MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akihutubia mkutano huo jana, Profesa Lipumba, alianza kwa kulaani tukio la mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi, kisha akasema kwa sasa nchi iko njia panda kutokana na hali ngumu ya maisha, huku kundi kubwa la vijana likiwa limepoteza matumaini.
Alisema ukosefu wa ajira kwa vijana hapa nchini ni sawa na bomu ambalo wakati wowote linaweza kulipuka kutokana na mfumo mbovu uliopo.
Alisema haki sawa si kauli mbiu isiyo kuwa na mashiko bali ni haki sawa ya namna rasilimali za nchi zitakavyoweza kuwanufaisha Watanzania wote.
Alisema lazima wahakikishe watu wanapata ujira kwa kazi wanayoifanya, kwa kuwa haki za jamii ni huduma za msingi endapo wauguzi, madaktari na walimu watathamiwa.
“Nchi yetu ina bahati ya kuwa na rasilimali nyingi kama maziwa makubwa, bahari, dhahabu, almasi na vitu vingine na sasa tumevumbua gesi, katika hili tuna matumani makubwa ya kuwa wa pili kwa utajiri duniani.
“Lakini katika hili watu wachache wanatumia utajiri wa nchi hii, hivyo tunapopata hiyo gesi ni muhimu tukaweka utaratibu ili wananchi wote waweze kunufaika nayo, tuweke utaratibu wa kuiwajibisha Serikali iliyopo madarakani.
“Watafiti wamebaini njia nyepesi ya kuondoa umasikini ni kuwakabidhi wananchi fedha kwa kuwa kufanya hivyo akina mama watatumia njia hiyo kuwalisha watoto wao, nchi nyingi za wenzetu wanatumia utaratibu huo,” alisema Profesa Lipumba.
Katika mkutano huo ulio dumu kwa saa mbili, alisema kupanda kwa bidhaa kumetokana na kubadilika kwa uchumi kwa kuwa nchi kubwa zimeweza kuongeza uchumi wake.
Alisema ripoti ya ushindani wa kiuchumi unaonyesha katika nchi 144 Tanzania imekuwa ya 120 wakati Rwanda ya 63.
Alisema katika ripoti hiyo suala la ubora wa miundombinu Tanzania imeshika nafasi ya 137 huku katika uwekezaji katika elimu ikishika nafasi ya 132 kati ya nchi 144.
Aidha, alizindua rasmi operesheni ya chama hicho ijulikanayo kama Vision For Change (V4C) itakayofanyika Mikoa ya Arusha, Bukoba na mikoa mingine itakayotolewa taarifa zake siku zijazo.
Alisema Septemba 16, mwaka huu, kutakuwa na matembezi ya hisani kutoka Buguruni Rozana hadi Viwanja vya Jangwani, kwa ajili ya kuchangisha fedha kuendesha chama hicho.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Julius Mtatiro, alisema kwa sasa wanataka kuhakikisha haki ya Watanzania inapatikana kwa kuwa nchi imegubikwa na viongozi wezi kuanzia askari mgambo, wilayani hadi mikoani.
Alisema vyama vingine vimejaa ujanja ujanja na watu kutumia nguvu badala ya kuwatetea wananchi kwa kuwahakikishia maisha bora na huduma nzuri za kijamii ambazo wananchi wanazikosa.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Hamis Ally, amewaomba Waislamu wote kujiunga na chama hicho kwa kuwa vyama vingeni vinasema ni cha Waislamu.
“Imeelezwa kuwa CCM na CHADEMA wanasema CUF ni chama cha Waislamu basi kama ni hivyo Waislamu wote waingie CUF kwa kuwa vyama vingine hawawataki nyie,” alisema Ally
Imeachapishwa Jumatatu, Septemba 10, 2012 na Gazeti Mtanzania
0 maoni:
Post a Comment