TUME ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kukamilisha majukumu yake ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo nchi kuwa na Katiba Mpya ifikapo Aprili, mwaka 2014.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba, aliwaeleza mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa pamoja na changamoto zilizopo, dhamira hiyo ya tume ipo palepale.
Mawaziri hao, Mathias Chikawe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Abubakar Khamis Bakari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walitembelea ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana, ili kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo.
“Tunafahamu hii ni changamoto, lakini tumeikubali na tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kama taifa tunakuwa na Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, mwaka 2014,” alisema Jaji Warioba.
“Ukiangalia hali ya kisiasa, tunadhani itakuwa vizuri tukiwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema Jaji Warioba.
Pamoja na nia hiyo, Jaji Warioba pia aliwaeleza mawaziri hao kuwa kwa sasa tume yake imejikita katika kukusanya maoni binafsi ya wananchi na kuwa baada ya hatua hiyo tume itaanza kukusanya maoni ya makundi mbalimbali kama vyama vya siasa, taasisi za kidini, jumuiya za kitaaluma na asasi za kiraia.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alieleza kufurahishwa na utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo na kuahidi serikali itaendelea kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.
Source: Tanzania Daima
HABARI ZAIDI KWA MUJIBU WA MSEMAJI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kukamilisha majukumu ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 na hivyo nchi kuwa na Katiba Mpya ifikapo mwezi Aprili, 2014.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Joseph Warioba amewaeleza Mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa pamoja na changamoto zilizopo, dhamira hiyo ya Tume ipo palepale.
Mawaziri hao, Bw. Mathias Chikawe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bw. Abubakar Khamis Bakari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walitembelea ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba (Jumatatu, Septemba 3, 2012) ili kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume hiyo.
“Tunafahamu hii ni changamoto, lakini tumeikubali na tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kama Taifa tunakuwa na Katiba Mpya ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014,” alisema Jaji Warioba katika mkutano Mawaziri hao ambao walitembelea vitengo vya Utafiti na Taarifa Rasmi (Hansard).
Jaji Warioba amesema kuwa lengo hilo la Tume linaongozwa na sababu kuu mbili ambazo ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambayo inaipa Tume muda wa miezi 18 kutekeleza majukumu yake. Tume hiyo ilianza kazi mwezi Mei mwaka huu (2012).
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, sababu ya pili ni hali ya kisiasa ilivyo hapa nchini ambayo amesema Taifa linahitaji kuwa na mwafaka wa kisiasa kupitia Katiba kabla ya mwaka 2015.
“Ukiangalia hali ya kisiasa, tunadhani itakuwa vizuri tukiwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Angellah Kairuki, Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu wa Tume Bw. Casmir Kyuki.
Pamoja na nia hiyo, Jaji Warioba pia aliwaeleza Mawaziri hao kuwa kwa sasa Tume yake imejikita katika kukusanya maoni binafsi ya wananchi na kuwa baada ya hatua hii, Tume itaanza kukusanya maoni ya makundi mbalimbali kama vyama vya siasa, taasisi za kidini, jumuiya za kitaaluma na asasi za kiraia.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias Chikawe alieleza kufurahishwa na utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.
“Kwa niaba ya Serikali napenda nikuhakikishia tena kuwa tutaendelea kuwapa kila aina ya ushirikiano mtakaouhitaji ili mtekeleze majukumu yenu kwa ufanisi,” alisema Waziri Chikawe.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Abubakar Khamis Bakari aliwapongeza watendaji wa Sekretarieti hiyo kwa ubunifu
“Huu mfumo wa teknolojia wa kupokea na kuyafanyia kazi maoni ya wananchi ni mzuri na ingekuwa umetengenezwa na mtaalam kutoka nje, ingekuwa gharama kubwa,” alisema Waziri huyo wakati akizungumzia mfumo wa kompyuta ulitengenezwa na wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Tume hiyo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba hivi sasa inaendelea na kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya kupitia mikutano katika mikoa saba ya Morogoro, Lindi, Katavi, Kigoma, Mwanza, Mbeya na Ruvuma. Tayari Tume hiyo imeshakusanya maoni katika mikoa ya Tanga, Manyara, Kagera, Shinyanga, Dodoma, Pwani, Kusini Unguja na Kusini Pemba.
Ismail Ngayonga,
Information officer,
Constitutional Review Commission (Tanzania),
PO Box 1681,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2133425,
Fax: +255 (0) 22 2133442,
Mobile: +255 (0) 717 084252
Email: ngayongaismail@yahoo.com,
Website: www.katiba.go.tz
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba (kushoto) akiongea na Mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mathias Chikawe (kulia) na Abubakar Khamis Bakari (kulia kwa Jaji Warioba) nje ya ofisi za Tume mara baada ya Mawaziri kutembelea ofisi za Tume leo (Jumatatu, Sept. 3, 2012). Katikati ni Naibu wa Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki na wengine ni watendaji kutoka Tume na Wizara za Katiba na Sheria
Mkuu wa Kitengo cha Taarifa Rasmi katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba Hanifa Masaninga (kushoto) akitoa maelezo jinsi sauti zenye maoni ya wananchi zilizorekodiwa mikoani zinavyofanyiwa kazi kwa Mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mathias Chikawe (kwa pili kulia) na Abubakar Khamis Bakari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (watatu kushoto) na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki (kulia). Wa pili kushoto ni Katibu wa Tume Assaa Rashid
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mohammed Khamis Hamad (kulia) akiwaeleza jinsi maoni ya wananchi yanavyopokelewa kutoka katika mitandao ya kijamii Mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw.Abubakar Khamis Bakari (kushoto), Bw. Mathias Chikawe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Naibu wake Angellah Kairuki (watatu kushoto). PICHA ZOTE NA TUME YA KATIBA
0 maoni:
Post a Comment