SITAKI polisi wazuie maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani. Sitaki wazuie maandamano ya vyama. Sitaki wapige na kujeruhi waandamanaji. Sitaki waue wanaofanya kazi ya kisiasa.
Jirani yangu hapa ananiambia, “…wanaua kwa bahati mbaya. Si kwa kukusudia.” Ninakataa.
Huwezi kuzuia maandamano kwa bahati mbaya. Huwezi kuswaga wananchi kwa kiboko kwa bahati mbaya. Hapana! Huwezi kupiga wananchi mabomu ya machozi kwa bahati mbaya.
Huwezi kufyatua risasi ya plastiki katikati ya wananchi waandamanaji wasio na silaha kwa bahati mbaya. Nasema huwezi! Huwezi kutwanga risasi ya moto katikati ya umati kwa bahati mbaya.
Huwezi kuendeleza vitisho kwa wananchi, viongozi wao na vyama vyao kwa bahati mbaya. Huwezi kujiapiza, kwa bahati mbaya, kuvuruga mikutano ya vyama vya siasa.
Huwezi kufinyanga na kuvaa sura ya ukatili wakati wa kubugudhi wananchi halafu ukasema ni bahati mbaya. Hapana.
Huwezi kutumwa, ukatii, ukafinyanga na kuvaa sura ya ukatili; ukashika silaha, ukafyatua bomo la machozi au risasi katikati ya wananchi – iwe ya plastiki au ya moto – halafu ukasema ni bahati mbaya.
Mbona hakuna bahati mbaya ya kushindwa kuua au bahati mbaya ya kukosa shabaha; lakini kuna bahati mbaya ya kufaulu kujeruhi na kuua? Tunavuja machozi na damu.
Nasema yote haya kwa kuwa polisi ni chombo cha serikali. Katika demokrasi, serikali huja na kuondoka. Leo kuna serikali hii. Kesho kuna serikali ile. Keshokutwa kuna serikali nyingine.
Hata katika udikiteta, serikali huja na kuondoka. Ama lidikiteta kuu litapinduliwa kwa mabavu kama linavyotawala, litazeeka, litalewa na kusambaratika akili na wenzake watachukua au litakufa.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, jeshi la polisi linabaki la serikali iliyoko madarakani. Hii ndiyo maana askari polisi hupaswa kuwa; na hasa kubaki waandilifu.
Hii ndiyo maana polisi wakaitwa walinzi wa raia na mali zao. Hii ndiyo sababu baadhi ya wananchi hujitolea kufanya kazi ya polisi – ulizi – wakati baadhi ya polisi wamelala na kukoroma.
Mlinzi wa raia hafanyi mambo kwa bahati mbaya. Mlinzi wa mali za raia haongozwi na bahati mbaya. Kukubali upolisi ni kukubali bahati nzuri ya kulinda raia na mali zao. Bahati mbaya inatoka wapi?
Upolisi unaingiliwa na wanaotaka kulindwa kuliko wengine. Wanaotaka kuiba haki za wengine. Wanaotaka kupora mali za wengine. Wanaotaka kuneemeka zaidi kuliko wengine.
Hapa ndipo upolisi unapochafuliwa. Ni hapa panapozaliwa kinachoitwa bahati mbaya. Sasa tukubali kwamba “bahati mbaya” ni moja ya kazi ya polisi.
Tunajadili haya kwa kuwa Tanzania imo katika hatua muhimu ya mabadiliko. Kuna vyama vya siasa vinapambana kuhakikisha utawala uliodumu kwa miaka 50 unapisha akili mpya na mipango mipya.
Akili iliyogota haikukwamisha elimu peke yake; biashara peke yake; usafiri peke yake, tiba peke yake; ilikwamisha pia mafao kwa wananchi wakiwamo polisi.
Mafao ya jamii ni mengi – siyo mishahara peke yake. Ukosefu wa mipango inayohakikisha kwamba mtumishi wa kima cha chini anastahili kuishi hata baada ya kustaafu, ni mipango ya kwenda kuzimu.
Ukosefu wa mipango na taratibu za kukuza kilimo cha mkulima mdogo – kwa ushindani tu wa kununua mazao yake ili achocheke kuongeza eneo, kutumia mbegu bora, mbolea na mbinu za kisasa ili aweze kupata zaidi na kuuza zaidi – ni kuita kifo kije haraka.
Mipango ya kufuga wananchi kama kuku wapumbavu aina ya broila; kwa kuwazuia kusema au kuzima nyenzo zao za mawasiliano na hivyo kunyamazisha umma na kuziba mifereji yake ya fikra, ni kuandaa jahanamu kwa waliohai.
Kushiriki, kuruhusu au kufumbia macho wizi, uporaji, ufisidi fedha na raslimali za umma na halafu kukaa kimya na kupakatana na wezi na mafisadi, huku ukijiita mtawala; siyo tu kudharau akili ya umma uliohai, bali pia ni kuangamiza umma huo.
Wanapotokea wenye hoja mpya, sera mpya, muono mpya – wakitafuta mabadiliko katika utawala wa siasa, uchumi na utamaduni wa wengi waliopoteza matumaini zamani – inatoka wapi “bahati mbaya” ya polisi kuwapiga?
Au ni bahati mbaya kwamba polisi wametumwa au wameamrishwa na wakubwa zao, kwenda kuzima nyota iliyoanza kutoa nuru kwa jamii iliyoishi gizani kwa miaka nendarudi?
Iko wapi bahati mbaya isoyoona umuhimu wa mabadiliko, tena kwa njia bora ya majadiliano na umma?
Nani asiyeona umuhimu wa wananchi kufikia hatua wakasema, tena katika mazingira ya amani: nataka huyu aniongoze na sitaki yule anitawale?
Tunavuja machozi na damu. Inatoka wapi bahati mbaya ya kuzima matumaini ya umma? Polisi, acheni wananchi watafute ukombozi wao na wenu pia.
IMEANDIKWA NA: NDIMARA TEGAMBWAGE KUPITIA TANZANIA DAIMA
0 maoni:
Post a Comment