishi mkubwa alionao ndani ya wanahabari na nafasi yake ya Uenyekiti wa Jukwaa la Wahariri ni silaha ya kuwaangamiza 2015.

Kibanda amekuwa akiwindwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa akiwa bado anaishi eneo la Ubungo Kibangu, aliibiwa simu yake ya mkononi na kompyuta dogo ‘laptop.’

Mapema mwaka huu, watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwake majira ya usiku wakiwa na nia ya kuiba baadhi ya nyaraka zilizokuwa ndani ya gari lake, lakini kabla hawajatekeleza lengo lao, gari hilo lilianza kupiga king’ora, jambo lililosababisha watu hao wakimbie.

Aidha, Kibanda akiwa Hospitalini nchini Afrika Kusini chini ya uangalizi maalumu, watu wasiofahamika wamekuwa wakijitahidi kumfikia katika chumba alicholazwa pasipo mafanikio.

Habari kutoka Hospitali ya Mill Park alikolazwa zimeeleza kuwa siku chache baada ya Kibanda kulazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi ambako madaktari walielekeza abaki katika uangalizi wao pekee, watu watatu walifika hospitalini hapo na kujitambulisha kuwa wanatoka ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini na kutaka kumuona.

Mmoja wa watu waliosafiri na Kibanda nchini Afrika Kusini kwenda kusaidia kumuuguza ameeleza kuwa alitaarifiwa na uongozi wa hospitali hiyo kuwa kuna maofisa wa ubalozi waliokuwa wakitaka kumuona ili kumjulia hali, lakini wamezuiliwa hadi atakapofika na kuwatambua, lakini katika hali ya kushangaza, watu hao walipotea eneo hilo baada ya kuambiwa kuwa yeye alikuwa njiani kwenda kuwatambua.

Alisema, baada ya tukio hilo, alipokea simu nyingine kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni ndugu wa Kibanda, aliyetokea Tanzania kwa lengo la kwenda kumjulia hali, huku akitaka amuelekeze wodi aliyolazwa, lakini alipomtaka amsubiri ili waonane kwanza, alikata simu na hata alipompigia tena, simu yake ikawa haipatikani.

Ni kutokana na mwenendo huo wenye kutia mashaka, Kibanda alilazimika kuwekewa ulinzi maalumu katika wodi aliyolazwa.

Mwanasiasa kijana, Hussein Bashe, ambaye ni kada wa CCM, naye yumo katika orodha ya watu wanaowindwa kwa sasa na kundi la watu wasiojulikana, huku taarifa nyingine zikionyesha kuwa miongoni mwa watu wanaofuatilia nyendo zake kwa karibu ni polisi.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Bashe naye ni mmoja wa wanasiasa ambao misimamo yao ya kisiasa imekuwa ikiwatesa baadhi ya vigogo wa kisiasa hapa nchini na zipo pia taarifa kuwa hatua yake ya kutangaza kumuunga mkono mmoja wa wanasiasa waliotajwa kutaka kuwania urais kupitia CCM imezidi kumjengea maadui, hususan mahasimu wa kisiasa wa kambi anayoiunga mkono.

Kwa mujibu wa Bashe, mapema mwaka huu akiwa anatoka ofisini kwake, gari la polisi lililokuwa na askari wenye silaha lililokuwa limeegesha nje ya ofisi yake lilianza kumuandama na kumsimamisha akiwa eneo la Sinza Makaburini, ambapo askari hao walidai kuwa wana wasiwasi naye na baada ya kumhoji walimuacha.

Bashe, akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, katika mkutano wa wadau wa habari, alisema tukio hilo lilitokea akiwa ameandamana na Kibanda. Alisema kabla ya tukio hilo, gari lake liliwahi kugongwa kwa nyuma na gari aina ya pick up ambalo lilikimbia baada ya tukio hilo na mwishoni mwa wiki iliyopita watu wanaodhaniwa kuwa polisi walifika katika ofisi za New Habari majira ya usiku na kujaribu kuingia ndani ya uzio wa ofisi hizo kwa uficho, kabla ya kutambuliwa na walinzi ambao walifukuzwa pamoja na mbwa.

Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa Bashe anao maadui ndani ya CCM anaohasimiana nao kwa muda mrefu na chanzo cha uhasama huo kinaelezwa kuwa ni vita ya makundi ya ndani ya chama ambayo yanapambana kushika hatamu za uongozi wa dola mwaka 2015.

Mwingine katika orodha ni mwandishi wa habari, Msaki ambaye naye taarifa za uchunguzi wa MTANZANIA Jumapili zimeonyesha kuwa amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na kundi hilo la watu wasiofahamika.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Msaki, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, amekuwa akitajwa kuwa karibu na kundi la akina Lowassa, lakini pia akiwa na urafiki wa karibu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi na Zitto.

Msaki pia anatajwa kulengwa na kundi la wahalifu linalohasimiana na Zitto kutokana na ukaribu wake na mwanasiasa huyo, ambapo inaaminika ni mmoja wa makamanda wanaoratibu mikakati ya vita yake ya kisiasa dhidi ya maadui zake.

Uchunguzi wa Mtanzania Jumapili umeonyesha Msaki aliwahi kuvamiwa na watu wasiojulikana wakati akiwa hayupo, ambao waliondoka na kasiki ya kutunzia pesa iliyokuwa na nyaraka zake mbalimbali za kazi.

Vyanzo vya habari kutoka Mwananchi Communication Ltd vimeeleza kuwa Msaki aliwahi kuibiwa kompyuta yake ndogo iliyokuwa ofisini kwake na watu wasiojulikana na kwamba katika siku za karibuni amekuwa akiandamwa na watu wasiofahamika, jambo ambalo limemfanya aishi maisha ya wasiwasi.

Mbali na Msaki, miongoni mwa viongozi wa dini wanaowindwa ni pamoja na Askofu Valentino Mokiwa, ambaye misimamo yake inahusishwa na siasa zinazoegemea kundi fulani la watu wanaowania madaraka 2015.

Tayari Askofu huyo alivamiwa nyumbani kwake wiki iliyopita na watu wasiojulikana ambao baada ya kumkosa walimjeruhi vibaya mlinzi wake.

Kauli ya Polisi

MTANZANIA Jumapili ilimtafuta msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, ili kuzungumzia taarifa ya kutafutwa kwa watu hao, alisema kuwa suala la uchunguzi wa tukio alilofanyiwa Kibanda, lipo chini ya polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na hivyo akashauri kuwasiliana na Mkuu wa Kanda hiyo, Suleiman Kova

Hata hivyo juhudi za gazeti hili ziligonga mwamba, baada ya simu ya mkononi ya Kamanda Kova kutokupatikana muda wote.

Dk. Bashiru Ally azungumza

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally, amesema kitendo cha kinyama alichofanyiwa Mhariri wa Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda ni cha kukanganya.

Akizungumza na Mtanzania Jumapili kwa njia ya simu, Dk Bashiru alisema tukio hilo limesababisha jamii kutoamini mamlaka husika.

Dk. Benson Bana

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema matukio yanayotokea sasa ya watu fulani fulani kuwindwa na wengine kudhurika yanatokana na msuguano wa kuwapo na makundi ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Alisema kuwa umefika muda kwa Rais Kikwete kuteua warithi wake mapema ambao watapunguza hali ya mnyukano wa urais ndani ya CCM.

Dk. Azaveli Lwaitama

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema matukio ya sasa yanafanywa na watu wa kundi fulani linalowatumia usalama wa taifa vibaya.

Alisema kundi hilo bila shaka ni miongoni mwa yale yanayowania urais 2015.

“Nakumbuka Mwigulu Nchemba ameishawahi kusema kwamba kuna mkanda wa video, haujaelezea unazungumzia nini na hivyo anatakiwa ahojiwe, kumeishawahi kumwagwa vipeperushi vya uchochezi katika vikao fulani vya juu vya CCM mjini Dodoma, mtu aliyeviandaa mpaka leo hajulikani …sasa iweje leo Chadema wabambikiwe jambo hili, haya ni mapambano ya urais 2015,” alisema Dk. Lwaitama.

Imeandikwa na Mtanzania Jumapili, Machi 17, 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO