Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

SAKATA LA KIBANDA, LWAKATARE: Mtuhumiwa mwingine akamatwa

 

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph Ludovick, amekamatwa na Jeshi la Polisi akihusishwa na matukio ya kigaidi ambayo yamelitikisa taifa katika siku za karibuni.

Habari za kuaminika zilizozifikia MTANZANIA Jumapili zimeeleza kuwa, Tume ya watu 12 iliyoundwa na serikali kupitia vyombo vyake vya usalama kuchunguza tukio la kutekwa na kuteswa kinyama kwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd. Absalom Kibanda, imemkamata Ludovick akiwa mkoani Iringa.

Kwamba, Ludovick amekamatwa na makachero wa polisi baada ya kupatikana kwa taarifa zinazomhusisha kupanga njama za kudhuru watu na pia kuwepo kwa mazingira yenye shaka kuhusu mwenendo wake usiku wa tukio la kutekwa kwa Kibanda.

Hata hivyo, taarifa nyingine zilizopatikana zinadaiwa kuwa kukamatwa kwa Ludovick, ambaye pia anadaiwa kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, ni mkakati unaoratibiwa kwa umakini wenye lengo la kupoteza mwelekeo wa uchunguzi wa tukio la kutekwa na kuteswa kinyama Kibanda.

Kibanda alitekwa na kujeruhiwa usiku wa kuakia Machi 6 mwaka huu, nyumbani kwake Mbezi, jijini Dar es Salaam, akiwa ndani ya gari lake akisubiri kufunguliwa geti aingie ndani.

Katika tukio hilo, Kibanda alijeruhiwa kwa kupigwa mapanga kichwani, kung’olewa meno na kucha, kutobolewa jicho na kunyofolewa kidole.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilieleza kuwa Ludovick, ambaye ni mkazi wa Jijini Dar es Salaam, alikamatwa juzi akiwa mkoani Iringa.

Habari za kukamatwa kwa Ludovick zilianza kuenea tangu juzi usiku katika mitandao mbalimbali ya kijamii, kabla ya jana kuthibitishwa na polisi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa viongozi wake wakuu, akiwemo, Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, walikwepa kuzungumzia tukio hilo.

Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alipotafutwa na MTANZANIA Jumapili kupitia simu yake ya kiganjani ili kuthibitisha kukamatwa kwa Ludovick alishindwa kukubali au kukataa.

Senso alilitaka gazeti hili liliache Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake na kisha kutoa taarifa yake baadaye.

Kuhusishwa kwake na tukio la Kibanda

Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa siku na wakati ambao Kibanda alitekwa na kuteswa, Ludovick naye alidai kutekwa na majambazi akiwa eneo la Sinza, jirani na mahali ilipo ofisi ya Kibanda.

Duru za habari zinaeleza kuwa Ludovick alidai kutekwa na watu wasiojulika majira ya saa tano usiku siku ya Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, ambapo watekaji wake walimnyang’anya vitu vyake mbalimbali na kumvua nguo zote.

Taarifa hizo zinathibitishwa na mwanablog maarufu, Maggid Mjengwa, ambaye katika andishi lake aliloweka kwenye mitandao ya kijamii jana, anaelezwa kuwa Ludovick, alidai kutekwa na kuvuliwa nguo na kwamba tukio hilo aliripoti katika kituo cha Polisi cha Kigogo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mjengwa kwenye gazeti hili na yale aliyoyaeleza kwenye mtandao wa Jamii Forum, siku ya kutekwa na kuteswa kwa Kibanda alikuwa pamoja na Ludovick kwenye mgahawa wa Rose Garden, ambako walikula chakula jioni kabla ya kuondoka pamoja kwenye gari lake hadi eneo la Sinza Shekilango, alipomuacha akidai kuchukua usafiri wa umma kuelekea nyumbani kwake eneo la Tabata.

Mjengwa anasema baadaye usiku huo, Ludovick alikwenda hadi hoteli aliyofikia eneo la Kariakoo, huku akiwa hana nguo na kumueleza kuwa alitekwa na majambazi muda mfupi baada ya kuachana naye.

Anasema taarifa za kutekwa kwake (Ludovick) aliziripoti katika kituo cha Polisi Kigogo, ingawa kwa mujibu wa maelezo aliyompa Mjengwa ni kwamba alipofika Shekilango, alichukua bajaj ambayo alipanda na watu wengine wawili, yeye akiwa katikati na alipofika katika eneo la Relini Tabata alihisi watu aliokuwa nao ni majambazi.

Hata hivyo, haijajulikana mara moja ni kwa nini akiwa alitekwa eneo la Relini, alikwenda kuripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi cha Kigogo.

Pia haijajulikana sababu za kukimbilia hotelini alikofikia Mjengwa badala ya nyumbani kwake, Tabata.

Maswali hayo pia yamempatia kigugumizi Mjengwa, ambaye hata hivyo anakiri kumfahamu Ludovick anaeleza kuwa amekuwa akimsaidia baadhi ya kazi zake za kihabari, lakini anasema hamfahamu sana.

Ludovick ni miongoni mwa watu waliofika katika Hospitali ya Muhimbili asubuhi kumjulia hali Kibanda, na alikaa hadi Kibanda anasafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Ahusishwa na video ya Lwakatare

Habari zaidi zilizolifikia MTANZANIA Jumapili, zinadai kuwa Ludovick ndiye mtu aliyerekodi video ambayo Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, anaonekana akipanga mipango ya kudhuru watu mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari.

Wapasha habari wetu wanaeleza kuwa Ludovick ndiye mtu ambaye sauti yake inasikika katika video hiyo, hata hivyo habari hizo hazijathibitishwa na Jeshi la Polisi.

Katika video hiyo iliyosababisha Lwakatare atiwe nguvuni na Polisi hadi sasa, Ludovick anadaiwa kuwa ndiye mtu ambaye alikuwa akimuuliza maswali Lwakatare, wakati wakiandaa mipango hiyo.

Watu wa karibu na Ludovick waliliambia gazeti hili kuwa, Lwakatare na Ludovick wana uhusiano wa karibu na kwamba wote ni wenyeji wa Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa watu hao, ukaribu kati ya Ludovick na Lwakatare ni wa muda mrefu na amepata kumsaidia kufanya kampeni za kuwania ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mwaka 2000.

Wakati huo huo, inadaiwa kuwa Lwakatare mwenyewe amekiri kuwa mtu anayeonekana akizungumza katika mkanda wa video maneno ya kupanga matukio ya utekaji ni yeye na pale anapoonekana akizungumza ni nyumbani kwake, lakini amekataa kwamba maneno anayozungumza si yeye.

Ludovick ni nani?

Ludovick, mbali na kuwa na ukaribu na Lwakatare, pia ni mtu wa karibu na Mjengwa, akimsaidia katika shughuli mbalimbali hususani katika blog yake.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba Ludovick ni mtu wa idara ya usalama wa taifa na watu ambao wako naye karibu wanasema hawajui anafanya kazi gani zaidi.

Alipoulizwa ni kazi gani ambayo Ludovick anafanya, Mjengwa alisema hajui.

Ila katika maelezo yake aliyoandika kupitia kwenye mtandao wa Jamii Forum, Mjengwa anasema anamfahamu Ludovick tangu akiwa Chuo Kikuu (DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania wengi waliomfahamu kupitia kazi zake magazetini.

Haijaeleweka mara moja uhusiano wake na Lwakatare ni wa aina gani na katika kazi gani.

Chanzo: Mtanzania Jumapili, Machi 17, 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO