Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

IKULU YATHIBITISHA KUPOKEA BARUA YA CHADEMA, YADAI INASUBIRIA KAMATI YA NCHIMBI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi

Ikulu imethibitisha kupokea barua ambayo iliandikwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, kikimuomba kuunda tume huru ya kimahakama kwa lengo la kuchunguza vifo vyenye utata vinavyotokea kwenye mikutano ya kisiasa na maandamano.

Barua hiyo ya Chadema kwenda kwa Rais Kikwete iliandikwa Septemba 10, mwaka huu na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, aliiambia NIPASHE jana mjini Dodoma kuwa, barua hiyo ilipokelewa, lakini itafanyiwa kazi baada ya kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, itakapomaliza kazi yake.

Rweyemamu alisema kuwa haiwezekani kuundwa kwa tume na kufanya kazi wakati mmoja na kamati ambayo inafanya kazi ya uchunguzi.

Kamati ya serikali iliundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Septemba 4, mwaka huu kuchunguza chanzo cha mauaji ya Mwangosi aliyeuawa kwa bomu wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, mkoa wa Iringa Septemba 2, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza kamati hiyo, Waziri Nchimbi alisema nia ni kupata matokeo yasiyoegemea upande wowote kwa kuwa kamati iliyoundwa ni huru.

Kamati hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, huku wajumbe wakiwa ni Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye pia ni Mahariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL); Pili Mtambalike, Ofisa Mipango kutoka Baraza la Habari (MCT); mtaalamu wa milipuko kutoka JWTZ, Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu.

Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita na itafanyakazi kwa siku 30 kuanzia terehe hiyo.

Hadidu za rejea ni kuchunguza chanzo cha kifo cha Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya waandishi wa Iringa na Polisi; kama kuna orodha ya waandishi watatu waliopangwa kushughulikiwa na polisi mkoani humo; kama kuna taratibu za kukata rufaa ya vyama vya siasa dhidi ya polisi pindi mikutano yao inapozuiwa;  je, kuna tatizo la mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa kwa ujumla wake na kama ukubwa wa nguvu zilizotumika katika tukio la Iringa ni sahihi.

Chadema katika barua hiyo pia kilimuomba Rais Kikwete kuchukua hatua ya kuwafukuza kazi viongozi waandamizi wa serikali na Jeshi la Polisi.

Aidha, Chadema, kilimuomba Rais Kikwete achukue hatua ya kuwafukuza kazi viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na ongezeko la mauaji hayo wauaji wakituhumiwa kuwa ni Jeshi la Polisi.

Chama hicho kinapendekeza kuwa Dk. Nchimbi afukuzwe kazi pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema.

Viongozi wengine ambao chama hicho kinapendekeza wafukuzwe ni  Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja; Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

Mbowe katika barua yake aliwataka wanachama na viongozi wakati Chadema  kikisubiri majibu ya barua hiyo kutoka kwa Rais wasitoe ushirikiano kwa kamati  iliyoundwa na Dk. Nchimbi kuchunguza mauaji Mwangosi na matukio mengine ambayo zimeundwa kamati za kuchunguza vifo hivyo vyenye utata.

Katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu watu kadhaa walifariki kwenye matukio ya kisiasa yaliyotokea Arusha, Igunga, Arumeru Mashariki, Iramba, Morogoro na Iringa.

MLOLONGO WA MAUAJI

Chama hicho kimeorodhesha matukio ya mauaji yaliyotokea mwaka jana na mwaka huu katika harakati za kisiasa kuwa ni pamoja na lile la Januari 5, mwaka jana ambalo watu watatu waliuawa jijini Arusha na polisi wakati wa kuvunja maandamano ya wanachama na wapenzi wa Chadema ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa umeya wa Jiji hilo.

Wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, mwanachama wa Chadema, Mbwana Masoud, aliuawa kwa kunyongwa katika mazingira ya kutatanisha. 

Kiongozi wa kata wa Chadema, Msafiri Mbwambo, alichinjwa na chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kusababishwa na masuala ya kisiasa baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Julai 15, mwaka huu mkoani Singida, katika Jimbo la Iramba Magharibi, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30), aliuawa katika vurugu baina ya CCM na Chadema baada ya kumalizika kwa mkutano wa Chadema. 

Mjini Morogoro, Agosti 27, mwaka huu  polisi walimuua kwa risasi, Ally Zona wakati wakivunja maandamano ya Chadema kabla ya kufanyika kwa mkutano wa hadhara.

Chanzo: Nipashe, kupitia Rundugai Blog

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO