MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kuzima mitambo ya analojia katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro Jumapili ya Machi 31, ili iingie katika mfumo wa digitali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi Mkuu wa Utangazaji wa TCRA, Habbi Gunze, alisema maandalizi yote kwa ajili ya uzimaji mitambo hiyo yamekamilika.
Alisema uzimaji huo utahusisha watumiaji wa luninga pekee ambapo watalizimika kutumia ving’amuzi ili kupata matangazo hayo.
Gunze alisema kwa siku tano wanaendelea kutoa elimu kwa umma kuwafahamisha uzimaji huo wa mitambo ya analojia na kutoa maagizo kwa wasambazaji wa huduma za ving’amuzi kuongeza huduma hiyo katika maeneo mengi ndani ya mikoa hiyo.
“Tuna uhakika idadi ya ving’amuzi vilivyopo hivi sasa katika mikoa hiyo miwili vinatosha na hivyo hatutegemei uwepo wa foleni katika vituo vya kupatia huduma hiyo,” alisema Gunze.
Awali, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa mamlaka hiyo, Mhandisi Anethi Matindi, alielezea changamoto zinazokumbana na zoezi hilo kuwa ni pamoja na huduma kwa wateja kutoka makampuni yanayosambaza ving’amuzi hivyo kutokuwa bora.
Pia alisema changamoto kubwa nyingine ni uelewa wa wananchi katika kutumia ving’amuzi hivyo, hali inayosababisha maeneo mengi kwa waliofunga ving’amuzi kutopata picha vizuri na hivyo kuwa na malalamniko mengi.
Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment