MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana aliongoza matembezi ya hisani katika jiji la Dar es Salaam. Matembezi hayo yalilenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendeshea Operesheni ya chama hicho ya Dira ya Mabadiliko (V4C).
Mamia ya wananchi walijitokeza katika matembezi hayo, ambapo jumla ya Sh milioni 129.2 zilichangwa, huku Sh milioni 325 zikitajwa kama ahadi.
Viongozi wengine waliohudhuria matembezi hayo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Machano Khamis Ally na Naibu Katibu Mkuu (bara), Julius Mtatiro.
Matembezi hayo yalianzia katika makao makuu ya chama hicho, Buguruni Rozana na kupita maeneo ya Mchikichini, Kariakoo, Barabara ya Morogoro na kuishia Jangwani.
Katika harambee hiyo, Profesa Lipumba alichangia Sh 110, 000 na kufuatiwa na viongozi wengine wa chama hicho na baadaye wanachama wakafuata.
Katika mkutano huo Profesa Lipumba alisema, fedha hizo zitaanza kutumika katika kuendesha operesheni hiyo inayoanza kesho katika jiji la Arusha.
Profesa Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma, alisema Tanzania hivi sasa ipo njia panda kutokana na kukosa viongozi wazalendo wenye uchungu na rasilimali za nchi.
Alisema uongozi wa CCM sasa umefika mwisho ndiyo maana Serikali ya chama hicho haina dhamira ya kuwakomboa wananchi na kuwatoa katika lindi la umasikini.
“Kwanza nawashukuru kwa kujitokeza katika matembezi na kuchangia CUF, ili kuendesha operesheni za V4C nchi nzima.
“Naomba niwatoe hofu kwamba, fedha zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na zitakaguliwa na mtaalamu wetu kila mwezi.
“Tunakwenda kuvunja ngome ya Chadema inayosifiwa, Arusha ni jiji linalohitaji utulivu wa kisiasa kwa kuwa ni kivutio cha wawekezaji.
“Tunawaomba wananchi kutupokea kwa mikono miwili, ili kuwatoa tongotogo wanazopakwa na vyama vingine.
“Tanzania ilipofikia tunapaswa kuchangiana wananchi sisi wenyewe sio kufadhiliwa na wageni au matajiri, kwani tutarudi katika hali ya ukoloni wa kutumikishwa.
“Fedha hizi zitatumika kueneza sera ya CUF, kutoa elimu kwa wananchi juu ya CCM ilivyoshindwa kuwakomboa miaka 50 ya uhuru, sasa operesheni hii itawaandaa wananchi kukichagua CUF 2015 na kushika dola,” alisema.
MTATIRO
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Bara), Julius Mtatiro, alisema chama chake hakina mpango wa kupokea michango kutoka kwa wafadhili kwa kuogopa kutumikishwa.
Mtatiro alisema, chama chake hakipo tayari kupokea misaada ya aina hiyo na kutolea mfano wa misaada inayotolewa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Sabodo.
Mtatiro alisema anashangazwa na kitendo cha tajiri huyo kutoa msaada kwa CCM, ili chama hicho kiendelee kubaki madarakani, wakati huo huo akiisaidia Chadema ili kiweze kuiondoa CCM madarakani.
Alisema CUF haiwezi kupokea fedha kutoka kwa matajiri wa aina hiyo ili kuepuka kutumikishwa hapo baadaye na kuongeza kwamba, chama hicho kitaendeshwa kwa nguvu ya wanachama hadi hapo kitaposhika dola.
“Jamani kazi ya ukombozi ni ngumu, inahitaji maandalizi makubwa sana na CUF imekuwa ikishindwa katika uchaguzi unaofanyika kwa sababu ya kukosa fedha tofauti na CCM wananvyotumia mabilioni katika chaguzi.
“CUF inaambulia Sh milioni 1 za ruzuku ambazo hutumika bara na visiwani, sasa kiasi hicho huwezi kusema ununue gari, kofia, fulana na kuwalipa posho wanachama.
“Hivyo CUF imekuja kwenu muichangie kama ilivyokuwa kwa baba wetu, marehemu Julius Nyerere alivyochangiwa na wazee kutafuta uhuru.
“Mchango huu uwe mwanzo wa kuchangia harambee nyingine zijazo, ili kuhakikisha tunafika vijiji, kata, wilaya na mikoa yote ya Tanzania kupitia V4C, ili kuwaandaa wananchi kukiweka CUF Ikulu kwa kauli ya ‘Mchakamchaka hadi kieleweke 2015,” alisema.
ABDUL KAMBAYA
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya, alimshambulia Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kwamba, katika uongozi wake alitumia vibaya fedha za walipakodi.
Alisema ni Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Mkapa, ndiyo iliyosaini mikataba mibovu iliyofanya wananchi kushindwa kunufaika na rasilimali za taifa.
“Kati ya uongozi mbovu ulioanza kuharibu mwelekeo wa taifa ni awamu ya tatu, awamu hiyo ndio iliyoongoza kutumia fedha hovyo kwa kununua rada mbovu, ndege kubwa ambayo haitumiwi na mtu hivi sasa na kusaini mikataba mibovu.
“Hali hii imesababisha uongozi uliofuata kukosa namna ya kutatua matatizo ya wananchi, lakini cha ajabu katika miaka 10 ya Mkapa, CHADEMA haikuthubutu kusema chochote kama inavyosema sasa hawa walikuwa kitu kimoja, lakini cha ajabu wanatusema tumefunga ndoa na CCM,” alisema.
Pamoja na mambo mengine matembezi hayo yalitawaliwa na mambo mbalimbali, yaliyokuwa na ujumbe wa kuwahamasisha wananchi kuchangia CUF na kuepuka ufadhili wa matajiri na watu kutoka nje ya nchi.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka hivi: “CUF makabwela haina Saboda changia chama chako”.
“Wanawake tupo kifua mbele kuchangia chama, mkombozi wa nchi hii ni makabwela changia chama, tofauti ya makabwela na mabepari tazama maisha yetu,” liliandika bango jingine
Source: Mtanzania 17 September, 2012
0 maoni:
Post a Comment