Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Chadema waonyesha picha za video alivyouawa Mwangosi

 

*Picha zinaonyesha jinsi RPC Iringa alivyoshuhudia tukio
*Zinaonyesha baada ya Mwangosi kuuawa, polisi walilaumiana
*Waandishi wa habari, viongozi wa Chadema waangua vilio

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonyesha picha za mnato na video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alivyouawa.

Picha hizo zilionyeshwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichohudhuriwa pia na waandishi wa habari. Kikao hicho cha Kamati Kuu kilikuwa ni cha dharura na kilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Wakati picha hizo zikionyeshwa wazi wazi, viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari, walishindwa kujizuia kwani baadhi yao walijikuta wakiangua vilio wakionyesha kusikitishwa na jinsi Mwangosi alivyouawa.

Katika tukio hilo, Mbowe ni kati ya waliolia na ilifika wakati akanyanyuka kutoka meza kuu na kwenda nje ya ukumbi, ili asiendelee kushuhudia Mwangosi alivyouawa.

Wakati picha hizo zikionyeshwa kwa zaidi ya masaa mawili, askari polisi walioshiriki kumuua Mwangosi walionekana wazi wazi na pia Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana pia eneo la tukio akishuhudia Mwangosi akiuawa.

Kwa mujibu wa picha hizo, mwandishi wa habari aliyeanza kukamatwa na askari polisi na kupata kipigo ni Godfrey Mushi wa Gazeti la Nipashe.

Picha hizo za video zilionyesha kuwa, baada ya Mushi kukamatwa, Mwangosi alikwenda kumuokoa mwenzake huyo na alipofika eneo la tukio, askari hao walianza kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda Kamuhanda.

Picha hizo zinaonyesha kuwa, kabla Mwangosi hajauawa, polisi mmoja alipitisha bunduki yake miguuni kwa polisi mwenzake kisha Mwangosi akauawa.

Baada ya tukio hilo, picha hizo zinaonyesha kuwa, baadhi ya askari polisi waliokuwa wakimpa kipigo Marehemu Mwangosi, walikimbia na kuacha mwili wa marehemu ukiwa vipande vipande.

Kwa mujibu wa picha hizo, polisi hao walipokuwa pembeni, wenyewe kwa wenyewe walianza kulaumiana huku baadhi yao wakimlaumu muuaji na kusema umefanya nini hicho?.

Baada ya hapo, mmoja wa polisi hao alisikika akisema twende tukamchukue mwenzetu na walipofika mahali alipokuwa mwenzao ambaye alikuwa amejeruhiwa kwa bomu lililomuua Mwangosi, gari ya Kamanda Kamuhanda ilisogea karibu na kumpakia askari polisi aliyejeruhiwa.

Picha hizo za video ambazo zinaonekana zilirekodiwa kwa umakini wa hali ya juu, zinaonyesha baada ya mauaji hayo, askari walishikwa na butwaa huku baadhi yao wakionekana kushika pua.

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya askari ambao ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walionekana katika mkanda huo wa video, wakifungua kofia zao zilizokuwa zimefunika uso na macho yao, ili waone vizuri maiti ya Mwangosi iliyokuwa vipande vipande.

Wakati wakivua kofia hizo, baadhi yao walikuwa wakinawa nyuso zao kutokana na moshi uliokuwa umesambaa eneo la tukio wakati walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA.

Pia picha hizo, zilionyesha askari polisi mmoja akiwa amevaa kiraia, huku shingoni akiwa na skafu ya CHADEMA lakini baada ya vurugu kuanza, askari huyo alionekana akiivua skafu hiyo na kuiweka mfukoni.

Alipoivua na kuiweka katika mfuko wa nyuma wa kaptula aliyokuwa amevaa, mwenzake mmoja akampa kofia ya kujikinga na moshi kisha askari huyo akachomoa bastola kwa ajili ya mapambano.

Pamoja na picha hizo kuwaonyesha askari polisi walivyotekeleza tukio hilo, Kamanda wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wa CHADEMA, Benson Kigaila, alionekana pia akijibizana na ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Iringa kuhusu wafuasi wa CHADEMA kuwepo katika Kijiji cha Nyololo kilichopo Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Vile vile, picha hizo za video, awali zilionyesha marehemu Mwangosi alivyokuwa akimuuliza Kamanda Kamuhanda kuhusu sheria ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na maswali hayo yalionyesha jinsi kamanda huyo wa polisi alivyokuwa amechukizwa nayo.

Kutokana na picha hizo, Mbowe alisema huo ni ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi Jeshi la Polisi lilivyokuwa limedhamiria kuua.

Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA itatoa tamko zito leo kuonyesha ni hatua gani zitachukuliwa baada ya kifo cha Mwangosi.

KABLA YA PICHA

Awali, akifungua kikao hicho, Mbowe alisema ajenda zitakazojadiliwa na kutolewa tamko ni za kitaifa, kijamii na kiusalama kwa manufaa ya wananchi wote.

Mbowe alianza kutoa pole kwa waandishi wa habari nchini kutokana na kifo cha Mwangosi na kuwataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho kamati imeundwa kuchunguza tukio hilo.

“Kifo cha mwenzenu marehemu Mwangosi kimetugusa sote, ninachoweza kusema ni kwamba, kimesababishwa na Jeshi la Polisi kwa lengo wanalolijua wenyewe, lakini najua wanataka kuwadhoofisha.

“Jambo jingine ambalo napenda kuwaeleza waandishi, ni kwamba sote tunafahamu Rais Jakaya Kikwete alivyo mwepesi kutoa pole na kuhudhuria pale panapotokea msiba, lakini hadi sasa kitu hicho hakijafanyika.

“CHADEMA tunalaani sana kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kutoa pole hata ya kauli, huku akijua tukio hilo limegusa watu wote duniani, tunashangaa kuendelea kutatua migogoro ya nchi nyingine, huku ya kwetu yakitushinda.

“Hakuna asiyefahamu kuna migogoro ya walimu, madaktari, wafanyakazi wa kada mbalimbali, wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla, lakini hakuna jitihada zozote zinazofanyika kutatua badala yake

KAULI YA TENDWA

Akizungumzia kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, aliyesema wiki iliyopita, kwamba atakifuta CHADEMA kama mauaji yataendelea kutokea kwenye mikutano yao, Mbowe alisema haitawezekana chama hicho kufutwa vinginevyo ni kuhatarisha amani ya nchi.

Mbowe alisema, mpango wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia vyombo vya dola kama polisi na viongozi kutaka kuzuia mikutano ya M4C inayoendelea nchi nzima, hautafanikiwa.

“Tendwa asijaribu kutoa kauli za kuhatarisha amani ya nchi, kama ni kufuta vyama aanzie CCM, CHADEMA sio chama cha mfukoni, kama amelewa na usajili wa vyama na kuwa kibaraka wa CCM sasa amekanyaga pabaya.

“Napenda kutangaza rasmi kwamba, mikutano ya M4C itaendelea nchi nzima na hakuna mtu anayeweza kuizuia, tunataka kuleta demokrasia na mabadiliko ya kweli.

“Serikali ya CCM isijaribu kuleta machafuko nchini, itambue kwamba, CHADEMA ina mamilioni ya wafuasi na kila siku wanaendelea kuongezeka na kama Serikali hii itaendelea kulea ufisadi, wizi, ubabaishaji, mauaji na kushindwa kuwajibika kwa wananchi, ijue mwisho wake umefika, hakuna cha kulindana,” alisema.

tunaendelea kuongeza matatizo mengine,” alisema Mbowe.

TUZO KWA WAANDISHI
Akizungumzia picha zilizopigwa na waandishi wa habari siku ya tukio la mauaji ya marehemu Mwangosi, alisema wanastahili kupatiwa tuzo.

Mbowe alisema kuwa, CHADEMA kinaandaa tuzo kwa waandishi wa habari waliopiga picha za video na mnato katika tukio la mauji ya marehemu Mwangosi.

“Waandishi wa habari wameonyesha uhodari mkubwa sana licha ya kuwa katika msukosuko wa mabomu ya polisi, picha zilizopigwa zimeondoa dhamira chafu ya polisi na Serikali ya CCM, kutaka kutumia mwanya huo kukichafua CHADEMA, picha zote za mnato na video zimeonyesha ukweli wa jambo na wahusika.

“Sisi kama CHADEMA tunathamini mchango wa vyombo vya habari na umuhimu wake na ni mtaji mkubwa sana kwetu, tumesikia waandishi wanatafutwa hatutasita kuwasaidia na mpaka sasa tupo sambamba katika hili,” alisema.

AISHUKIA TBC
Katika hali nyingine, Mbowe alionyesha kutoridhishwa na mwenendo wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), kwa kusema kuwa limekuwa likifanya kazi ya kuibomoa CHADEMA badala ya kueleza ukweli ulivyo.

DK. SLAA

Naye Katibu Mkuu CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa alikiri kumtumia ujumbe mfupi wa simu za mkononi (SMS), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Said Mwema na kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.

Alisema alituma ujumbe huo baada ya kuzuiwa barabarani na polisi wakati wakiwa katika mikutano ya M4C.

Alisema baada ya kuzuiwa na kushushwa kwenye magari yao wakiwa mkoani Iringa na kulazimishwa kutembea kwa miguu hadi hotelini, aliamua kumpigia simu IGP Mwema na kumuelezea jambo hilo, lakini hakumjibu na ndipo alipoamua kumtumia ujumbe huo mfupi.

Hata hivyo alimtaka IGP Mwema na Tendwa kueleza chanzo cha kutuma ujumbe huo na kuachana na tabia ya kupotosha jamii.

Alisema kama kweli sms hiyo aliituma kwa uchochezi ni vema wamkamate na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria

Imechapishwa na Mtanzaia, Jumatatu, Septemba 10, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO