Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mbunge wa CUF afariki

MBUNGE wa Chambani, kisiwani Pemba, Salim Hemed Khamis (CUF), pichani, amefariki ikiwa ni siku moja baada ya kuanguka ghafla wakati akishiriki kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje.

Hamisi (62) alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa baada ya afya yake kuzorota ghafla juzi.

Kutokana na msiba huo kamati za kudumu za Bunge zimeahirisha kazi zake kwa muda hadi baada ya kumalizika siku kuu za Pasaka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa kwa mujibu wa daktari, Khamis amefariki kutokana na shinikizo la juu la damu lililosababisha mishipa ya ubongo kupasuka.

Alisema kuwa kupasuka huko kulisababisha damu nyingi kuvuja katika ubongo ambapo madaktari walikuwa wakijitahidi kumsaidia lakini ilishindikana.

Joel alisema kuwa mbunge huyo ambaye aliwahi kutibiwa mjini Dodoma na nchini India alifariki saa 6:00 mchana jana.

Awali, mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ambayo marehemu alikuwa mjumbe wake, Edward Lowassa, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.

“Jana tulikwenda kumtazama na alikuwa anaendelea vizuri na hata leo nimetoka kumuangalia na presha yake iliyokuwa imepanda ilikuwa imeshashuka, lakini ndio hivyo ni mpango wa Mungu,” alisema.

Lowassa alisema kuwa Khamis alianza kujisikia vibaya wakiwa kwenye kikao na watendaji wa ICC ambao miongoni mwao alikuwepo daktari aliyewashauri wampeleke hospitali kabla ya kuishiwa nguvu na kuanguka.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa walipokea kwa masikitiko taarifa hizo.

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema kuwa ni pigo kwa Bunge na CUF kwani marehemu alikuwa anajituma na kuchangia mada vizuri bungeni hususan katika masuala ya kilimo.

Nacho chama cha CUF kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Julius Mtatiro, kimeeleza kuwa kimepokea kwa masikitiko kifo cha mbunge huyo na kwamba baada ya kukaa kikao na Spika wa Bunge, Anna Makinda, viongozi na wabunge wamekubaliana azikwe leo.

“Kuanzia saa 2:30 mpaka saa 4:00 asubuhi, mwili wa marehemu utaagwa katika ukumbi wa Karimjee na baada ya hapo utasafirishwa kuelekea Pemba na mazishi yatafanyika saa 7:00 mchana Chambani.

Wabunge 12 wameteuliwa kuhudhuria mazishi hayo akiwemo Lowassa pamoja na katibu wake katika Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Mussa Zungu.

Huyu ni mbunge wa nne kupoteza maisha tangu Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipochaguliwa, akitanguliwa na Regia Mtema wa Viti Maalumu (CHADEMA), Jeremiah Sumari (Arumeru Mashariki) na Mussa Khamis Silima (Baraza la Wawakilishi) wote wa CCM.

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO