Shauri lililofunguliwa na aliekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaaa nchini kupinga kuenguliwa kwake kuwa mbunge limeahirishwa hadi tarehe 2 mwezi ujao litakaposikilizwa tena.
Mapema asubuhi ya leo mamia ya wafuasi wa Chadema walijitokeza katika eneo la Mahakama Kuu kusikiliza rufaa hiyo ambayo ilisikilizwa kwa muda mrefu kiasi kabla ya kuahirishwa.
Taarifa za awali kutoka mahakamani hapo kabla ya kusikilizwa kwa shauri hilo hii leo zilieleza kuwa tayari mawakili wa pande zote mbili walishaandika barua ya kuomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo hadi Oktoba 2, mwaka huu, kufuatia mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na kaka yake, Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji, kufiwa na baba yao mzazi.
Imeelezwa kuwa, upande wa walalamikaji wameweka mapingamizi fulani ambayo jopo la majaji litayapitia hiyo tarehe 2 oktoba. Taarifa nyingine ambayo haijaweza kuthibitishwa na Blog hii zinaeleza kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa hukumu ya rufaa hii kusomwa Dar es Salaam.
Godbless Lema wakati akiwasili viwanja vya Mahakama Kuu Arusha kusikiliza rufaa yake mapema leo asubuhi
***********
Rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande na wenzake, Natalia Kimaro na Salum Massati.
Wakili Mughwai anashirikiana na wakili Modest Akida kuwawakilisha wadaiwa kwenye shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo, waliofungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa wakati wa kampeni alimdhalilisha mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian kwa kutumia lugha za matusi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na Lissu, aliwasilisha kwenye mahakama hiyo hoja 18 za madai akipinga kutenguliwa kwa ubunge wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Kwenye baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotengua ubunge wake, huku akiitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na zile za kesi iliyomalizika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Lema anadai kuwa jaji alikosea wakati alipoamua kuwa mpiga kura yeyote anaruhusiwa kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki zake za msingi hazijaguswa.
Shauri hilo lililikuwa likisubiriwa kwa hamu na wakazi wengi wa Jiji la Arusha na Watanzania wengi lilitarajiwa kusikilizwa kwa siku moja kisha kupangiwa tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Maelezo ya ziada na Grace Macha wa Tanzania Daima
1 maoni:
Mh! mungu yopo!kama kunauonevu wowote
Post a Comment