Nilipoanza kazi, Polisi hawakuwa wakipiga watu hovyo, tena hadharani - Jaji Mihayo
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema Taifa ambalo maisha ya wananchi wake wanapotea bila sababu, lina matatizo kwani hata Katiba ya nchi lengo lake kuu ni kulinda uhai wa watu na sio kuua.
Akizungumza kwenye kipindi cha Jenerali on Monday kinachorushwa na televisheni ya Channel TEN, kila Jumatatu usiku, Jaji Mihayo alisema yapo matukio mengi ya mauaji ya raia wasio na hatia yanayoihusisha Polisi na kushangaa hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao, “Kuna haja ya kubadilisha jina la Jeshi la Polisi, kutoka neno jeshi na kuwa chombo cha Usalama wa Raia, kwani neno hili halijakaa kirafiki, na ndio maana hata wanapokwenda kukamata raia wanawapiga bila hata sababu, kwa nini? alihoji Jaji Mihayo.
Akifafanua kauli yake kuhusu taifa ambalo maisha ya raia wake yanapotea bila sababu halina haja ya kuwepo, Jaji Mihayo alisema, uhai ni haki ya msingi ya raia yeyote na kwamba hata Katiba ya nchi msingi wake mkubwa ni kujali utu na kwamba kukatiza uhai wa mtu ni kosa na linahitaji adhabu, “Nilipoanza kazi mahakamani miaka mingi iliyopita, polisi hawakuwa wakipiga watu ovyo tena hadharani, hata kama walifanya hivyo walifanya kwa siri na walijitahidi wasionekane wakipiga, lakini sasa kipigo kwa raia kinafanywa wazi na polisi,” alisema Jaji Mihayo.
Alisema matukio mengi ya kunyanyasa raia bila sababu yamekuwa yakifanywa na Polisi na hakuna aliyewawajibisha, jambo ambalo amewashangaa hata wanasheria nchini kwa kutochukua hatua ya kuwafungulia mashtaka polisi hao, kwani mwanasheria mzuri ni yule anayezungumzia jambo mahakamani na sio kutoa matamko.
Jaji Mihayo aliongeza, kutochukuliwa hatua kwa polisi hao kumewapa kiburi kujiona wako juu ya sheria na kwamba pamoja na hayo upo umuhimu wa polisi hao kufundishwa sheria ili wazifahamu na kutofanya maamuzi ya kinyama, “Haiwezekani kutoka maeneo mbalimbali kama vile Singida, Arusha, Morogoro na Iringa polisi kote iseme hawajakosea, kwenye mauaji ya raia wasio na hatia, hii sio sahihi hata kidogo, kwani polisi wanahusika,” alisema Jaji Mihayo.
via gazeti la HabariLeo
Ziro ana uhakika kuwa Jehanamu ipo Duniani, tena ni nchini India
Jibu la Waziri Nchimbi kuhusu ujumbe wa simu wa mauaji kwa IGP kutoka kwa Dkt. Slaa
Katika mazungumzo yake, Dkt. Nchimbi alimlaumu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa kuwa ni mmoja wa watu waliosababisha mauaji hayo kwani Septemba Mosi, siku moja kabla ya mauaji hayo, alimwandikia IGP ujumbe unaoonesha kuwa walidhamiria kufanya vurugu.
Alinukuu ujumbe huo unaodaiwa kuandikwa na Dk Slaa; “IGP nasubiri simu yako, wajulishe polisi wako waandae risasi za kutosha na mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha mtasherehekea, mjiandae kwenda Mahakama ya The Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya, Dk Slaa.”
Waziri huyo alisema anamshangaa IGP Mwema kwa nini Polisi hawajamkamata Dkt. Slaa na kumhoji kwani ujumbe wake aliotuma unaashiria kutaka kuanzisha vurugu kama ilivyotokea huko Nyololo.
---
Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la HabariLeo
Majibu 4 ya Waziri Nchimbi alipoulizwa maswali kadhaa kuhusu msiba wa Mwangosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipoulizwa:
Kama yuko tayari kumsimamisha kazi Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda ili kupisha uchunguzi huo alisema ndani ya tume hiyo kuna Naibu Kamishna wa Polisi; hivyo kamanda huyo ambaye cheo chake ni Kamishna Msaidizi hana ubavu wa kuharibu uchunguzi huo.
Kuhusu askari aliyempiga bomu Mwangosi kama anashikiliwa na Polisi au bado yuko nje, alisema atachukua hatua mara baada ya tume hiyo au ile ya Polisi, iliyoundwa na Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema kukamilisha uchunguzi wake.
Kuhusu kama atajiuzulu iwapo ripoti itabaini kuwa polisi ndio waliofanya mauaji hayo, alisema “Nikijiuzulu mtampata wapi Waziri kama mimi? (kicheko) Shauri yenu… lakini nawahakikishieni kuwa ukweli utaanikwa wazi.”
Kwamba Polisi wanatumiwa kukikandamiza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kwa manufaa ya CCM, alisema hataruhusu hali ya namna hiyo na akasisitiza kuwa Polisi wamekuwa wanatekeleza agizo la Msajili wa Vyama vya Siasa la kupiga marufuku mikutano ya kisiasa katika kipindi hiki cha Sensa ya Watu na Makazi.
Alipotolewa mifano ya namna ambavyo wanachama wa CCM wamekuwa wakifanya mikutano yake bila kuingiliwa na Polisi, Dkt. Nchimbi alisema alipata taarifa hizo na akamjulisha Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye alimhakikishia kuwa hakuna mkutano wa hadhara unaofanywa na chama chake badala yake wanafanya vikao vya ndani, “Mikutano ya ndani haikupigwa marufuku, kilichokatazwa ni mikutano ya hadhara na ninaomba wenzetu wawe wastahimilivu kwani zimebaki siku nne tu za sensa.”
---
Majibu yamenukuliwa kutoka kwenye gazeti la HabariLeo
Walioteulizwa na Waziri kuunda Tume ya Kuchunguza mauaji ya Daudi Mwangosi
Majina ya walioteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi ili kuunda Tume Huru ya kuchunguza mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi ni pamoja na:
- Jaji Mstaafu Stephen Iihema - Mwenyekiti na Kiongozi wa Tume hii
- Theophil Makunga (Tanzania Editors Forum (TEF))
- Pili Mtambalike (Media Council of Tanzania (MCT))
- Kanali Wema Wapo (JWTZ)
- Isaya Mangulu, Mtaalamu wa Mabomu ambaye ni Naibu Kamishina
Tume hiyo imetakiwa, ndani ya siku 30, kupata taarifa zenye majawabu ya maswali 6 ambayo yanawatatiza Wananchi.
Waziri akayataja maswali hayo kuwa ni:
- Kipini chanzo cha mauaji ya Mwangosi
- Kama kuna ukweli kuwa kuna uhasama kati ya polisi wa Iringa na waandishi wa habari wa mkoani humo
- Kama ni kweli kuna waandishi watatu wa mkoani Iringa ambao wako kwenye orodha ya kuuawa na polisi
- Kama nguvu iliyotumiwa na polisi Nyololo ilikuwa sahihi
- Kama kuna utaratibu kwa vyama vya siasa kukata rufaa kama haviridhiki na uamuzi wa Polisi
- Kama kuna uhusiano mbaya kati ya polisi na baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini
Waziri amesema, iwapo tume hiyo itahitaji msaada wa kitaalamu kutoka nje ya nchi, Serikali iko tayari kuagiza wataalamu hao, ili waisaidie ili wapate majibu yenye taarifa zinazojitosheleza na kuridhisha
0 maoni:
Post a Comment