Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Muuaji wa Mwangosi huyu hapa

ASKARI polisi aliyefyatu bomu lililomlipua na kumuua kinyama mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi (40), amejulikana.
Tayari mazishi ya masalia ya mwili wa Mwangosi yamefanyika jana katika Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, huku ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari polisi waliosababisha kifo hicho na jina baya la jeshi hilo.
Picha zilizopigwa kwenye tukio la mauaji hayo, zinaonyesha askari wakiwa wamemzingira na kumpiga Mwangosi, baadhi yao wakiwa na virungu, na wengine bastola. Mmoja miongoni mwao, ameshikilia bunduki na kuielekeza tumboni.Nyololo masacre 6
Vile vile, baadhi ya askari wamemtaja mwenzao aliyemlipua Mwangosi, wakataja na mahali anakoishi mjini Iringa. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, polisi ilikuwa haijasema wazi kama imemtia mbaroni yeye na wenzake, huku wizara na jeshi hilo zikiunda tume za kuchunguza “chanzo” cha tukio hilo!
Baadhi ya askari waliokuwepo siku ya tukio, walilieleza gazeti hili jana kwa sharti la kutotaja majina yao kwamba askari aliyemlipua Mwangosi na kumuua papo hapo yuko chini ya ulinzi tangu siku ya tukio pamoja na askari wengine walioonekana wakimpiga mwandishi huyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda, alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo, alisema hana taarifa za askari yeyote kushikiliwa na kuhojiwa kwa tukio hilo.
Kutoka mazikoni, habari zinasema kuwa haikuwa kazi ndogo kuzuia vilio na simanzi zilizoonyeshwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliofika kushuhudia mwili wa marehemu Mwangosi ulioharibiwa vibaya ukionyeshwa baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Busoka, Mathayo Mwantemanie kuongoza ibada ya mazishi.
Kifo cha mwandishi huyo ambacho kimevuta hisia za wananchi wengi ndani na nje ya nchi, hususani wakazi wa Wilaya ya Rungwe, kilimgusa kila mmoja akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya na mkewe, Lucy Mwandosya waliofika nyumbani kwa marehemu.
Profesa Mwandosya alieleza jinsi msiba wa Mwangosi ulivyomgusa, kumuumiza moyo na kumfanya ashindwe kujizuia kutoa machozi kwani tayari alishapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita.
“Ni vigumu sana kwangu kuzungumzia hali hii, Mwangosi ameniuma sana, nimezunguka naye sana, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, nimepotelewa na kijana wangu, mtoto wangu, mwenzangu katika kazi, kila nilipokuwa naye alinipiga sana maswali na mengi yalikuwa ya msingi,” alisema Profesa Mwandosya.
Kwa upande wake, Dk. Slaa ambaye alikuwa kwenye msafara wa kusafirisha mwili wa marehemu, alieleza mazingira ya kifo hicho na kusema msiba hauna itikadi, dini wala rangi, na kubeza kauli za ubaguzi dhidi ya msiba wa mwanahabari huyo.
Alisema CHADEMA itahakikisha haki ya Mwangosi haipotei na kuongeza kuwa binadamu si kuku, kwani damu yake lazima ipiganiwe kwa haki na kueleza jinsi chama hicho kinavyoshtushwa na vitendo vinavyofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya habari, hususani kulifungia gazeti la MwanaHALISI na sasa wameamua kupoteza maisha ya mwanahabari huyo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, Dk. Steven Kimondo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Idara ya Thiolojia, aliuliza umati huo baada ya kusema kuwa Jeshi la Polisi linahusika na mauaji ya Mwangosi.
“Akili yangu inakataa kusema uongo kuwa Jeshi la Polisi halihusiki na tukio la kifo hiki, vitendo hivi vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia vinajenga chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao na kwamba lazima uchunguzi ueleze ukweli kuwa marehemu hajafa kifo cha Mungu isipokuwa binadamu wamehusika,” alisema Dk. Kimondo.
Dk. Slaa alitoa ubani wa sh milioni 2, Mbeya Press Club (sh 700,000), Iringa Press Club (sh 1,750,000), MISA-Tan (sh 500,000), huku Profesa Mwandosya akiahidi kumsomesha mtoto mkubwa wa marehemu ambaye yupo kidato cha nne na wadogo zake, na alitoa ubani wa sh 500,000.
Waziri Nchimbi aunda tume huru
Katika hatua nyingine, serikali imeunda tume huru ya watu watano wa kada tofauti akiwemo mtaalamu wa milipuko kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Licha ya kuwepo kwa tume nyingine iliyoundwa na Jeshi la Polisi chini ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, tume ya serikali itafanya kazi kwa siku 30 na imepewa hadidu sita za rejea.
Mwangosi aliuawa Septemba 2 mwaka huu kwa kitu kinachoaminika kuwa ni bomu lililoelekezwa kwake na askari polisi waliokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye ufunguzi wa tawi katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi, mkoani Iringa.
Akitangaza kuundwa kwa tume hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwaeleza waandishi wa habari aliokutana nao ofisini kwake jana kwamba hakuna askari atakayenusurika iwapo itathibitika kuwa alishiriki kwenye mauaji hayo.
Dk. Nchimbi ambaye muda mwingi wa mazungumzo hayo alijinasibu kuwa muumini mzuri wa utawala wa sheria, aliwataja wajumbe wa tume hiyo kuwa ni wanahabari Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication inayochapisha magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti.
Wengine ni Kanali Wema W. Wapo ambaye ni mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Pivel Ihema.
“Tume hii itafanya kazi zake kwa uhuru na iwapo wataona wataalamu wa hapa ndani wameshindwa jambo fulani wasisite kutueleza… serikali itautafuta utaalamu huo kutoka nje ya nchi.
“Ninaomba kuwahakikishia Watanzania kwamba askari yeyote atakayeguswa na tume hii hatabaki salama, sikubaliani na dhuluma hasa ya vifo vya raia na sipuuzi malalamiko yao,” alisisitiza Dk. Nchimbi huku akikwepa kujibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa waziri huyo, hadidu hizo za rejea zimetokana na taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri ambayo ni kujua chanzo cha kifo cha Mwangosi, ukweli kuhusu uhasama kati ya polisi wa mkoani Iringa na waandishi wa huko.
Aliitaka pia tume hiyo kueleza iwapo kuna orodha ya waandishi wa habari watatu mkoani Iringa wanaowindwa na polisi, na usahihi wa nguvu ya polisi iliyotumika kuwadhibiti wafuasi wa CHADEMA.
Jukumu lingine la tume hiyo ni kueleza kwa kina utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa pale vinapohisi kutotendewa haki na kama kweli kuna uhusiano mbaya kati ya polisi na vyama vya siasa hasa wapinzani.
Kwa msisitizo Dk. Nchimbi alisema vurugu zilizofanyika Iringa ni matokeo ya kuongezwa kwa muda wa kazi ya sensa ya watu na makazi ambapo Jeshi la Polisi liliwazuia wanasiasa wote kufanya mikutano ya hadhara.
Hata hivyo, waziri huyo alishindwa kutoa ufafanuzi wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo huko Bububu visiwani Zanzibar ambapo Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilali, alishiriki.
Waziri huyo alisema serikali inajiuliza iwapo suala la sensa si muhimu kwa CHADEMA kiasi cha kushindwa kuvumilia kwa siku saba za nyongeza.
Katika hali inayoonyesha waziri kukosa hisia na kuguswa na ukatili wa jeshi lake, aliilaumu CHADEMA kwamba ndiyo iliyosababisha mauaji hayo.
“Hivi CHADEMA wanajisikiaje katika kipindi cha miezi mitatu kwenye mikutano yao mitatu wamesababisha vifo vya watu watatu, familia za marehemu hao zinawachukuliaje… unajua harakati za siasa hawakuanza wao, Mwalimu Nyerere aliutafuta uhuru wa nchi hii kwa miaka saba bila kumwaga damu (Tangu 1954 hadi 1961) tena akiwa na serikali ya kikoloni,” alisema.
Amshukia IGP Mwema, Dk. Slaa
Katika kile alichokiita kumshangaa IGP Mwema, Dk. Nchimbi alisema haelewi sababu za kiongozi huyo wa polisi kuendelea kumwacha huru Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, wakati ametoa vitisho vilivyosababisha mauaji ya mwandishi huyo.
Akizungumzia vitisho vya katibu huyo aliyewahi kugombea urais mwaka 2010, waziri huyo aliwaonyesha waandishi wa habari ujumbe mfupi wa simu ya mkononi aliotumiwa IGP Mwema kutoka kwa Dk. Slaa.
Ujumbe huo ulisomeka hivi: ‘IGP nasubiri simu yako wajulishe polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya The Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya. Dk. Slaa.’
Kutokana na ujumbe huo huku akizungumza kwa mafumbo, kauli ya Dk. Nchimbi ni kumtaka IGP kumkamata Dk. Slaa na kumfikisha mahakamani kwa madai ya kutoa vitisho na kusababisha mauaji.
“Namshangaa IGP Mwema mtu anatoa vitisho lakini hapelekwi mahakamani, mtu ametuma ujumbe kama huu halafu anarudi nyumbani kwake analala… anaendelea kuwa huru.
“Lakini zaidi namshangaa Dk. Slaa licha ya vitisho hivyo na kifo cha mwandishi, bado hajaenda kujisalimisha polisi,” alisema waziri huyo alipoulizwa hatua anazochukua baada ya IGP kukaa kimya licha ya ujumbe aliotumiwa na Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa waziri huyo wakiwa kwenye kikao Agosti 28 mwaka huu, IGP Mwema alitumia muda mwingi kumwomba Dk. Slaa asitishe mikutano ya hadhara kupisha shughuli za sensa jambo lililofikia muafaka kwa wawili hao.
“Nilimsikia IGP akiongea kwa upole… ‘nakuomba kaka yangu Slaa nielewe ndugu yangu nakuomba’ naamini waliafikiana,” alisema Dk. Nchimbi.
Akiendelea Nchimbi alisema; “Nikiwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia jeshi hili na kuona haki inatendeka polisi wanaodhulumu raia hawatasalimika hata kidogo, nitawashughulikia nanyi mtaona hebu nipeni miezi minne hivi.
“Baada ya tume hii mtaona… tangu niingie kwenye wizara hii nimeshaunda tume tatu ambazo matokeo yake nitayatoa hivi karibuni,” alisema Dk. Nchimbi na kuongeza kuwa hakuna waziri mpenda haki kama yeye na wananchi hawatampata wa kufanana naye.
“Mtampata wapi waziri kama mimi…(wote kicheko),” alisema waziri huyo ambaye kabla ya kupewa wizara hiyo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo aliyewaahidi waandishi kusimamia upatikanaji wa sheria mpya ya vyombo vya habari jambo lililokwama.
Alisema milango ipo wazi kwa raia kupeleka malalamiko yao huku akisisitiza kwamba hana tabia ya kupuuza kero za wananchi zinazowagusa askari polisi.
Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa amesema anasikitishwa kuona raia wakiendelea kuuawa na polisi bila kuchukuliwa hatua.
Dk. Malasusa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utetezi wa masuala ya Kiuchumi, Haki za Binadamu na Utunzaji wa Uumbaji, alisema hali hiyo inahatarisha amani na utulivu nchini.
“Inashangaza kuona uhai wa mwanadamu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu unakatishwa kikatili tena katika mazingira yasiyoashiria hatari,” alisema.
Alisema KKKT inaitaka serikali kukomesha mauaji ya aina hiyo yasiendelee na polisi wazingatie maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Taarifa hii imeandaliwa na Irine Mark na Efracia Massawe Dar, Joseph Senga, Iringa na Christopher Nyenyembe, Rungwe (TANZANIA DAIMA, 5 Septemba 2012)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO