Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lwakatare ashtakiwa kwa ugaidi

na Happiness Katabazi

 

MKURUGENZI wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya ugaidi.

Lwakatare ambaye anatetewa na jopo la mawakili wanne Prof. Abdallah Safari, Tundu Lissu, Peter Kibatara na Nyaronyo Kichere, alishtakiwa pamoja na Ludovick Joseph ambaye anakabiliwa na mashtaka matatu.

Washtakiwa hao wakifikishwa mahakamani hapo saa mbili asubuhi chini ya ulinzi mkali wa askari kanzu waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ilala, Duwani Nyanda.

Washtakiwa hao waliingizwa ndani ya ukumbi namba moja wa mahakama saa 7:06 mchana chini ya ulinzi mkali huku Lwakatare akiwasalimu wafuasi wa CHADEMA waliofurika kwa wingi akiwaonyesha ishara ya vidole viwili.

Jopo la mawakili wakuu wa seriakali likiongozwa na Mwanasheria Kiongozi wa Kanda ya Dar es Salaam, Ponsian Lukosi, Purdence Rweyongeza na Peter Mahugo, lilidai kuwa hati ya mashtaka ina jumla ya makosa manne.

Wakili Rweyongeza alilitaja kosa la kwanza ambalo linawakabili washtakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Kwamba Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Denis Msaki  ambaye ni mwanahabari wa gazeti la Mwananchi.

Kosa la pili ni kula njama; kosa ambalo pia linawakabili washtakiwa wote ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Katika kosa la tatu, washtakiwa wote wawili wanadaiwa kufanya mkutano wa kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana, washtakiwa walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.

Alilitaja shtaka la nne ambalo linamkabili Lwakatare peke yake kuwa ni kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki wa nyumba hiyo iliyoko Kimara King’ong’o  kwa makusudi aliruhusu  kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki.

Washtakiwa wote walikanusha mashtaka hayo huku Wakili Rweyongeza akidai kuwa makosa  hayo yaliletwa chini ya sheria mbili tofauti yaani kosa la kwanza linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu lakini makosa yaliyosalia yanaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia ugaidi.

Aliongeza kuwa makosa yanayoangukia kwenye sheria ya ugaidi huwa  hayana dhamana na kwamba ni Mahakama Kuu peke ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Rweyongeza aliieleza mahakama kuwa jamhuri inawasilisha ombi la pili ambapo wanaiomba mahakama imruhusu mshtakiwa wa pili (Ludovick) aende kukaa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi kwa sababu anahitajika kwa ajili ya hatua za kiupelelezi zaidi.

Hata hivyo wakili wa utetezi, Peter Kibatara, aliiomba mahakama iwapatie wateja wake dhamana na kwamba suala la washtakiwa kupatiwa dhamana au kunyimwa ni la mahakama.

Kwa upande wake wakili Lissu alidai hati ya mashtaka ni kipande cha karatasi kilichowasilishwa na DPP, Dk. Elieza Feleshi, ambacho hakionyeshi nembo ya serikali, mhuri na wala hakikuletwa mahakamani hapo kwa ridhaa ya DPP.

Lissu aliomba mahakama hiyo isikiamini hicho kipande cha karatasi kuwa ni waraka halali wa serikali.

Kwa upande wake wakili, Prof. Safari, aliiomba mahakama irejee kesi za kubambikiwa zilizowahi kufunguliwa mahakamani hapo na ofisi ya DPP miaka ya nyuma ikiwemo kesi ya mauji ya fundi majeneza wa Manzese ya mwaka 2002, iliyofunguliwa na jamhuri dhidi ya Sheikh Issa Ponda na Sheikh Kundecha.

Alidai kuwa wakati huo alikuwa akiwatetea washtakiwa hao ambapo alilazimika kwenda kuonana na DPP pamoja na jaji mstaafu kwa sasa Juxon Mlai, kumueleza kuwa kesi ile ya mauaji ni ya kubambikwa ambapo Mlai alitumia mamlaka yake kuifuta.

“Katika kesi hii ya Lwakatare ninachokiona ni matumizi mabaya ya sheria na wale waliombakizia kesi Lwakatare wanastarehe na kufurahi kuona anaenda kuishi gerezani,” alidai Prof. Safari.

Akipangua hoja za mawakili hao wa utetezi, Rweyongeza alidai kuwa hoja hizo tatu ni dhaifu na kwamba anaomba mahakama isiione kesi hii ni ya macho ya chama fulani cha kisiasa.

Kuhusu hoja ya kuwabambikizia kesi washtakiwa hao, Rweyongeza alidai kesi hiyo siyo ya kubambikiziwa  na kwamba ofisi ya DPP inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria.

Akijibu hoja ya Lissu, alimtaka aache kasumba ya kuongea mambo bila ya kufanya utafiti kwani DPP amefungua kesi hiyo na amewasilisha kibali chake mahakamani hapo ambapo wakili huyo alikitoa kibali hicho kama kielelezo.

Kuhusu hoja ya kutaka washtakiwa wapatiwe dhamana, Rweyongeza alidai kuwa sheria ya ugaidi imetungwa na Bunge ambapo kifungu cha 49 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kinakataza kabisa mshtakiwa kupewa dhamana.

Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba atatolea uamuzi kesho na kuamuru washtakiwa wote wapelekwe mahabusu, huku akiikataa hoja ya wakili Kibatara iliyotaka Lwakatare apelekewe daktari maalumu wa kuangalia afya yake kwani ni mgonjwa

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO