Nimesikitishwa na kauli za jazba na mwangwi wa kiwewe za Mhe Dr. W Slaa alipokuwa Iringa juzi hadi kuniita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari n.k Hali hii inatia mashaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa kuhimili kukosolewa ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa yeyote hususani anapojinadi kuwa anaweza kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi.
Kauli zisizo na staha alizozitoa Dr Slaa dhidi yangu kama vile sifai hata uongozi wa kata zinadhihirisha mambo mawili:
-Dr Slaa ni dicteta. Hana uvumilivu. Ana hulka ya kujiskia kwamba mawazo yake hayapingwi.
-Ni mzushi asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu kushinda hoja. Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee uraisi kupitia chama chake mwaka juzi leo aseme sifai kuongoza hata kata kwasababu tu nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?
Niliyoyasema pale Karagwe majuzi katika uchambuzi wangu wa vyama vya siasa nchini ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na kuishambulia CCM na serikali zake lakini wanasau kuwa ili wawe mbadala kwa kuiongoza nchi hawana budi kurutubisha safu yao ya uongozi nawe na watu wakutosha kuweza kushika madaraka ya ngazi mbalimbali za uongozi wa Taifa. Kuukataa ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni nyembamba ni kujidanganya tu.Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo yote ya wananchi yanatokana na CCM ni kazi rahisi na ina mvuto wake kisiasa lakini mwanasiasa makini hana budi kwenda mbele zaidi ya hapo. Hana budi kutuambia wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo ya nchi. Ahadi za alinacha za tiba bure, elimu bure bila kuonyesha vyanzo halisi vya mapato ni porojo tu. Kusema kwamba raslimali za nchi kama vile gesi asilia, madini, makaa ya mawe, utalii zinatosha kuondoa umaskini ni nadharia tupu ambayo uhalisia wake hauna budi kubainishwa kwa mikakati dhahiri na thabiti ya kiutawala (uendeshaji) inayoweza kuchuma utajiri huo kwa ufanisi, kwa uendelevu na kwa faida ya wengi 1. Kuhusu mwenyekiti Mh Mbowe – MB
Katika hotuba yangu sikukejeli uzoefu wa Mhe Mbowe, wala sijasema Mhe Mbowe ni mcheza disko. Niliuchambua wasifu wa viongozi wa CHADEMA na kutamka uzoefu wa Mhe Mbowe katika vitega uchumi vya burudani hii siyo kudharau bali ni kutamka ukweli tu.Huwezi kuuelezea wasifu wa Mhe Mbowe bila kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani.Mmoja wa maraisi maarufu wa marekani (USA)alikuwa ni mcheza sinema Ronald Reagan.Na hapa Tanzania tulikuwa na mzee R. Kawawa ambaye alianzia katika tasnia ya uigizaji, kwa hiyo Mhe Mbowe au Dr.W. Slaa anaweza akawa Rais wetu kwa maana ya kupigiwa kura za uchaguzi wa demokrasia.Kumudu au kutoyamudu madaraka hayo ni suala tofauti. Tathmini yangu ilihusu safu nzima ya uongozi wa CHADEMA kwa ujumla wao.Ni safu nyembamba mno.
2. Kujiunga na CHADEMA
Kama alivyosema Dr. Slaa Chadema walifanya jitihada ya kunishawishi niingie CHADEMA 2010 na niwe mgombea wao wa Urais. Jambo hili nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu wangu wa karibu na nikabaini kwamba:-
-CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari kwasababu ni ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.
-Kutokana na yaliomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015 nilibaini mambo ya kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya majimbo. Sera ya majimbo inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na pia isiyo na tofauti kubwa ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali za nchi kama vile Marekani (USA). Kuleta majimbo Tanzania ambako kuna tofauti kubwa za kimaendeleo baina ya Kaskazini, Mashariki, kati, Kusini na Magharibi ni kusababisha nchi ichanike vipande vipande. Huduma bure za elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu na huduma bure za afya kwa wote ni ndoto na ni ghilba kwa wananchi. Isitoshe siamini kwamba kazi ya Serikali yoyote Duniani ni kuwalea Wananchi kwa umaskini huku ukiwaahidi huduma za bure badala ya kuwaendeleza wajitume na waongeze kipato ili wamudu gharama za maisha. Kwa hiyo nisingeweza kuwa mgombea Uraisi ndani ya chama ambacho itikadi zake za msingi sikubaliani nazo.
Baada ya hapo nisingeweza eti baada ya uchaguzi Mkuu niombe kugombea Uspika kupitia chama cha CHADEMA.
3. Kuhusu CCJ
Kama ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni miongoni mwa vyama vilivyonifuata mimi na baadhi ya wanasiasa wakati wa maandilizi ya uchaguzi mkuu. jambo hili si la siri wala la ajabu na Nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na kujiunga na chama kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini. Na kama Ningeridhika na mambo yao ningejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini sikufanya hivyo. Pia ni uzushi usio na msingi kunihusisha na uanzishaji wa chama hicho. Waanzilishi wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai, ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na chama chochote cha siasa.
4. Madai mengine
Eti nilitamka kwamba ningehamia chadema na Wabunge wa CCM 55 ni porojo za Dr. Slaa kama ulivyo usemi ningeihama CCM siku chache kabla ya kuvunjwa Bunge la 9.
Inashangaza kwa Dr Slaa kukejeli uendeshaji wa bunge la 9 ambalo ndilo lililowapa fursa watu kama yeye kujulikana na kujipatia umaarufu.
Haya madai ya mimi nikiwa Spika kukwamisha uchunguzi wa Meremeta na Richmond ni kutokana na hisia tu za chuki. Taratibu za Kibunge hazimwezeshi Spika kuwa Dikteta anayeamua nini kijadiliwe na nini kisijadiliwe. Yote yapo katika kanunu za Bunge. Maamuzi ya Bunge si lazima yawe ni ya Spika.
Kuhusu ofisi ya Mbunge jimboni Urambo mahasimu wangu ndani ya CCM na nje yake wameng’ang’ania kwa makusudi maalum kuiita ofisi ile kuwa ni ya Spika. Michoro yake na gharama zake hata ukijumuisha samani haifikii tarakimu za ajabu wanazotaja mahasimu wangu kujenga hoja istoshe ofisi hiyo haina maslahi yeyote binafsi kwangu Aidha viongozi wengine waliofikia hadhi za juu mathlani ya uwaziri mkuu nao wamejengewa majimboni ofisi zinazolingana na hiyo
Porojo nyingine binafsi kama vile kumuhusisha mke wangu kumpigia simu Dr Slaa kumsihi anisaidie kisiasa ni upuuzi wa aina yake unaodhihirisha umahiri wa Dr.Slaa katika siasa za kiwango cha chini.
5. HITIMISHO
Mimi nikiwa mwanasiasa mzoefu na mkongwe nimetoa ushauri na nitaendelea kutoa ushauri kwa makundi mbalimbali nchini.Kuniambia naingilia mambo ya CHADEMA ni kichekesho.Wakiwa wao ni chama cha siasa kinachoendesha harakati za kuwania kuchukua madaraka ya kuongoza nchi ambayo mimi ni raia wasitazamie kuwa sisi wapiga kura tutaacha kuwachambua.Wanalo tatizo kubwa la safu nyembamba mno ya uongozi, Kulingana na majukumu ya kuendesha nchi. Kujilinganisha na safu ya uongozi ya Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere ni mzaha wako wapi akina R.M Kawawa, Pauli Bomani, George Kahama, Amir Jamal, Solomoni Eliufoo, Tewa Saidi, Tewa Abdallah, Fundikira wa CHADEMA? Kutembea nchi nzima kuhamasisha chuki dhidi ya serikali iliopo madarakani ni jambo jepesi lakini Watanzania walio makini wanahitaji maelezo ya mipango mbadala ya uchumi kuinua hali za maisha yao na kuiona safu ya uongozi itakayowezesha kwa dhati kubuni na kusimamia mikakati endelevu ya kuondoa umaskini kujenga uchumi imara na kuimarisha umoja wa watanzania.
0 maoni:
Post a Comment