Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

JK: Sijauza ardhi kwa George Bush • Awasuta wapinzani, ataka wafanye zaidi wakishinda

RAIS Jakaya Kikwete, amekana kumuuzia ardhi ya eneo la Mji Mpya wa Kigamboni Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush, akisema kuwa madai hayo ni uzushi na upotoshaji.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuzuka kwa tetesi hizo wakati akizindua rasmi ujenzi wa daraja la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Tetesi hizo za uuzwaji wa eneo hilo ambalo linatarajiwa kujenywa mji mpya wa Kigamboni, zilivuma miaka kadhaa nyuma hasa baada ya Rais Bush kuzuru Tanzania mwaka 2008 na kushika kasi baada ya kuja nchini Desemba mwaka jana akiwa amemaliza utawala wake.

“Watu wana uongo mwingi eti nimeuza eneo kwa Bush, huo ni upotoshaji mwingi. Maana kuna watu kila kukicha wana viwanda vya kutengeneza uongo. Wako ambao hawapendi maendeleo,” alisema.

Alibainisha kuwa amefanikisha ujenzi wa madaraja, barabara, shule lakini yote wapinzani wake wanayaona mabaya, kwamba watu wengi wa aina hiyo hawafurahi kuona serikali yake inavyofanikiwa na hivyo wanatamani washindwe.

Rais Kikwete aliwataka wapinzani wajifunze utamaduni wa kusifu yale mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM ili nao wakipata madaraka wafanye mara tatu maana ni lazima wataendeleza pale alipoishia yeye.

Alisema mara kadhaa watu wamekuwa wakiwabeza ili waweze kuwatoa katika mstari kwa kile walichokilenga kufanya lakini wamekuwa hawayumbi na wala kutoka nje ya mstari.

Rais alifafanua kuwa ujenzi huo utagharimu kiasi cha sh bilioni 214.6 ambapo asilimia 60 ni fedha za Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na 40 zitatolewa na serikali.

Akizungumzia umuhimu wa daraja hilo, Rais Kikwete alisema litasaidia kukuza uchumi kutokana na kujengwa kwa kuungana na barabara za juu na chini ‘fly overs’ ambazo zitaunganisha hadi barabara ya Nyerere na Mandela.

Kuhusu ujenzi wa makazi mji mpya wa Kigamboni, alisistiza kuwa ni lazima kujengwa na kwamba kwa wakazi watakaotaka na wasiotaka wataondoka kwa hiari yao.

“Tunataka pembezoni mwa miji kuwe na miji iliyojengwa kisasa zaidi na kwa kuanza tunaanza na Kigamboni ambapo wakazi wa eneo hilo wasiwe na shaka fedha zao za fidia zipo na watalipwa,” alisema Kikwete.

“Hili daraja na barabara ambazo nasimamia vitabeba watu wa vyama vyote CCM, CUF, CHADEMA, TLP na wasio na vyama na wasiposhukuru au wakishukuru shauri yao lakini maendeleo yanafanyika na watu wanaona hata kama wanajifanya hawaoni,” alisema Kikwete.

Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliendeleza vijembe hivyo kwa wapinzani akisema hiyo ni hatua nzuri ambapo kwa sasa madaraja 4,880 makubwa yalijengwa likiwemo la Mkapa, Umoja na Malagarasi.

Aliyataja madaraja mengine kuwa ni pamoja na la Kilombero ambayo yote kwa pamoja alisema yatasaidia kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi wa nchi mara baada ya kukamilika.

Kuhusu daraja hilo la Kigamboni, Magufuli alisema kuwa wanataka uzinduzi ufanywe na Rais Kikwete ili Rais mwingine ajaye asije kujivunia mafanikio hayo awe ametoka CCM au upinzani kwani fedha za ujenzi zimetafutwa na serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo alisema wamefanya mazungumzo na mkandarasi ambapo wameahidi kumaliza ujenzi huo katika kipindi cha miaka miwili na nusu ambapo litakuwa na njia sita.

Magufuli aliwaacha hoi maelfu ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo pale alipomuomba Rais Jakaya Kikwete, kumpa nishani maalumu Mkurugenzi wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, kwa kutambua juhudi zake katika mchakato huo wa ujenzi wa daraja hilo.

“Badala ya kuwavalisha nishani wanajeshi pekee, unatakiwa kufanya hivyo pia kwa Mkurugenzi wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, kutokana na mchango wake mkubwa wa shirika hilo kwa jamii mbalimbali,” alisema Magufuli.

Naye, Dk. Dau alisema kuwa daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 680, na kwamba NSSF kwa kutambua umuhimu wa wananchi hasa katika suala zima la kukuza uchumi wa nchi ndiyo sababu ya wao kuamua kuchangia gharama za ujenzi huo

Source: Tanzania Daima, 21 Sept. 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO