RAFIKI yangu Kalasinga wa kule Njiro, Mrenyii wa kituo cha mabasi na Mrema wa pale kituo cha Vifodi Arusha ndio walionituma leo niulize kama askari walisoma kanuni za maadili za Jeshi la Polisi ukutani kabla ya kwenda kumkamata Godbless Lema?
Kanuni hizi zipo kila kituo cha polisi, kama kuna wengine hawazisomi huko naomba wasome hapa. Kanuni za maadili za Jeshi la Polisi Kamanda wa Polisi wa Arusha anazijua, Mkuu wa Polisi wa wilaya anazijua, na Mkuu wa Upepelezi ambaye kwa namna ya pekee alinikasirikia nisihojiane naye bila shaka naye anazijua.
Haya si maneno yangu, ni ya baadhi ya wakazi wa Arusha, pamoja na hao ambao nimewataja hapo juu. Wanahoji utendaji wa Jeshi la Polisi jijini Arusha lilivyojiaibisha. Lilivyotumika kisiasa bila kutumia akili yake.
Sisi askari wa upande wa polisi jamii wenye nia na mapenzi mema kwa nchi yetu turudie kuzisoma kanuni hizi na maadili yao.
Kanuni hizi zinasema: “Nikiwa ofisa wa polisi nina wajibu wa kutekeleza sheria, wajibu wangu ni kuwahudumia watu, kulinda maisha na mali.
“Kuwalinda wasio na hatia dhidi ya udanganyifu, dhaifu dhidi ya ugandamizaji au vitisho na utulivu dhidi ya vurugu au fujo, kuheshimu haki za kikatiba za raia wote katika uhuru usawa na haki.
“Nitatunza heshima yangu binafsi kama mfano kwa wote, kuwa jasiri wakai wa utulivu na wakati wa hatari. Sitakuwa na dharau au dhihaka, kuwa na uvumilivu na kujali ustawi wa wengine.
“Nitakuwa mwaminifu kimawazo na kimatendo katika maisha yangu binafsi na ya kijamii. Nitaonyesha mfano wa kufuata sheria za nchi na kanuni ya idara yangu. Chochote nitakachoona au kusikia ambacho ni siri au ambacho nimeaminiwa kutokana na wadhifa wangu kitakuwa siri isipokuwa tu pale itakapobidi kufichuliwa katika kutekeleza wajibu wangu.
“Sitaingilia au kuruhusu hisia binafsi, chuki, uhasama au urafiki viathiri uamuzi wangu, sitakubaliana na uhalifu. Nitatekeleza sheria kwa heshima na inavyopasa bila woga au upendeleo, uovu au nia mbaya.
“Sitatumia kamwe nguvu za ziada bila sababu, ninatambua kuwa beji yangu ni ishara ya uaminifu wangu kwa umma, nitakuwa mwadilifu kwa umma na kwa maadili ya kazi za polisi. Nitajitahidi muda wote kufikia malengo hayo na kujitoa kikamilifu kwa Mungu, kwa chaguo la kazi ya kutekeleza sheria.”
Polisi ambao hadi leo sijapata jibu kama wamemkamata aliyeua mwanachuo kuile Arusha, ndio walioamua kutokulala, kwenda kukesha nyumbani kwa Mbunge wa Arusha mjini, Lema kwa bunduki, mabomu, mbwa na kuwekeza kila aina ya mbinu eti kumkamata.
Nimeombwa niulize huyu Lema alifanya kosa gani kubwa ambalo angesubiriwa kesho yake asingeonekana?
Je, mbunge huyu angeweza kutoroka kwa sababu ya kauli ya kumwambia Mkuu wa Mkoa kuwa anakuja kama anaenda kwenye “Send Off”? Kama mbunge anakamatwa kwa vitisho hivi, hizo kanuni tunazotaja hapo juu zilizingatiwa?
Maneno haya kwamba: “Sitaingilia au kuruhusu hisia binafsi, chuki, uhasama au urafiki viathiri uamuzi wangu, sitakubaliana na uhalifu.
“Nitatekeleza sheria kwa heshima na inavyopasa bila woga au upendeleo, uovu au nia mbaya. Sitatumia kamwe nguvu za ziada bila sababu” nimetumwa niwaulize nguvu waliyotumia kumkamata Lema kweli ilihitajika?
Je, hapa kulikuwepo na chuki au uhasama katika maamuzi yaliyofikiwa katika kumkamata mbunge huyo?
Kwanini jeshi letu litumike kwa mambo ya aibu hivi? Jeshi letu linazidi kushuka hadhi siku hadi siku sio kwa kuwa kanuni zao ni mbovu, kanuni zao ni nzuri isipokuwa hazifuatwi, na viongozi wakubwa wa jeshi ndio viongozi wa kuvunja kanuni hizi.
Nimeombwa niulize hivi polisi hawakujua suala hili? Kama Lema alikosea sana wakati akiwa Chuo cha Uhasibu kwanini Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na makachero wote hawakumkamata pale pale? Alifanya kosa hilo baada ya kuondoka?
Kama alifanya vile kwanini aliachwa ili aende na kuja kutafutwa baadaye? Maneno ya Lema yalionekana kuwa kosa baadaye wakati wanafunzi wametawanyika na mbunge huyo akaenda zake?
Hakuna uwezekano wowote kukubali kuwa jeshi letu halitumiki vibaya. Kila tendo lina gharama zake, hili la kumkamata Lema limegharimu heshima ya Jeshi la Polisi. Huo ndio ujumbe niliotumwa niwaambie. Si maneno yangu, mtapima kama mpo tayari kubadilika au la.
Chanzo: tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment