Taswira halisi ya marehemu Daudi Mwangosi, aliekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoani Iringa na ripota wa kituo cha televisheni cha Channel 10 kwa mkoa Iringa hadi siku anafariki.
--------
Ushuhuda uliotolewa na waandishi wa habari wawili waliokuwa wanahojiwa na mtangazaji wa kipindi cha Morning Jam cha Capital Radio ya Jijini Dar es Salaam (majina yanahifadhiwa), umeeleza kuwa marehemu alipigwa sana na askari takribani 8 kwa kutumia marungu, ngumi, mateke, vitako na mitutu ya bunduki kabla ya umauti kumfika kwa kulipuliwa na bomu.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda hao ambao walikuwepo eneo la tukio na kushuhudia kipigo cha Polisi kwa Daudi Mwangosi na baadae kulipuliwa na bomu, wahusika wakuu wa kifo cha mwandishi huyo ni Jeshi la Polisi na RPC wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alikuwa anajua na kushuhudia pia.
Awali RPC Kamuhanda akielezea tukio hilo alisema marehemu alikuwa anakimbizwa na wafuasi wa CHADEMA kwa mawe na hivyo kukimbilia kwa Polisi kuomba msaada na baadae ukatokea mlipuko ambao hawajui chanzo chake, maelezo ambayo yanakinzana na simulizi za mashuhuda ambao nao pia walidhurika.
Hapa marehemu Daudi Mwangosi kulia anaonekana akiwa kazini akipiga picha kukusanya matukio tofauti muda mchache kabla ya kulipuliwa hadi kufa.
Katika simulizi za mashuhuda hao kupitia redio hiyo, wanasema marehemu Mwangosi alikuwa anafanya kazi yake kama mwandishi na hakuwamo katika msafara wa CHADEMA na alifika eno lile yeye binafsi kwa kutumia usafiri wa basi.
Hapa ni marehemu akihojiana na RPC Kamuhanda ambapo inaelezwa walishindwa kuelewana. Muda mfupi baadae ndio kadhia ya kupigwa ikamkuta Mwangosi na hatimae kufariki kwa mlipuko.
Mashuhuda wakasimulia kuwa chanzo cha Mwangosi kupigwa hadi kufa ni kitendo cha yeye kwenda kumsaidia mwandishi mwingine wa Nipashe aliekuwa anapata kipigo. Mwangosi aliwafuata polisi kuhoji kwanini wanampiga mwandishi Mushi wa Nipashe Godfrey Mushi na ndipo na yeye akaanza kutembezewa mkong’oto.
Shuhuda mmoja akasema, alipomuona Mwangosi anapigwa sana akaenda kwenye gari ya RPC kumuomba asaidie kwa kumfahamisha kuwa anaepigwa ni mwandihsi wa habari. Ikaelezwa kuwa RPC Kamuhanda akshusha kioo cha gari, akamuangalia kwa dharau na kisha kukipandisha tena. Hakutoa msaada wowote.
Mashuhuda hao wakasema walikitafsiri kitendo hicho cha RPC kukataa kumsaidia mwandishi asipigwe kinashiria kuwa alibariki tukio hilo.
Msimuliaji akadai kuwa, baada ya kukosa msaada wa RPC alirudi kuendelea na kupiga picha matukio huku Mwangosi anaendelea kupigwa tu hadi kuzidiwa nguvu.
Hapa marehemu Mwangosi anaonekana yuko chini ya miguu ya OCS alieingilia kati kumsaidia. Naye Mwangosi amemkumbatia kujiokoa na kipigo. Picha hii ikitazwmwa vizuri inaonesha mtu alievaa kiraia amenyanyua juu bastola na kidole kiko kwenye trigger tayari kwa lolote. Pia askari wa mwanzo kushoto anaonekana ameelekeza mtutu wa bunduki tumboni kwa marehemu Mwangosi ambae amemkumbatia OCS kujiokoa nae akielekea kuanguka.
Hapa anaonekana OCS alieingilia kati kumuokaoa akiugulia maumivu ya mguu wake baada ya yeye pia kujeruhiwa katika mlipuko huo.Pembeni yake unaelezwa kuwa mwili wa marehemu ukiwa vipande vipande.
Hapa askari OCS aliejeruhiwa akiondolewa na askari wenzake baada ya kujeruhiwa miguu.
Baadae akatokea OCS akaingia katikati ya maaaskari hao waliokuwa wanampiga Mwangosi ili kumuokoa. Daudi akajificha chini ya miguu ya OCS huyo huku miguu amemkumbatia katika hali ya kuishiwa nguvu.
Akiwa katika hali hiyo akatokea askari ameshika batola ameielekeza juu, akiwa amevaa kiraia na askari mwingine akamuwekea mtutu wa bunduki tumboni kwa Mwangosi kama picha ya kwanza inavyoonesha hapo juu.
Shuhuda anasimulia kuwa kilichofuata baada ya hapo ni kishindo kikubwa. Mwangosi akawa tayari ni marehemu huku utumbo na nyama vikizagaa chini. Yule OCS aliekuwa anamuokoa Mwangosi nae akaumizwa vibaya mguu wake.
RPC Michael Kamuhanda ambae chini ya uongozi wake pia raia wanne wasio na hatia waliuwawa Mkoani Ruvuma (Songea) maema mwaka huu. (Picha zote kutoka vyanzo mbali mbali vya habari)
Mashuhuda hao hawajaweza kujua ni kitu gani au bomu la aina gani hasa lililomlipua Mwangosi kiasi chakuchana chana vipande mwili wake.
"Gari ya Kamanda wa Polisi ilikuwa kama mita tano kutoka alipokuwa anapigwa mwandishi, nilienda na kumgongea alishusha kioo, nilimwambia Afande yule anayepigwa ni mwandishi wa habari nikamtajia hadi na jina, akaniangalia kwa dharau akapandisha kioo …….nikasikia mshindo mkubwa kutoka pale alipokuwa anapigwa mwenzetu, nikaona wale polisi wametawanyika lakini vipande vya nyama vya mwenzetu na polisi mmoja ambaye alikuwa ni OCS wa kituo cha Mafinga akiwa chini..” alisema shuhuda mmoja.
Hapo awali ilielezwa kuwa dakika chache kabla ya Mwangosi kulipuliwa, alikuwa na mahojiano na RPC Kamuhanda eneo la tukio na hawakuweza kuelewana. Inaelezwa kuwa Mwangosi alikuwa anahoji kwanini wafuasi wa CHADEMA walikuwa wnapigwa mabomu mbele ya ofisi yao, na pia kujua msimamo wa Jeshi la Polisi juu ya katazo la mikutano ya kisiasa wakati wa sensa, na RPC Kamuhanda akamjibu Mwangosi kuwa anauliza hayo yeye kama nani!
Aidha kuna tetesi ambazo hazijathibitishwa (si sehemu ya ushuhuda huo) kuwa kulikuwa na mkakati wa kuhakikisha wanawafundisha adabu waandishi watatu akiwemo marehemu, Francis Godwin (mwandishi wa kujitegemea) na Godfrey Mushi wa Nipashe.
Dr Slaa kutoa tamko leo
Nae Katibu Mkuu wa CHADEMA akihojiwa katika kipindi hicho ameeleza kuwa baadae hii leo atazungumza na waandishi wa habari kuelezea mambo mbalimbali kuhusiana na tukio zima la kuuwawa kwa mwandishi huyo wa habari.
Alisema kwasasa wanasaidiana na ndugu wa marehemu na wahusika wengine kufanikisha maziko ya mwiili wa marehemu kwasababu hauwezi kukaa sana kwa jinsi ulivyoharibika.
0 maoni:
Post a Comment